1 Siku za Awali za Mapambano Dhidi ya Ukoloni

Kipindi cha katikati ya miaka 1950 na mwanzoni mwa miaka ya 1960, wakati masimulizi haya yanapoanzia, kilikuwa na mambo mengi yanayofanana na yale ya hivi sasa. Katika bara la Afrika, Marekani na Uingereza walifanya kila juhudi ili kuleta ‘mabadiliko ya utawala’ na kuziweka madarakani serikali ambazo wangeliweza kuzichezea akili na kuzitumia kwa maslahi yao. Walitumia mbinu za chini kwa chini na itikadi za vitisho na kutia wahaka watu na kuanza kuwatafuta wachawi – lakini wakati huo ilikuwa dhidi ya makomunisti, na si ‘magaidi wa kiisilamu’. Katika mpango wao wa kuendelea kuzinyonya nchi za Afrika (wakati huo nyingi zikiwa ndiyo kwanza zimepata uhuru au zinapambana na ukoloni), Zanzibar ilionekana kuwa ni pahala muhimu. Marekani waliiona kuwa ni sehemu ya ukanda wa Afrika ya Kati ambayo kama itadhibitiwa, itailinda sehemu ya Kusini mwa Afrika (pamoja na mali iliyowekezwa na nchi za magharibi) dhidi ya ushawishi wa wapenda maendeleo na masoshalisti wa nchi kama zile za Algeria na Ghana. Kama Zanzibar ingelitoka nje ya mzunguko huu, walikuwa na hofu kuwa na Afrika yote ingeliifuata.

Zanzibar ilikuwa, na bado ni sehemu muhimu mashuhuri. Kituo kikubwa cha biashara kwa miaka elfu mbili ikiziunganisha Afrika na Asia na rasi ya Arabuni. Imekuwa, kama ilivyokuwa hapo zamani, kituo cha mchanganyiko wa watu wa mataifa mbalimbali ya dunia. Mwanahistoria Abdul Sheriff anaelezea kwa hisia mji wa Zanzibar jinsi ulivyokuwa wakati wa utoto wake, mwanzoni mwa miaka ya 1950, alipokuwa akicheza katika barabara nyembamba zenye vichochoro pamoja na watoto wenye asili ya kiswahili, ya kiomani, ya kiajemi, ya kihadhrami au ya kihindi, na jinsi kila upepo wa musimu (monsoon) ulivyoshuhudia kuwasili kwa ‘majahazi na mabaharia kutoka Arabuni, Ghuba ya Uajemi, Bara Hindi na Somalia … bandari vile vile ilijaa majahazi kutoka Lamu na Kilwa. Ulikuwepo mwingiliano mkubwa wa watu’ (Sheriff, 2008)

Taswira hii ya mchanganyiko wa utamaduni wa aina mbalimbali ilidhihirisha pia kuwepo kwa mapambano makali dhidi ya ubeberu yaliyotokana na uzoefu uliopatikana wakati wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia na kujenga mwamko wa wananchi kuwa na hisia na nchi yao; na wanamapinduzi wengi wa miaka ya 1950 na 1960. Wakati wa vita, kama alivyoandika Abdulrahman Mohamed Babu:

Vijana wengi wa Kizanzibari waliandikishwa kwenye majeshi ya Uingereza, kwenda vitani wengi katika Afrika na Asia … Baada ya vita walirudi kutoka vitani huku wakiujua ukweli juu ya hali halisi na kiwango cha vurugu za wabeberu. Hadithi zao za kukutana na askari kutoka katika makoloni mengine (hasa wale kutoka ‘Gold Coast’, sasa Ghana, katika uwanja wa mapambano ya Burma) zilitusaidia sisi wa Zanzibar kuwa na mwamko wa kuwepo kwa uwezekano wa mshikamano na mapinduzi. (Babu, 1996)

Zanzibar: Ukabila, Matabaka na Mzuka wa ya Zamani

Vipi mfumo wa kijamii wa visiwa hivi umeumbika? Kuanzia miaka ya 1830 na kuendelea, vilitawalia na koo za Masultani, ambao ijapokuwa asili yao ni Oman, walilowea Zanzibar, wakaoana na wenyeji, wakisema Kiswahili na ilipofika katikati ya karne ya 20 hata hicho Kiarabu hawakukijua tena. Zaidi ya hayo, kwasababu ya pale ilipo, mahali pa aina ya pekee, Zanzibar ilikabiliana na mfululizo wa uvamizi wa wakoloni wa Kireno, wa Oman, Wajarumani na Wafaransa, na hatimaye, mwaka 1890 Waingereza.

Kwa kiwango fulani, ilikuwa ni kwasababu ya matokeo ya matukio hayo ya kikoloni ndiyo maana Zanzibar ikawa ni jamii iliyogawika kwa migogoro, ikiwa na umoja madhubuti wa kiutamaduni kwa upande mmoja, na migawanyiko mikubwa ya kikabila kwa upande mwengine; migawanyiko ambayo mzuka wake bado unavitisha visiwa hivi hadi hivi leo. Historia ya Zanzibar, ikiwa ni kituo kikuu cha biashara, na ukweli kuwa ilikuwa ndiyo njia ya kuingizia na kutolea bidhaa kutoka ndani ya bara la Afrika, iliisababishia kuwa ndiyo njia ya kupatia na kusafirisha watumwa, ijapokuwa idadi ya watumwa hao ilikuwa ni ndogo sana ukilinganisha na ile ya biashara ya watumwa waliokuwa wakisafirishwa kuvuka bahari ya Atlantic[1]. Wakati huo huo, kukua kwa mahitaji ya nchi za kibeberu visiwani katika karne ya 19 kulisadifu kutokea pamoja na kuingizwa kwa zao la karafuu nchini Zanzibar. ‘Maendeleo yaliyofuatia ya kuwepo kwa mfumo wa mashamba makubwa yaliathiri sana mahusiano ya kiuzalishaji visiwani. Watumwa waliokuwa wakichukuliwa kutoka bara hawakuwa tena bidhaa ya biashara ya pekee lakini badala yake wakawa nguvu kazi ya uzalishaji mashambani’ (Depelchin, 1991: 14). Wakati huo Zanzibar ilikuwa ni jamii yenye mfumo wa utumwa, na iliendelea kuwa hivyo mpaka utumwa ulipoondolewa Unguja na Pemba mwaka 1897.

Awamu hizi zilizofuatana za historia ya Zanzibar zimekuwa na athari kubwa na ya kudumu visiwani. Historia ya utumwa ilikuwa na maana kuwa kila mmoja alionekana, na wengi walijiweka katika makundi ya ama ‘Waarabu’ au waliohusiana na ‘Waarabu’ na waliokuwa wakimiliki watumwa na kwa hivyo Mabwana (mabwana waliokuwa na kila fursa) au Waafrika waliokuwa watumwa waathiriwa wa Mabwana. Hata hivyo, juu ya kuwepo kwa mivutano hii, katika kipindi cha kabla ya ukoloni wa Kiingereza hapajawahi kutokea mgogoro mkubwa wa kikabila.

Migawanyiko hii haikuambatana na hali ya kutokuwepo kwa usawa au matabaka katika jamii ya Kizanzibari, hivi sasa au nusu karne iliyopita. Hapo zamani, kama ilivyo hivi sasa, idadi kubwa ya watu ilikuwa ni ya mchanganyiko wa watu wenye asili ya Kiarabu na Kiafrika na makundi ya Waarabu na Waafrika yalikuwa yamechanganyika kiasi kwamba baina ya mwaka 1924 na 1948 asilimia ya wale waliojiainisha kuwa ni Waarabu iliongezeka kutoka asilimia 8.7 hadi kufikia asilimia 16.9 kwasababu wengi ya wale wasiokuwa Waarabu ‘waliamua’ ‘kuungana’ na jamii ya Waarabu’ (Lofchie, 1965: 74), bila ya kuulizwa maswali au kuwekewa pingamizi zozote.

Lakini kwa bahati mbaya, hofu na wasiwasi wa historia hiyo ya ukoloni na utumwa zimeendelea kuvisumbua visiwa hivi na zimekuwa zikichochewa mara kwa mara na wanasiasa wasio waadilifu.

Mnamo katikati ya karne ya 20 visiwa hivi havikuwa koloni rasmi bali vilikuwa chini ya himaya ya Uingereza. Lakini nchi zilizokuwa chini ya himaya hazikuwa na tofauti yoyote na zile zilizokuwa makoloni kuhusiana na suala la unyonyaji – Sultani alikuwa mfalme aliye chini ya katiba akilipwa mshahara na Uingereza na wao ndio waliokuwa wakiidhibiti serikali, wakiyadhibiti masoko na njia za kufanyia biashara, na kutia mfukoni faida ya mazao maarufu ya Zanzibar – karafuu na nazi.

Wakati huo, mgawanyiko wa kitabaka na kikabila kwa wakazi wa mashamba wa visiwa hivyo viwili ulikuwa ni tofauti kidogo na bila shaka tofauti na ulivyo hivi sasa. Kisiwani Unguja walikuwepo wamiliki mashamba wadogowadogo wasioishi mashambani bali wakiishi zaidi mjini, wakulima wa kilimo cha kujikimu walioishi katika maeneo yasiyokuwa na rutuba nzuri na wavamizi kwenye mashamba makubwa.

Katika miaka ya 1950 wamiliki mashamba hawa wa Unguja, takriban wote walikuwa Waarabu. Wakulima wa kilimo cha kujikimu wa Unguja, wengi walikuwa ni Washirazi watu waliochanganya damu, kama alivyo kila mtu Zanzibar, lakini wenye asili ya kutoka Shiraz nchini Iran, ambako wahamiaji kutoka huko waliwasili Zanzibar tokea karne ya 10. Wavamizi, wengi walikuwa ni watu ambao walikuja kutoka bara ya Tanganyika wakiwa vibarua wa kufanyakazi kwa mkataba wakati wa msimu wa kuchuma karafuu lakini waliendelea kubaki na kuingiliana na wenyeji kwa kuoana, na kwa vizazi kadha wakajumuika katika jamii ya Zanzibar.

Mji wa Zanzibar ulio katika pembe ya magharibi ya Unguja ulikuwa umeendelea sana na ijapokuwa ulikuwa wa kizamani lakini ulikuwa ni wa kisasa vile vile. Ulikuwa na taa za barabarani za umeme muda mrefu kabla hata London haikuwa na taa kama hizo. Wakazi wake walikuwa wafanya biashara, wachuuzi wauza vitu barabarani, wauza maduka, vibarua, makuli, wasafirishaji na kadhalika.

Hata hivyo, ukabila na matabaka havikuambatana pamoja na wala mfumo wa matabaka haukuwa ni mfumo usiobadilika. Kwa mfano, ijapokuwa Washirazi walikuwa ndio wengi miongoni mwa wakulima wa kilimo cha kujikimu na Waafrika (ambao mara nyingi walikuwa ni wahamiaji kutoka bara) walikuwa ndio wengi miongoni mwa wafanyakazi wa mjini, makabila haya, kama yalivyo makabila mengine, yalikuwa yametawanyika katika mgawanyiko wa matabaka mbalimbali (Kuper, 1970: 366).

Pemba, tofauti na Unguja, takriban yote ilikuwa ni eneo la mashambani katika miaka ya 1950 na haikuwa na maendeleo makubwa ya kiteknolojia. Ardhi yake ilikuwa nzuri na yenye rutuba, na walikuwepo mabwana wakimiliki mashamba wakubwa wachache na idadi kubwa ya Washirazi na Waarabu waliokuwa wakulima matajiri na wa hali ya kati[2].

Namna ambayo ubepari wa kikoloni ulivyoendelea ilikuwa na maana kuwa makabila mengi yalijikuta yakiingizwa, na baadhi ya wakati yakifungika katika kazi maalum na kuwa katika makundi ya kiuchumi ambayo yalikuwa yakikinzana. Kwa mfano, watu wa kutoka Kusini ya Asia waliowasili Zanzibar mapema katika karne ya 1 AD wakiwa wafanya biashara na wachuuzi (Bader, 1991: 170) waliziona shughuli zao za kiuchumi zikipungua mnamo robo ya mwisho wa karne ya 19. Matokeo yake kwa upande mmoja, iliwafanya idadi kubwa ya watu waliotoka Kusini ya Asia waliokuwa matajiri wakaingia katika shughuli za kukopesha pesa. Wakiwa katika shughuli hiyo, waliwatia katika umasikini Waarabu waliomiliki ardhi ambao walikuwa katika hatari iliyosababishwa na kupanda na kushuka kwa bei ya karafuu na hili lilisababisha mvutano kati ya makundi mawili haya

Kama ilivyokuwa katika makoloni mengine, visiwani Zanzibar sera ya kikoloni ya Uingereza vile vile ilishadidia na kusababisha kushamiri migogoro ya kikabila iliyokuwepo. Kwa mujibu wa itikadi ya kikabila ya wakoloni ambayo iliwaona Waarabu kuwa ni waovu, walafi wa dhahiri wenye watoto wengi (Lofchie. 1965: 108) na wakati huo huo iliwaona Waafrika kuwa si chochote ila ni watu wa chini kabisa; kwa mnasaba huo serikali ya kikoloni ilianzisha vyama vya kikabila ambavyo kila raia alitakiwa ajiunge navyo. Vilikuwepo kiasi ya vyama 23 vya aina hiyo – Chama cha Waafrika (African Association), Chama cha Waarabu, ( ambacho kiligawika katika vyama vya Waarabu wa Omani, Hadhramout na Yemen), Chama cha Washirazi (Shirazi Association) na kadhalika. Vyama hivi ambavyo viliongozwa na matabaka ya juu ya kila kikundi vilijenga mgawanyiko wa kikabila na kusababisha uhasama wa kikabila.

Wakati huo huo mfumo wa elimu uliowekwa na Waingereza ulizingatia matabaka na kutokuwepo kwa usawa kati ya makabila kwa kuwa ilitoa elimu iliyolipiwa na serikali kwa watoto wa matabaka ya waliokuwa na uwezo tu, isipokuwa labda kwa wachache ambao hawakuwa wa matabaka hayo (Sheriff, 1991: 87).

Kama zinavyoonyesha taarifa na barua za wakati huo, ukabila wa kikoloni wa Waingereza, kama ilivyokuwa katika makoloni mengine ya Uingereza, ulikuwa na maana kuwa Waingereza waliwatambua watu kwa mujibu wa kabila na dini zao. Walikataa kuamini kuwa makundi mbalimbali na watu binafsi wanaweza kuwa na utambulisho wa aina yoyote ya kisiasa. Jambo pekee lililokuwa tofauti na mawazo haya ni pale watu walipotuhumiwa kuwa ‘wakomunisti’, na kwa hivyo kutawaliwa na mabwana wa kigeni, Wachina au Warusi na kuthibitisha imani yao kuwa watu hawa walio katika makoloni hawakuwa na uwezo wa kuwa na mawazo yao wenyewe binafsi. Wamarekani, ambao walikuwa wawe na jukumu muhimu katika kuupa mwelekeo mustakbala wa Zanzibar na Tanganyika walikuwa na mtazamo kama huo.

Mapambano Dhidi ya Ukoloni na Chama cha Kwanza cha Wananchi

Kipindi cha mwanzoni mwa miaka ya 1950 kilishuhudia mvuvumko wa hisia za kiuwananchi visiwani Zanzibar. Kabla ya mwaka 1946 wajumbe wa Baraza la Kutunga Sheria la kikoloni walikuwa ni Wazungu, Waarabu na Wahindi, na hata baada ya mwaka 1946 uwakilishi wa Waafrika ulifanywa kuwa mdogo. Waingereza waliweka wazi kabisa kuwa hali hiyo isingelibadilika katika siku za mbele. ‘Kuanzishwa kwa mfumo wa bunge wa demokrasia kamili kulionekana kuwa ni mpango wa muda mrefu katika kukua kwa siasa … Dhana ya kuwa kujitawala wenyewe kwa njia ya kidemokrasia kungeliwezekana tu baada ya vizazi vingi kuelimishwa kwa makini ndiyo ilikuwa mtazamo wa Waingereza katika makoloni mengi’ (Lofchie, 1965: 19).

Kutokana na hali ya safu za kikabila katika jamii ya Zanzibar, moja katika njia chache ambazo wananchi wangeliweza kuzifanya sauti zao zisikike ilikuwa ni kwa kupitia kwenye magazeti ya vyama vyao. Kwa mfano, wanachama wakakamavu wa Chama cha Waarabu walianza kulitumia gazeti la chama hicho Al Falaq kupinga sera ya uwakilishi wa kikabila katika Baraza la Kutunga Sheria[3].

Kama mwamko dhidi ya ukoloni ulivyokuwa ukikua, moja ya mapambano ya awali dhidi ya ukoloni yalikuwa ni machafuko ya wakulima yaliyotokea baina ya mwaka 1951 na 1954 magharibi ya kisiwa cha Unguja karibu na mjini Zanzibar. Waingereza waliyazima machafuko hayo kinyama.

Machafuko hayo yalisababishwa na mambo mawili ya ghafla. La kwanza ni kwa serikali ya wakoloni kupora sehemu kubwa ya ardhi ambayo ni mali ya kaya za wakulima wa kati – kwa maneno mengine ya familia zilizolima katika ardhi yao wenyewe bila ya kukodi, wao wenyewe kukodiwa kuwa wakulima vibarua – kujenga uwanja wa ndege; na la pili ni kulazimishwa kuwachanja ng’ombe wao dhidi ya kimeta na kulazimishwa kuwakogesha ng’ombe wao kwenye josho dhidi ya Homa ya Mwambao. Mpango wa kulazimishwa kuwakogesha ng’ombe ulianzishwa mwaka 1948: Wakulima si kama walilazimishwa kulipia kukogeshwa huko tu lakini kukogeshwa huko kulisababisha vifo vingi vya ngombe. (Kama serikali ilivyokiri baadae, kumwogesha ng’ombe kungeliweza kumfanya ng’ombe apoteze kinga dhidi ya maradhi, kusababisha apate maambukizi na kufa ikiwa kama hakuendelea kukogeshwa mara kwa mara.)

Ng’ombe walikuwa ni chanzo muhimu cha mapato kwa wakulima, na pale serikali ilipojaribu kuanzisha mtindo wa kuwalazimisha kuwapiga ng’ombe wao sindano wakulima walikataa. Adhabu za kukamatwa na kutozwa faini zilisababisha kugomewa kwa shughuli mbalimbali za serikali. Viongozi wa wakulima kumi na tisa walitiwa hatiani lakini wakati wakipelekwa gerezani, wakulima kutoka maeneo ya karibu ambao walikuwa wamelizunguka jengo la mahakama walilivamia gari lililokuwa limewachukua na kuwafungulia wenziwao kumi na moja. Baadaye walijaribu kulivamia gereza ili kujaribu kuwafungulia wengine. Polisi waliwapiga risasi na kuua watu tisa (Bowles 1991: 95).

Kuzimwa kwa machafuko hayo kulisababisha kuibuka kwa vuguvugu la kwanza la kupigania uhuru na Chama cha Umoja wa Kitaifa cha Raia wa Sultani kilianzishwa na wakulima – na jina hilo lilidhihirisha madhumuni ya chama hicho yaliyokuwa ni kuyaunganisha makundi ya watu wa makabila mbalimbali na wakati huo huo kuwajumuisha siyo tu watu wa Unguja na Pemba bali pia watu wote wanaoongea Kiswahili wa mwambao wa Kenya. Utambulisho wa ‘raia wa Sultani’ inapasa ueleweke kuwa ni kwasababu Sultan hakuchukuliwa kuwa ni mtawala wa kigeni; tofauti na Waingereza. Kusema kweli, zilikuwepo hadithi zilizotolewa na wakulima wa Zanzibar juu ya namna gani wazazi wao walisafiri hadi Oman ili kuomba msaada wa Sultani dhidi ya Ukoloni wa Kireno (Babu, 1991:223).

Habari za machafuko hayo na namna yalivyokandamizwa zilizagaa kama moto wa mbugani katika sehemu zote za Zanzibar, mashambani na mjini. Serikali ya kikoloni ilishikwa na kiwewe. Ilihofu kuwa ari ya machafuko ya Mau Mau ilikuwa inazagaa siyo miongoni mwa wakulima tu bali pia miongoni mwa makundi mengine ya jamii.

Vile vile, waliuogopa muungano wa Waafrika na Waarabu na kutishia kupitisha sheria ambayo ingelipiga marufuku ushiriki wa watumishi wa serikali katika siasa. Hii iliwazuia watumishi wa serikali Waafrika kuweza kujihusisha na siasa na kuathiri kwa kiwango kikubwa siasa za Chama cha Waafrika. Rais wa Chama cha Waafrika alikuwa ni Daktari mpenda maendeleo na aliyefanya kazi serikalini. Kwa hivyo ilimbidi ajitoe katika siasa na Abeid Karume aliyekuwa baharia na baadae mmiliki wa mashua na kiongozi wa Shirikisho la Wenyekumiliki Mashua akawa raisi wake. Chama cha Waafrika chini ya uongozi wa Karume kilianza kuwa na msimamo wa kimuhafidhina na wa kuwapinga Waarabu. Kilipinga kile ilichokiona kuwa ni uzalendo wa Waarabu na wakati huo huo kilianza kufanya kampeni ya kutaka uwakilishi wa kikabila uendelee hata kama ulikuwa ukiwapunguzia nguvu Waafrika (Lofchie, 1965; 166).

Pale makala yaliyoandikwa katika gazeti la Al Falaq yalipoeleza mshikamano wake na machafuko ya wakulima na kulaani ukandamizaji wa wakoloni katika kuyazima machafuko hayo, Waingereza walimshtaki kwa kosa la uchochezi mchapishaji wa gazeti hilo na wajumbe wote wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Waarabu. Miongoni mwa wajumbe hao wa Halmashari Kuu alikuwemo Ali Muhsin ambaye baadae alikuwa miongoni mwa watu muhimu wa vuguvugu la kisiasa la wananchi. Chama cha Waarabu kiligoma na kiliwatoa wawakilishi wake wote kutoka katika Baraza la Kutunga Sheria na kulilaani baraza hilo kuwa ni la kikabila na kutaka kuharakishwa kwa mchakato wa kupatikana uhuru. Mgomo huu ulifanikiwa kikamilifu kwa kipindi cha mwaka mmoja na nusu.

Kesi ya uchochezi ilikuwa na athari kubwa kwa mwamko wa kisiasa wa wananchi katika nchi nzima. Wafanyakazi wa mjini, wachongaji na wajenzi, mabepari uchwara na wasomi walianza kujiunga na Chama cha Umoja wa Kitaifa cha Raia wa Sultani (PNUSS). Wakulima, ambao ndio waliokuwa waasisi wa chama hicho waliwakaribisha kwasababu sasa chama hicho kilihitaji ustadi ambao wakulima wenyewe hawakuwa nao. Baada ya muda mfupi, Chama cha Umoja wa Kitaifa cha Raia wa Sultani (PNUSS) kilianza kuendelea kuwa chama kamili cha wananchi. Kilibadili jina lake na mwaka 1955 kikawa Chama cha Wazalendo cha Zanzibar (Zanzibar Nationalist Party- ZNP). Ali Muhsin akawa kiongozi wake

Chama hicho kilianza kufanya kampeni ya uwakilishi usio wa kikabila katika Baraza la Kutunga Sheria, haki ya watu wazima wote kupiga kura na katiba mpya itakayoihakikishia nchi uhuru mapema iwezekanavyo.

Hofu za Waingereza na Kuundwa kwa Chama cha Afro-Shirazi

Waingereza waliingiwa na hofu kubwa kwa jinsi hali ilivyokuwa. Kama nyaraka za wakati huo zinavyoonyesha, kwa siri walielezea hofu yao kwa kuanzishwa kwa chama cha ZNP likiwa ni vuguvugu la ukombozi na kwa mujibu wa fikra za vita baridi, walidhani kuwa chama hicho kimejaa wakomunisti waliokuwa wakilipwa na Umoja wa Kisovieti na China. Hata hivyo, hadharani walionyesha vuguvugu la kupinga ukoloni lililoongozwa na ZNP kuwa ni tukio ambalo watu wa Zanzibar inabidi waliogope.

Kwa wamiliki mashamba wa Kiarabu, walilionyesha vuguvugu hilo kuwa ni tishio la moja kwa moja kwa maslahi yao binafsi na nafasi yao katika uchumi wa nchi. Kwa mabepari uchwara wa Kiafrika na Kishirazi walilionyesha vugu vugu hilo kuwa ni chama cha ‘umoja’ uliojengwa kwa hila wa Waarabu ili kuwaondoa Waingereza na kuuweka umma wa Waafrika chini ya utawala wa Waarabu (Babu 1991: 225).

Kufuatana na fikra hizi, wanadiplomasia wa Kiingereza walijishughulisha kuleta ushawishi wa kuanzishwa kwa chama cha Waafrika ambacho kitaipinga ZNP na kuwa kitiifu kwa Waingereza. Hili lilikuwa rahisi kwa vile Chama cha Waafrika kilivyokuwa, ambacho kwa namna yoyote ile hakikupinga ukoloni na kiliitaka Tume ya Katiba ya Coutts ya mwaka 1956 iendeleze utaratibu wa uwakilishi wa kikabila katika Baraza la Kutunga Sheria kwa angalau miaka mitano mengine ijayo.

Hata hivyo, mipango ya Uingereza haikufanikiwa kwa muda kwa kuwa Chama cha Waafrika kilikuwa na washiriki wachache. Washirazi wa Pemba, ambao wengi walikuwa wakulima matajiri na kuongozwa na watu kama vile mwalimu wa skuli mstaafu Mohammed Shamte na mmiliki ardhi Ali Shariff, hawakutaka kushirikiana nacho. Sababu walizotoa ni kwamba hawakutaka kuwa sehemu ya kitu ambacho asili yake inaambatana na mtazamo wa kikabila. Lakini kilichojificha nyuma yake kilikuwa hisia za uzalendo finyu wa mrengo wa kulia wa Washirazi uliojengeka chini ya misingi ya chuki dhidi ya Waafrika na Waarabu.

Hata hivyo, msaada wa kuwasaidia Waingereza haukuwa mbali kwasababu wakati huo Julius Nyerere akiwa kiongozi wa chama cha Tanganyika African National Union (TANU), aliamua kuingilia kati siyo kuleta umoja kati ya chama cha ZNP na Chama cha Waafrika kama ambavyo ingelitarajiwa, bali ili kujenga umoja dhidi ya kile alichokiona kuwa ni chama cha Waarabu. Aliitembelea Zanzibar mara kadha mnamo mwaka 1956 ili kuwashawishi Waafrika na Washirazi kujenga umoja kama huo dhidi ya Waarabu (Lofchie, 1965: 168). Kwa mbali inaonyesha kuwa labda hizi ni dalili za mwanzo za jukumu ambalo Nyerere angelilitekeleza baada ya mapinduzi.

Hatimae, mwezi Februari 1957 muda mfupi kabla ya uchaguzi, umoja ulioitwa Afro-Shirazi Union (ASU) ulianzishwa, huku Chama cha Waafrika na Chama cha Washirazi cha Unguja vikikubaliana kushirikiana wakati wa uchaguzi unaokuja (lakini siyo kuunganisha vyama) na Chama cha Washirazi cha Pemba kukataa kufanya hivyo (Sheriff, 1991: 134).

Kuundwa kwa ASU kulikifanya chama cha ZNP kumtuhumu Karume, kiongozi wa ASU kuwa si raia asilia wa Zanzibar na kumpeleka mahakamani. Tuhuma hii ya kipuuzi, na uzalendo finyu  ilimfanya Karume aonekane kuwa shujaa. Alishinda kesi hiyo kwa urahisi na kwa hukumu iliyotolewa muda mfupi kabla ya uchaguzi, kura za waliomuhurumia zilimfanya atambulike kuwa ‘kiongozi wa kitaifa’.

Katika uchaguzi huu chama cha ZNP kilishindwa vibaya. Hata hivyo chama cha ASU nacho hakikushinda uchaguzi vile vile, kilipata chini ya humusi mbili ya kura zote visiwani na viti vitatu kati ya viti sita vya wajumbe wa kuchaguliwa katika Baraza la Kutunga Sheria. Miezi michache baadae, Washirazi wa Pemba, kwa shingo upande, walikubali kushirikiana na ASU na Chama cha Afro-Shirazi Party kiliundwa.

Kaulimbiu ya chama cha Karume wakati wa kampeni ya uchaguzi … ‘Uhuru Zuia’ ilionyesha wazi msimamo wa ASP kuwa ni mshiriki wa Uingereza. Karume, juu ya hofu yake na chuki kwa Waarabu aliweza kuwa na tabia za unyonge wa kushangaza. Baada ya kutoa hotuba ambayo alihisi itamkera Sultani, tarehe 26 Julai, 1958, Karume alimwandikia Sultani ifuatavyo:

Mheshimiwa, mimi ni raia wako pamoja na wanachama wote wa Chama cha ASP ninapenda kuahidi kwako utiifu wangu kamili. Mimi binafsi, Abeid Amani Karume naomba kukueleza ukweli, Mfalme wangu. Wakati wa hotuba yangu hapo Raha Leo, nilidhani nilitumia maneno ya kistaarabu lakini sikuelewa maana ya maneno hayo. Kwa hivyo, nia yangu na nia ya wenzangu, kutoka ndani ya nyoyo zetu, Mfalme wetu mpendwa Maulana, kukuomba na kukufanya uelewe kuwa sisi tupo chini ya miguu yako na chini ya Utawala wako. Sisi ni watiifu, bila ya wasiwasi wowote, kwa kila amri yako. Sote sisi tunaujua wema wako wa dhati na ukarimu wako. Nakuomba unisamehe kosa langu kwa kutumia lugha ambayo sikuielewa, Maulana. Mimi nipo chini ya miguu yako na ninabaki kuwa mtiifu.

Abeid Amani Karume. (Makavazi ya Taifa, Zanzibar, Julai 1958)

Je, barua hii iliandikwa kwa amri ya Uingereza? Au ni mawazo yake Karume mwenyewe? Inaweza kuwa ni kwa amri ya Uingereza kwasababu Karume alikuwa raia mtiifu na mwenye shukrani kwa Uingereza. Anajulikana kuwa wakati akitoa hoja juu ya kuendelea kuwepo kwa utawala wa Uingereza, alisema kuwa, ‘Tutajifunza kutoka kwa Waingereza; Waarabu wapo nyuma kama sisi’ (Ayani, 1970: 50). Vyovyote itakavyokuwa inaonyesha sura ya mtu ambaye baada ya muda si mrefu angeliitawala Zanzibar.

Taswira ya kitabaka ya Chama cha ASP wakati huu inabidi kuchukuliwa kuwa ni ya kibepari uchwara. Ilipofikia mwaka 1957, kiongozi wake, Karume hakuwa tena baharia bali ni mmiliki wa mashua, na wafuasi wake ‘walikuwa ni miongoni mwa kundi la watu wanaojiweza wa Zanzibar (ukiwatowa mabwana wanaomiliki mashamba)’ (Bowles, 1991: 100).

Cheche za mapinduzi katika anga ya Zanzibar

Ilikuwa katika kipindi hiki ndipo Abdulrahman Mohamed Babu aliporudi Zanzibar baada ya kuishi London kwa muda wa miaka sita. Baba yake alitokana na ukoo wa wanazuoni wa Kiisilamu wenye asili ya mchanganyiko wa Mswahili na Mngazija. Mama yake aliyetokana na familia ya wafanya biashara wa kiarabu, ijapokuwa bibi yake alikuwa Muoromo, alifariki wakati Babu akiwa na umri wa miaka miwili. Alilelewa na shangazi lake mkubwa aliyekuwa na nyumba Mji Mkongwe, hapo Unguja. Alikuwa, kama Babu mara nyingi alivyomkumbuka ‘mwanamke madhubuti – mpiganaji’ ambaye hakuwahi kumlazimisha kufuata desturi fulani maalum.

Baada ya kumaliza skuli, Babu alifanyakazi ya ‘karani mpima mizani’ katika Shirika la Ununuzi wa Karafuu Clove Growers Association na aliweka pesa akiba ili aende Uingereza kwa masomo ya juu. Katika miaka ya 1950 London ilikuwa imejaa watu wenye siasa kali, wenye kupenda maendeleo na kuwepo kwa vuguvugu la kupinga ukoloni, kwa hivyo ijapokuwa alidhamiria kusomea uhasibu lakini mara alibadili mawazo. Wakati huku akifanyakazi ili kujitafutia riziki, alisoma falsafa na fasihi ya Kiingereza. Kwanza alikuwa na mawazo ya mfumo wa utawala huria na baadae kuwa na mawazo ya Kimarx na kujishirikisha na siasa za kupinga ukoloni. Kwa mfano, alikuwa katibu wa Kamati ya Afrika ya Mashariki na ya Kati ya chama kilichokuwa na ushawishi mkubwa cha Vuguvugu kwa Uhuru wa Makoloni (Movement for Colonial Freedom), akishirikiana pamoja na Samir Amin na Frene Jinwallah alikuwa mhariri mwenza wa jarida lililokuwa likichapishwa Paris la Africa, Latin America Asia – Revolution.

Kadhalika, alikuwa amejishirikisha sana na siasa za Umajumui wa Afrika. Wakati wa zama hizo za kihistoria za mapambano ya ukombozi na ushindi wa kimapinduzi, kitu kimoja muhimu ambacho kilikuwa na ushawishi mkubwa wa kisiasa kwa Waafrika wa kizazi cha Babu ulikuwa ni ushindi wa Nkrumah huko Ghana. Kama alivyoandika:

Kutokea kama ulivyotokea, baada ya Mapinduzi ya Uchina, ushindi wa Viet Minh dhidi ya Ufaransa Dien Bien Phu (1954) na mapinduzi ya Algeria … ushindi wa Ghana umetuonyesha kwa njia iliyo halisi umuhimu na athari za ‘chama cha siasa chenye kujumuisha umma wote dhidi ya ukoloni. (Babu, 1996: 325).

Hata hivyo, kama walivyokuwa vijana wengi wa Kiafrika na Kiasia wa kipindi chake, Babu alivutiwa vile vile na mapinduzi ya Uchina. Alijifunza kikamilifu kutokana na mapinduzi hayo na hasa juu ya umuhimu wake kwa Afrika. Mapinduzi ya kisoshalisti ya Uchina, aliandika:

Yalikuwa ni mwendelezo wa mapambano yake yenyewe ya ukombozi na matokeo yake ni kuwa ulikuwepo mstari mwembamba sana uliougawa utaifa wake na usoshalisti. Utiifu huu wa pande zote mbili kwa mavuguvugu mawili haya makubwa ya wakati huo, uliwawezesha Wachina kushirikiana kwa karibu zaidi katika hisia na matarajio ya mapambano ya ukombozi ya Afrika na mapambano ya ujenzi wa taifa, yote mawili haya yakiwa ndiyo vipaumbele vya juu vya Afrika.

Babu (1987a; 2002: 166)

Mnamo siku zake za mwisho za kuishi London, uongozi wa Chama cha ZNP ulifanya mpango ili Babu apatiwe mafunzo juu ya uendeshaji wa chama cha siasa na Chama cha Labour cha Uingereza; na mara baada ya kurudi Zanzibar alifanywa kuwa katibu mkuu wa Chama cha ZNP.[4]

Babu mara baada ya kurejea kutoka London mwaka 1957. Chanzo: Mohamed Amin/Camerapix
Babu mara baada ya kurejea kutoka London mwaka 1957. Chanzo: Mohamed Amin/Camerapix

Miaka iliyofuatia uchaguzi wa 1957 na ZNP kushindwa vibaya, kwa nguvu zake zote na bila ya kuchoka Babu alianza juhudi za kukiunda na kukijenga upya chama huku akiwa na matumaini mema. Ulijengwa mtandao madhubuti wa matawi nchi nzima na kuanza kuendesha mikutano ya kawaida ya maeneo ya wenyeji kila wiki na mikutano hiyo ilihudhuriwa na wawakilishi wa Halmashauri Kuu ya Taifa. Hii ilikiwezasha chama kuwajumuisha watu na kueleza mahitaji na uzoefu wao wakati kikijenga umoja, huku wakati huo huo kikiwapa viongozi wenyeji wa sehemu husika hisia kubwa za chama kuwa ni chama cha kitaifa chenye madhumuni ya kitaifa, na kupinga ushindani wa kimkoa na kuoneana wivu.

Nia ya Babu ilikuwa ni kukijenga Chama cha ZNP ili kiwe Chama chenye kujumiusha umma wote na kuunganisha nchi nzima katika mapambano dhidi ya ukoloni. Alikusudia kuwaleta pamoja watu wa kutoka katika makundi yote ya kikabila na matabaka kwa msingi wa itikadi ya kupinga ukoloni na wakati huo huo kuonyesha ukweli juu ya tofauti za kitabaka ndani ya makundi ya kikabila na haja ya kuliunganisha tabaka la wafanyakazi na la wakulima masikini.

Ili kulitekeleza hilo, aliunda chama cha kwanza cha vijana cha ZNP, Umoja wa Vijana (YOU) ili kiweze kuwafikia watoto wa skuli za msingi na za sekondari na vijana wa mjini na mashamba, wanaume na wanawake, wa matabaka na makabila yote. Umoja huu ulipendwa sana, na kuleta nguvu mpya ndani ya chama pamoja na kulifanya suali la umoja kuwa ndio lenye umuhimu mkubwa kiitikadi na katika kazi halisi za chama. Ufanisi wake ulikuwa ni ushahidi wa uwezo wa Babu kutafsiri nadharia kuwa vitendo vya uendeshaji pamoja na kuwatambua walio na uwezo zaidi na kuwashajiisha miongoni mwa wengine. Wenzake wanamkumbuka kuwa ni kiongozi wakimapinduzi wa kupigiwa mfano, asiyekubali kurubuniwa, mwenye kuheshimu utaratibu na si mwenye kung’ang’ania yale anayoyaamini yeye tu, mwenye kipaji na mwenye kujiamini lakini si fidhuli, aliyejitolea na makini, mchangamfu, mwepesi wa kuchangayika na watu na yuko tayari kuviangalia vitu kwa njia ya kufurahika.

Shaaban Salim na Hamed Hilal walikuwa wanafunzi pale walipojihusisha kwa mara ya kwanza na Chama cha ZNP, Hamed mwaka 1958 na Shaaban mwaka 1960. Walipata elimu yao rasmi ya kisiasa kupitia YOU. Shaaban anazikumbuka siku hizo za msisimko. ‘Tumekua ndani ya YOU, tukiwa na mihadhara na mijadala. Kwa mara ya kwanza tulijaribu kutafakari juu ya ukoloni na ubeberu na jinsi ya kupambana nao wakati tukiwa na mwamko’ (mahojiano na Shaaban Salim, 2009). Kwa mujibu wa maelezo ya Hamed Hilal, ilikuwa ni kuundwa kwa YOU ndiko kulikokigeuza Chama cha ZNP kuwa kundi lenye nguvu kubwa ya kisiasa.

Ilikuwepo mijadala ya kisiasa juu ya masuala mahasusi ili kufafanua maana halisi ya mapambano ya kiitikadi, ilikuwepo michezo ya kuigiza na madarasa ya kisiasa na kampeni kubwa ya kujifundisha kusoma na kuandika katika Zanzibar nzima. Yalikuwepo maandamano ya kudai elimu ya sekondari kwa wote na dhidi ya sera za kikabila, na maandamano ya kuunga mkono ukombozi wa Algeria na Palestina na dhidi ya utawala wa makaburu wa Afrika ya Kusini.

 

Wanafunzi wakike wanachama wa YOU waliopigwa picha na Waingereza waliokuwa na wasiwasi na ‘vijana wakakamavu’
Wanafunzi wa kike wanachama wa YOU waliopigwa picha na Waingereza waliokuwa na wasiwasi na ‘vijana wakakamavu’. Chanzo: Ofisi ya Kumbukumbu za Serikali CO 822/1377

Shughuli hizo zilikuwa kama cheche za kimapinduzi katika anga ya Zanzibar – ziliibadilisha mandhari ya kisiasa, zikanyanyua mwamko wa vijana na kufufua imani yao ya kujiamini, imani ambayo wakoloni walitaka kuibomoa kwa makusudi, na kuwafanya waelewe kuwa mustakbali wao na wa nchi yao umo mikononi mwao.

Nia na kujiamini huko kulianza kuelezwa waziwazi kama vile kwa mfano ilivyoelezwa katika azimio la mkutano wa chama cha wanafunzi wa Zanzibar, All Zanzibar Students Association lililoripotiwa katika gazeti la ZaNews, gazeti lililoanzishwa na Babu ambalo lilikuwa ni sauti ya wale waliofuata siasa ya mrengo wa kushoto visiwani Zanzibar.’ Tuna jukumu kubwa la kutekeleza katika mendeleo yanayotokea hivi sasa katika nchi yetu. Siku zote tumekuwa mstari wa mbele katika mapambano ya wananchi wetu dhidi ya ukoloni na ubeberu’ (i, 1963). Wakati huo, gazeti la ZaNews lilikuwa miongoni mwa magazeti machache sana katika Afrika ya Mashariki lililoandika mara kwa mara habari kuhusu mapambano ya kitaifa na ya kimataifa dhidi ya ubeberu na mapambano ya tabaka la wafanyakazi.

Shughuli za Chama cha YOU ziliangaliwa na Waingereza kwa makini na kwa hofu. Waliduhushi kuhusu YOU na hata kukusanya picha za watoto wa skuli wakiwa katika gwaride na wanachama wa umoja huo wakiwa katika mapumziko katika mandar. Huku wakiwa na kiwewe cha ajabu kinacholingana na hali ya leo ya vita dhidi ya ugaidi, walikuwa na wasiwasi na ukakamavu wa waziwazi wa wanachama wa YOU.

Ama kuhusu Babu, wakoloni walizidi kuwa na wasiwasi na kuzidi kupendwa kwake na uwezo wake mkubwa wa kuandaa na kusimamia kile ambacho Balozi Mkazi wa Uingereza, cheo cha juu kabisa cha kikoloni katika himaya hiyo, alichokiita ’udhibiti wake wa vijana wasiokuwa na kazi na kukata tamaa wa Chama cha ZNP’ ( Ofisi ya Kumbukumbu za Serikali, 1962a).

Kisiasa, Babu hakuwa pekee hata kidogo. Chama cha ZNP kiliwavutia vijana wengine wengi waliokuwa na vipawa – wasoshalisti pamoja na wazalendo waliopenda maendeleo. Walikuwa ni pamoja na Ali Sultan Issa, Khamis Ameir, AbuBakar Qullatein (Badawi), Hamed Hilal, Shaaban Salim, Muhsin Abeid, Abdulrazak Musa Simai, Amar Salim (kuku), Ali Khatib Chwaya, Mohamed Abdalla Baramia, Kadiria Mnyeji na Salim Rashid pamoja na Salim Ahmed Salim, ambao wote wawili, kwa nyakati mbalimbali walikuwa makatibu wakuu wa YOU. Ilikuwa ni kazi ya pamoja, nguvu za ubunifu na utashi wa wote hawa – ambao baadae walikuwa wanachama wa Chama cha Umma Party – Chama kilichosaidia katika kuirudisha haiba ya Chama cha ZNP katika kipindi hiki.[5]

Baadhi yao, kama vile Babu walikuwa wamerejea kutoka Uingereza katika kipindi cha katikati ya miaka ya 1950. Ali Sultan Issa aliondoka Zanzibar kwa kuzamia ndani ya meli na kuwa baharia melini akiwa na umri wa miaka 18. Alisafiri dunia nzima. Aliwasili London baada ya safari iliyomchukua miezi kadha akipitia Calcutta, Cape Town na Vancouver. Yeye pia alijiunga na kundi la wanasiasa waliokuwa wakipinga ukoloni mjini London na baadae alijiunga na Chama cha Kikomunisti cha Uingereza kabla ya kurudi Zanzibar na kujiunga na Chama cha ZNP na kuwa mwakilishi wake wa kimataifa.

Qullatein Badawi, kiongozi mshupavu wa vyama vya wafanyakazi alijishughulisha katika Zanzibar Club, iliyoanzishwa na wahitimu kutoka vyuo vikuu vya Makerere na London, wengi wao wakiwa na uhusiano na Chama cha Kikomunisti cha Uingereza. Baadaye, yeye na Khamis Ameir walikuwa mstari wa mbele katika shughuli za vyama vya wafanyakazi za Chama cha ZNP.

Badawi alipofariki mwezi Novemba 2011, komred na rafiki yake Salim Msoma aliandika makala yaliyojaa hisia kumtukuza (Msoma 2011). Alieleza juu ya namna gani katika miaka ya 1950 na 1960 Wazanzibari waliowasili Uingereza walijiunga na vuguvugu la ukoministi: ‘kila mmoja wao alipokelewa na Badawi pale aliporudi Zanzibar. Kila walipowasili, alihakikisha kuwa ama yupo gatini au uwanja wa ndege kuwapokea.’

Khamis Ameir, hivi sasa akiwa katika umri wa miaka 80, bado anaishi Zanzibar. Kama Babu, yeye pia alisoma na kufanyakazi London. Khamis alinieleza kuwa wakati wa safari yake ya kurudi Zanzibar alipitia Nairobi na alikutana na Ali Sultan aliyekuwa akielekea Cairo kufungua ofisi ya chama cha ZNP. Khamis aliniambia:

Nayakumbuka majadiliano makali tuliyokuwa nayo usiku kucha. Niliporejea Zanzibar nilikuwa na hamu ya kuanza harakati za kisiasa. Nilikutana na Badawi ambaye alifanyakazi ya afisa wa forodha na alijiunga na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi la “Zanzibar and Pemba Federation of Trade Unions” (ZPFTU) ambalo lilijishirikisha na Chama cha ASP. Badawi alikuwa hakuridhika na ZPFTU kwasababu, kwanza, kama kilivyokuwa Chama cha ASP lilidai kuwa uhuru ucheleweshwe na pili, lilijishirikisha na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi la Kimataifa la nchi za magharibi ICFTU. ICFTU lilikuwa ni shirikisho la vyama vya wafanyakazi lililoanzishwa na Marekani wakati wa kipindi cha vita baridi ili kuvidhibiti na kuvituliza vyama vya wafanyakazi vinavyopinga ubeberu katika nchi za Dunia ya Tatu. (Mahojiano na Khamis Ameir, 2009)

Badawi alishauri kuwa Khamis ajiunge na Chama cha ZNP na kujishughulisha na chama chake cha wafanyakazi. Na hivyo ndivyo Khamis alivyofanya. Alijishughulisha na kuwaandaa wafanyakazi wa mashambani na mabaharia ambao wengi walikuwa ni mabaharia katika majahazi katika chama cha Maritime and Allied Workers Union chama ambacho yeye alikuwa ni katibu mkuu wake. Aliniambia kuwa, wakati huo chama cha ZNP kilikuwa kikiwaandaa pia wafanyakazi wafua vyuma, wafanyakazi katika viwanda vidogo vilivyokuwa vikitengeneza sabuni na wafanyakazi wengine. Vyama hivyo vya wafanyakazi si kama viliwasaidia wafanyakazi na kuwawakilisha katika kudai mishahara mizuri na hali bora za kazi tu bali kilitoa mafunzo ya siasa vile vile.

Ilipofika mwaka wa 1960 Badawi alijitoa katika chama cha ZPFTU na yeye pamoja na Khamis walijishughulisha katika kuviunganisha vyama viwili vya wafanyakazi vilivyokiunga mkono Chama cha ZNP – Chama cha Wafanyakazi wa Mashambani the Agriculture and Allied Workers Union na chama cha Mabaharia the Maritime and Allied Workers Union – ili kuunda Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi la Kimaendeleo Federation of Progressive Trade Unions (FPTU). Mnamo mwaka 1960 ilitokea migomo katika viwanda kadha kudai mishahara mizuri na hali bora za kazi na mwaka uliofuata wafanyakazi wa majahazi waligoma kