Nyongeza Ya Kwanza

Program ya Wananchi: Programu ya Siasa na Katiba ya Chama cha Umma Party

Chama cha Umma Party cha Zanzibar ni chama cha wananchi, kilichoandaliwa kuwa ni kiongozi mwenye uelewa wa watu wanaokandamizwa wa Zanzibar. Kinawakilisha maslahi mapana ya Waafrika ambao hivi sasa wanabeba mzigo wa ukandamizwaji wa kiuchumi unaosababishwa na ukoloni wa kigeni na umwinyi wa ndani ya nchi. Wakati hivi sasa inapambana bila ya kuchoka dhidi ya ukandamizaji wa kibeberu, lengo lake hatimaye ni kujenga usoshalisti; yaani uangamizaji wa mfumo wa mtu mmoja kumnyonya mtu mwengine.

‘Programu ya Wananchi’ ya Chama cha Umma Party ni mbiu ya mgambo kwa ajili ya kuchukua hatua, hatua madhubuti, za kujenga na kuhakikisha mabadiliko ya haraka ya mfumo unaochukiza ambao mpaka hivi sasa umewadhalilisha wananchi wa Zanzibar, kimwili na kiakili na kuwafanya kuwa katika hali isiyo ya kibinadam. Nafasi ya mfumo huu unaochukiza lazima ichukuliwe na mfumo wa kisoshalisti ambao ndio pekee utaoweza kuhakikisha kuwepo kwa heshima ya kweli ya binadamu.

Uanachama katika Chama cha Umma Party unahitaji kuwa na moyo wa kujitolea. Kwa mwanachama wa Chama cha Umma Party hakuna kazi isiyowezekana. Woga hauna nafasi miongoni mwetu na mateso ya mtu binafsi hayawezi kutuzuia katika kupigania lengo letu ambalo ni usoshalisti. Chama cha Umma Party hakiwezi kuvumilia kuwepo kwa ubinafsi miongoni mwa wanachama wake na kitakuwa macho dhidi ya kujipenyeza kwa mafisadi kama hao. Chama cha Umma Party ni chama makini cha umma wa wananchi na wanachama wake wanatarajiwa kuutumikia umma kwa moyo wa kujitolea bila ya kutegemea kupata zawadi yoyote au manufaa binafsi.

Kukosoa na kujikosoa lazima kufanyike bila ya woga na kwa mujibu wa nidhamu ya Chama. Kwa hivyo, kukosoa kusikofuata nidhamu hakutavumiliwa. Makosa lazima yakosolewe kwa madhumuni ya kuyasahihisha na siyo kwa nia ya kujionyesha. Chama lazima kipinge tabia ya mtu kuwa na kiburi.

Wanachama wa Chama cha Umma Party, wakiwa watumishi wa umma, lazima wauhudumie umma kwa dhati. Lazima kila wakati wawe karibu na umma mkubwa wa watu, wayaelewe mahitaji yao na wawasaidie katika kutatua matatizo yao.

Kila mwanachama lazima afanyekazi bila ya kuchoka ili kuimarisha umoja na mshikamano wa Chama. Ni kwa umoja madhubuti tu ndipo tutakapoweza kuutumikia umma kikwelikweli na kuleta mabadiliko ya kijamii ambayo yatakuwa ni kwa manufaa ya umma kwelikweli.

Chama kinamtaka kila mwanachama wake kufanyakazi kwa bidii ili kuitekeleza Programu hii na maamuzi yote ya Chama ili kuangamiza moja kwa moja ubepari, umwinyi, ubeberu na ukoloni mamboleo kutoka katika ardhi ya nchi yetu.

Katiba ya Chama cha Umma Party cha Zanzibar

JINA: Chama kitaitwa UMMA PARTY

Malengo na Madhumuni (Kitaifa)

  1. Uhuru sasa hivi na maendeleo ya Zanzibar kwa misingi ya usoshalisti.
  2. Kuwa mbele katika kuondoa aina zote za ukandamizaji, mfumo wa mtu mmoja kumnyonya mwengine na kuanzisha jamii ya kisoshalisti.
  3. Kuleta umoja wa watu wote wa Zanzibar na watu wa Afrika ya Mashariki na wa Afrika yote kwa misingi ya Umajumui wa Kiafrika.
  4. Kufanyakazi pamoja, na kwa maslahi ya Vyama vya Wafanyakazi katika harakati za pamoja za kisiasa na harakati nyengine kwa mujibu wa katiba na Pogramu ya kisiasa ya Chama.
  5. Kuendeleza ukombozi wa kisiasa, kijamii, kiuchumi na kiutamaduni wa watu, hasa wale ambao wanategemea moja kwa moja bidii yao kwa kutumia mikono au akili kujikimu kimaisha.
  6. Kuanzisha dola la kisoshalisti ambalo watu wote, wanaume na wanawake watakuwa sawa na watakuwa na fursa sawa na hapatokuwepo unyonyaji wa kibepari.

Kimataifa

  1. Kufanyakazi na wananchi wengine, wanademokrasia na vyama vya kisoshalisti katika Afrika na mabara mengine kwa madhumuni ya kuangamiza ubeberu, ukoloni, ukabila na aina zote za ukandamizaji wa kitaifa na wa kikabila na hali ya kutokuwepo usawa wa kiuchumi miongoni mwa mataifa, makabila na watu wote na kuunga mkono harakati zote za kuleta amani duniani.
  2. Kuunga mkono madai ya wananchi ya kuwepo kwa Shirikisho la Afrika ya Mashariki na Umajumui wa Waafrika kwa kuendeleza harakati za pamoja miongoni mwa watu wa Afrika.
  3. Mtu yeyote anayeikubali Programu na Katiba ya Chama, iliyomo na anayefanyakazi katika mojawapo ya jumuiya za Chama, anafuata maamuzi ya Chama na analipa ada za Chama, anaweza kuwa mwanachama wa chama hiki.
  4. Wajibu wa mwanachama utakua kama ifuatavyo:

(a) Kujaribu kuinua kiwango cha uwelewa wake na kuielewa misingi ya usoshalisti na nadharia ya mapinduzi ya Afrika.

(b) Kufuata kwa uadilifu nidhamu ya Chama, kushiriki kikamilifu katika maisha ya kisiasa ya ndani ya Chama na mapambano ya watu wa Zanzibar, kutekeleza kwa vitendo sera na maamuzi ya Chama na kupambana dhidi ya kitu chochote, ndani na nje ya Chama, kinachopingana na maslahi ya Chama.

(c) Kuutumikia umma wa watu, kuimarisha uhusiano wa chama na umma huo, kujifunza mahitaji yao na kutoa taarifa kuhusu mahitaji hayo kwa wakati, kuwaelezea sera ya Chama.

(d) Kuonyesha mfano katika kufuata nidhamu ya Chama na ya jumuiya zetu, kuielewa vizuri nafasi yake ndani ya chama na kuonyesha mfano katika nyanja zote za kazi za kuleta maendeleo.

 5. Haki za mwanachama zitakuwa kama ifuatavyo:

(a) Kushiriki katika majadiliano huru na ya haki katika mikutano ya Chama na machapisho ya Chama juu ya matatizo yanayohusiana na utekelezaji wa sera za Chama.

(b) Kuchagua na kuchaguliwa ndani ya Chama,

(c) Kuwasilisha mapendekezo au taarifa katika kikao chochote cha chama, hadi kufikia katika kiwango cha pamoja na Kamati Kuu.

(d) Kumkosoa mtumishi yeyote wa Chama katika vikao vya Chama.

6. Mtu anaweza kukubaliwa kuwa mwanachama baada ya kufikia umri wa miaka 18 tu.

 

Maombi ya uwanachama kwa mtu mmoja mmoja yatafanywa kwa fomu maalumu ambayo itajazwa na mwombaji na kupitishwa kwa Katibu wa Tawi ili maombi yafikiriwe na kamati yake kama yakubaliwe au la. Baada ya kukubaliwa kila mwanachama atapatiwa kadi ya uanachama na kadi ya ada.

Ada ya kukubaliwa uanachama: Kila mwanachama binafsi wa Chama ataombwa alipie ada ya kuandikishwa uanachama ya shilingi mbili pale anapojiunga.

Ada ya kila mwezi: Kila mwanachama binafsi wa Chama atalipa ada ya kila mwezi ya senti hamsini katika Chama kwa kupitia tawi lake la Chama.

Uanachama (uanachama shirikishi)

Wanachama wanaoshirikishwa watakuwa ni wafuatao:

(a) Vyama vya Wafanyakazi pamoja na Vyama vya Watumishi wa Serikali;

(b) Vyama vya Wakulima na vya Kilimo;

(c) Vyama vya Ushirika, Vyama Vikuu na Vyama vingine kama hivyo;

(d) Vyama vya Kiweledi, Mafundi Mchundo na Mafundi Mitambo;

(e) Vijana, wanafunzi na vyama vya michezo;

(f) Vyama vya Wanawake

i) Vyama vyote vya aina hiyo lazima viyakubali madhumuni, sera na programu ya Chama.

ii) Lazima viwe, kwa maoni ya Kamati Kuu, vyama vya kuaminika.

iii) Chama kinachotaka kushirikishwa kitawasilisha azimio kuhusiana na ombi hilo, ambalo liwe limetiwa saini na Mwenyekiti na Katibu wake.

iv) Kila chama baada ya kukubaliwa kushirikishwa lazima kilipe ada ya kushirikishwa ya shilingi 25.

Muundo wa Chama

1. Muundo wa Chama utakuwa kwa misingi ya demokrasia iliyodhibitiwa, udhibiti ulio chini ya misingi ya kidemokrasia chini ya uongozi uliodhibitiwa. Misingi muhimu ni kama ifuatayo:

(a) Uongozi wa Chama katika ngazi zote ni lazima uchaguliwe;

(b) Uongozi wa Chama katika ngazi zote ni lazima utoe taarifa baada ya kila muda fulani uliopangwa kwa vikao vya chini yake vya Chama vinavyowachagua;

(c) Kila mwanachama mmoja mmoja ataheshimu kikao cha chama kinachomhusu; wachache watawaheshimu wengi; kikao cha chini cha Chama kitaheshimu kikao cha juu cha Chama na vikao vyote vya majimbo vya Chama vitaiheshimu Kamati Kuu;

(d) Nidhamu ya Chama itafuatwa kwa uadilifu na maamuzi ya Chama kutekelezwa bila ya pingamizi.

2. Vikao vya Chama vitaundwa kwa mujibu wa mgawanyiko wa kijiografia.

3. Muundo wa Chama utakuwa kama ifuatavyo:

(a) Kwa Zanzibar kwa jumla, kutakuwepo na Mkutano Mkuu wa Chama wa Taifa, Kamati Kuu na Mkutano wa Chama wa Taifa;

(b) Kwa Unguja na Pemba, kila sehemu itakuwa na Mkutano Mkuu wa Chama wa Kisiwa, Kamati ya Chama ya Kisiwa na Mkutano wa Chama wa Kisiwa;

(c) Kwa majimbo kutakuwepo na Mkutano Mkuu wa Chama wa Jimbo, Kamati ya Chama ya Jimbo na Mkutano wa Chama wa Jimbo;

(d) Kwa kila kiwanda, mtaa, ofisi na skuli kutakuwepo na mkutano wa wanachama wote, Kamati ya Chama ya Tawi na Mkutano wa Chama wa Tawi.

4. Chombo cha juu kabisa cha uongozi cha Tawi la Chama kitakuwa ni mkutano wa wanachama wote wa tawi. Chombo cha juu kabisa cha uongozi cha mji, jimbo au kisiwa kitakuwa ni Mkutano Mkuu wake. Chombo cha juu kabisa cha uongozi cha Chama chote kitakuwa ni Mkutano Mkuu wa Chama wa Taifa. Katika kipindi cha baina ya Mikutano Mikuu katika ngazi zote, Kamati za Chama zilizochaguliwa na vikao husika ndizo zitakazokuwa vyombo vya juu kabisa vya uongozi vya ngazi zinazohusika.

5. Vyombo vya uongozi vya Chama katika ngazi zote vitaanzishwa kwa njia ya uchaguzi kila inapowezekana. Vitachaguliwa na Mkutano wa Chama au kuteuliwa na kikao cha juu kabisa cha Chama pale tu hali halisi itakapokuwa hairuhusu kuitishwa kwa mkutano wa wanachama wote au Mkutano Mkuu wa Chama.

6. Uchaguzi wa Kamati ya Chama katika ngazi yoyote ile utafanyika ama kwa kura ya siri au kwa kura ya wazi kutoka kwenye orodha ya wagombea, ukiwepo uhakika kuwa wapiga kura watakuwa na haki ya kumkosoa mgombea yeyote na kumbadilisha mgombea yeyote aliye kwenye orodha.

7. Ili kufikisha au kujadili maamuzi muhimu ya vikao vya juu vya Chama, au ili kupitia au kupanga kazi yake, kikao cha Chama katika ngazi yoyote kinaweza kufanya mikutano ya namna mbalimbali ya makada wake au wanaharakati wake.

8. Kabla maamuzi hayakufikiwa, kila mwanachama anaweza kuendesha ndani ya Chama na kwenye mikutano ya Chama majadiliano yaliyo huru na kwa urefu ili kueleza maoni yake juu ya sera ya Chama na juu ya masuala mengine mbalimbali. Hata hivyo, uamuzi utakapofikiwa, ni lazima uheshimiwe na wote na utekelezwe bila ya pingamizi.

9. Ili kuendeleza nguvu za ubunifu za wanachama, kuimarisha nidhamu ambayo itakuwa ni ya uelewa na siyo nidhamu ya kulazimishwa, ili kuhakikisha kuwepo kwa uongozi sahihi wa Chama na kudumisha na kuimarisha udhibiti kwa misingi ya demokrasia, vyombo vya uongozi vya vikao vya Chama katika ngazi zote vitafanya kazi zao kwa mujibu wa misingi ya demokrasia ya ndani ya Chama.

10. Vikao vya Chama katika ngazi zote vitahakikisha kuwa magazeti yaliyo chini ya uongozi wao yanatangaza maamuzi na sera za vikao vya juu vya Chama na ya chombo kikuu cha Chama.

11. Juu ya suala la kiwango cha kitaifa, kabla ya Kamati Kuu haikutoa tamko lolote au kufanya uamuzi wowote, idara za vikao vya chini au watumishi wao wenye dhamana hawatakiwi kutoa tamko lolote au kufanya uamuzi wowote kama wapendavyo, ijapokuwa wanaweza kuwa na majadiliano ya faragha au kutoa mapendekezo kwa Kamati Kuu.

12. Kuanzishwa kwa kikao kipya cha Chama kutaidhinishwa na kikao cha juu zaidi kinachohusika.

13. Ili kufanya shughuli zozote za kawaida, Kamati ya Chama katika ngazi yoyote, chini ya uongozi wake, inaweza kuanzisha idara au tume ili kufanya shughuli za Chama na kufanya kazi miongoni mwa umma, kama hali halisi itakavyohitaji. Kamati ya Chama katika ngazi yoyote, inaweza kuanzisha tume ya muda au idara ili kufanya shughuli mahasusi za muda mfupi.

 

Kikao cha juu cha Chama

1. Mkutano Mkuu wa Chama wa Taifa

Mkutano Mkuu wa Chama wa Taifa utaamuliwa na kuitishwa na Kamati Kuu. Katika hali ya kawaida utaitishwa kila mwaka. Katika hali isiyokuwa ya kawaida, unaweza ama kuahirishwa au kuitishwa mapema zaidi kama Kamati Kuu itakavyoamua.

Ikiwa vikao vya chini vya Chama vinavyowakilisha zaidi ya nusu ya wanachama wote vitaomba uitishwe Mkutano Mkuu wa Chama wa Taifa, Kamati Kuu itafanya hivyo.

Mkutano Mkuu wa Chama wa Taifa utatambuliwa kuwa ni halali ikiwa tu utahudhuriwa na wajumbe wanaowakilisha zaidi ya nusu ya wanachama wote.

Idadi ya wajumbe kwenye Mkutano Mkuu wa Taifa na utaratibu wa kuchaguliwa kwao utaamuliwa na Kamati Kuu.

Kazi na madaraka ya Mkutano Mkuu wa Chama wa Taifa yatakuwa kama ifuatavyo:

(a) Kusikiliza na kupokea, kujadili, na kuridhia taarifa zitakazowasilishwa na Kamati Kuu na vyombo vingine;

(b) Kuamua kuhusu na kufanya marekebisho ya programu ya Chama na katiba ya Chama;

(c) Kuamua kuhusu mtazamo wa kimsingi na sera ya Chama;

(d) Kuchagua wajumbe wa Kamati Kuu.

 

 2. Kamati Kuu

Idadi ya wajumbe wa Kamati Kuu itaamuliwa na Mkutano Mkuu wa Chama wa Taifa.

Zinapotokea nafasi zilizo wazi katika Kamati Kuu zitajazwa na wajumbe wa muda wa Kamati Kuu kwa utaratibu wa kufuata ngazi za vyeo.

Kamati Kuu itakiwakilisha Chama katika mahusiano yake na vyama vyengine vya siasa na taasisi nyengine, itaanzisha vyombo vya Chama na kuelekeza shughuli zao na kuwa na madaraka ya mgawanyo wa watumishi na mgawanyo wa fedha.

Kamati Kuu itaitishwa na Kamati Kuu ya Siasa kwa ajili ya kukutana katika kikao cha wazi mara moja kila mwezi. Hata hivyo, Kamati Kuu ya Siasa inaweza kuahirisha au kuitisha kikao mapema kulingana na hali halisi. Wajumbe wa muda wa Kamati Kuu wanaweza kuhudhuria kikao cha wazi na wana haki ya kutoa maoni yao.

3. Kamati Kuu ya Siasa

Katika kikao cha wazi, Kamati Kuu itachagua Kamati Kuu ya Siasa, Sekretariati na Mwenyekiti wa Kamati Kuu.

Kamati Kuu ya Siasa itakuwa ndiyo chombo cha juu cha uongozi cha Chama na kitaongoza shughuli zote za Chama katika kipindi cha baina ya mikutano ya wazi ya Kamati Kuu.

Sekretariati: Sekretariat; itashughulikia kazi za kila siku za Kamati Kuu kwa mujibu wa maamuzi ya Kamati Kuu ya Siasa.

Mwenyekiti: Mwenyekiti wa Kamati Kuu atakuwa wakati huo huo ndiye Mwenyekiti wa Kamati Kuu ya Siasa na wa Sekretariat kuu ya Chama.

Kamati Kuu, kwa mujibu wa mahitaji ya kazi zake, itaanzisha idara (kama vile Idara ya Mipango, Idara ya Parapaganda, n.k) tume (kama vile Tume ya Vyombo vya Habari ya Chama, n.k) na vyombo vyengine ili kufanyakazi katika nyanja zao husika na kufanyakazi chini ya maelekezo na usimamizi wa Kamati Kuu ya Siasa, Sekretariati na Mwenyekiti wa Kamati Kuu.

4. Mikutano Mikuu ya Chama ya Taifa

Katika kipindi cha baina ya Mikutano Mikuu ya Chama ya Taifa Kamati Kuu inaweza kuitisha Mikutano kadha ya Taifa itakayokuwa na wawakilishi kutoka katika kamati za chini za Chama kujadili na kuamua kuhusu masuala yanayohusiana na sera za Chama na hali halisi ya wakati husika.

Wawakilishi wa Mkutano Mkuu wa Chama wa Taifa watachaguliwa katika mikutano ya wazi ya Kamati za Chama za Kisiwa na Kamati nyengine za Chama ambazo zipo moja kwa moja chini ya Kamati Kuu.

Mkutano Mkuu wa Chama wa Taifa lazima uhudhuriwe na wawakilishi kutoka zaidi ya nusu ya Kamati zote za Kisiwa.

Mkutano Mkuu wa Chama wa Taifa utakuwa na madaraka ya kuwaondoa wajumbe kamili au wajumbe wa muda wa Kamati Kuu walioshindwa kutekeleza majukumu yao, na kuchagua katika uchaguzi mdogo, sehemu ya wajumbe wa muda wa Kamati Kuu ilimradi tu idadi ya wajumbe waliochaguliwa kwa namna hiyo kwa wakati wowote ule wa mkutano haitazidi humusi ya jumla ya wajumbe wote kamili na wa muda wa Kamati Kuu.

Maamuzi ya Mkutano Mkuu wa Chama wa Taifa na kuwaondoa au kuwachagua wajumbe kamili au wa muda wa Kamati Kuu katika mkutano huo, kutaanza baada ya kuridhiwa na Kamati Kuu tu.

Maamuzi yote ya Mkutano Mkuu wa Chama wa Taifa, ambayo yameridhiwa na Kamati Kuu, lazima yatekelezwe na vikao vyote vya Chama.

Vikao vya Chama vya Kisiwa

Mkutano Mkuu wa Chama wa Kisiwa na Kamati ya Chama ya Kisiwa wataukubali uongozi wa Kamati Kuu au chombo kinachoiwakilisha Kamati hiyo.

1. Mkutano Mkuu wa Chama wa Kisiwa

Mkutano Mkuu wa Unguja au Pemba utaitishwa kila mwaka na Kamati ya Chama ya Kisiwa. Katika hali zisizokuwa za kawaida, Kamati ya Chama ya Kisiwa inaweza ama kuuahirisha mkutano huo au kuitisha mkutano huo mapema zaidi. Kamati ya Chama ya Kisiwa lazima iitishe Mkutano Mkuu kama huo baada ya kuombwa na zaidi ya nusu ya vikao vya Chama vilivyo chini yake au vyombo vinavyoviwakilisha vikao hivyo.

Idadi ya wajumbe katika Mkutano Mkuu wa Kisiwa, na utaratibu wa kuchaguliwa kwao, utaamuliwa na Kamati ya Chama ya Kisiwa, baada ya kuidhinishwa na Kamati Kuu au chombo kinachoiwakilisha Kamati hiyo.

Mkutano Mkuu wa Chama wa Kisiwa, utasikiliza na kupokea, utajadili na kuridhia taarifa zinazowasilishwa na Kamati ya Chama ya Kisiwa na vyombo vingine vya Chama vya kisiwa husika, na utachagua wajumbe wa Kamati ya Chama ya Kisiwa na wajumbe wa kwenye Mkutano Mkuu wa Chama wa Taifa

2. Kamati ya Chama ya Kisiwa

Kamati ya Chama ya Kisiwa ya Unguja au ya Pemba, wakati wa mkutano wake wa wazi, itachagua Kamati yake ya Kudumu, Katibu wake na Katibu wake msaidizi ili kufanya shughuli za kila siku za Kamati hiyo. Katibu wa Kamati ya Kisiwa ataidhinishwa na Kamati Kuu. Kamati ya Chama ya Kisiwa itakutana kwa mkutano wake wa wazi, kwa uchache mara moja baada ya kila miezi sita.

Kamati ya Chama ya Kisiwa itatekeleza katika kisiwa hicho maamuzi ya Mkutano Mkuu wa Chama wa Kisiwa na ya vyombo vya Kitaifa, itaanzisha vikao mbalimbali vya Chama, itapanga watumishi wa Chama na matumizi ya fedha na kuelekeza fikra za Chama katika asasi zisizokuwa za kichama.

3. Mkutano wa Chama wa Kisiwa

Katika kipindi cha baina ya mikutano Mikuu ya Chama ya Kisiwa, Kamati ya Kisiwa ya Chama inaweza kuitisha idadi kadha ya Mikutano ya Chama ya Kisiwa itakayokuwa na wawakilishi kutoka katika Kamati za Chama za majimbo na Kamati nyengine za Chama ambazo zipo moja kwa moja chini yake, ili kujadili na kuamua juu ya matatizo yanayohusiana na kazi za Chama ndani ya kisiwa husika.

Mkutano wa Chama wa Kisiwa utakuwa na madaraka ya kuwaondoa na kuwachagua katika uchaguzi mdogo, baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Kisiwa, ilimradi tu idadi ya wajumbe walioondolewa au wajumbe wapya waliochaguliwa namna hiyo, haitazidi robo ya wajumbe wote wa Kamati hiyo. Maamuzi yatakayochukuliwa katika Mkutano wa Chama wa Kisiwa, na kuondolewa au kuchaguliwa kwa wajumbe wa Kamati ya Kisiwa na mkutano huo, yataanza baada ya kuridhiwa na Kamati ya Kisiwa tu.

Vikao vya Chama vya Jimbo na Mji

Kanuni zinazotawala vikao na kazi za chama katika jimbo au mji zitakuwa ni zile zile zinazotawala vikao na kazi za Chama katika kisiwa kama ilivyoelezwa hapo juu. Kila mojawapo itakuwa chini ya uongozi wa kikao cha Chama cha juu yake.

Kikao cha Msingi cha Chama

Kikao cha Chini cha msingi cha Chama kitakuwa ni Tawi la Chama. Chama kitafungua matawi katika miji yote na mashamba. Tawi litakuwa kwa uchache na wanachama 25. Kila tawi litaongozwa na Kamati ya Chama ya Tawi ambayo itachaguliwa kila mwaka katika mkutano mkuu wa Tawi.

Tawi la Chama litajitahidi kujenga mshikamano wa karibu baina ya Chama na umma wa watu. Tawi la Chama litakuwa na majukumu yafuatayo.

(a) Kufanya parapaganda na kazi ya kuuandaa umma ili kuweza kukubalika kwa msimamo unaoelezewa na chama na maamuzi ya vikao vya juu vya Chama;

(b) Kila wakati kutilia maanani hisia na matakwa ya umma, kuunga mkono hisia na matakwa hayo katika vikao vya juu vya Chama, kuzingatia maisha ya kisiasa, ya kiuchumi na ya kiutamadani ya wananchi na kuuandaa umma ili kutatua matatizo yao;

(c) Kuingiza wanachama wapya, kukusanya ada za Chama, kukagua na kuthibitisha kumbukumbu za wanachama;

(d) Kuwaelimisha wanachama na kuandaa mafunzo yao.

Nidhamu

Vikao vya Chama katika ngazi zote vinaweza kuchukua hatua za kinidhamu zifuatazo, kwa mujibu wa hali halisi, dhidi ya kushindwa kutekeleza maamuzi ya chombo cha juu cha Chama au maamuzi ya Kamati Kuu au dhidi ya ukiukaji wa katiba ya Chama au nidhamu ya Chama.

(a) Hatua za kinidhamu kwa Chama chote zitakuwa: karipio kali, kufanyiwa marekebisho madogo katika chombo chake cha uongozi, kufukuzwa kwa uongozi wake wa juu na kuteuliwa chombo cha muda cha uongozi, au kukivunja chama chote na kuandikishwa tena kwa wanachama wake.

(b) Hatua za kinidhamu kwa mwanachama zitakuwa: kufahamishwa au kupewa onyo kwa njia za onyo la faragha, kufahamishwa au kupewa onyo hadharani, kuondolewa katika dhamana aliyopangiwa, kuwekwa katika kipindi cha majaribio, au kufukuzwa kutoka katika Chama.

Kama mjumbe au mjumbe wa muda wa Kamati Kuu ya Chama atakiuka kwa kiasi kikubwa nidhamu ya Chama, Kamati Kuu itakuwa na madaraka ya kumwondoa kutoka katika Kamati hiyo au hata kumfukuza kutoka katika Chama. Hatua kama hizo lazima ziidhinishwe na thuluthi mbili ya wajumbe wote wa Kamati Kuu kabla ya kuanza kutumika.

Mwanachama au kikao cha Chama ambacho hatua za nidhamu zimechukuliwa dhidi yake, lazima aelezwe sababu. Za kuchukuliwa hatua hizo. Mwanachama yeyote au kikao chochote cha aina hiyo, atakayedhani hatua ya kinidhamu iliyochukuliwa dhidi yake si ya halali anaweza kuupinga uamuzi huo na kuomba kesi yake ifikiriwe upya, au anaweza kukata rufaa kwenye kikao cha juu cha Chama. Vikao vya Chama vya ngazi husika vitawasilisha rufaa kama hizi bila ya kuchelewa. Ni marufuku kuzichelewesha au kuzikalia rufaa kama hizo. Kufukuzwa kutoka katika Chama ndiyo adhabu kubwa kuliko adhabu zote za kinidhamu za ndani ya Chama. Vikao vyote vya Chama vitachukua hadhari kubwa katika kuchukua au kuidhinisha hatua kama hiyo na vitamsikiliza mwanachama husika kwa makini na kuchunguza hali ya makosa yake.

Madhumuni chanya ya Chama katika kupendekeza au kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya mwanachama yatakuwa ni kuwaelimisha wanachama na umma wa watu pamoja na mwanachama husika na siyo kushajiisha tabia ya kuonyesha uwezo wa mtu binafsi au kuadhibu. Kukosolewa na kuchukuliwa hatua za kinidhamu kwa wanachama waliofanya makosa kuna nia ya kuwasaidia kusahihisha makosa yao pamoja na kuwa onyo kwa wengine.

Fedha za Chama

Chama kitapata fedha zake kutokana na ada za wanachama wake, mapato kutokana na shughuli za uzalishaji na shughuli nyengine za kiuchumi zinazofanywa na Chama na michango kutoka katika duru za wasiokuwa wanachama.

License

Tishio la Ukombozi Copyright © 2016 by Amrit Wilson. All Rights Reserved.

Share This Book

Feedback/Errata

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *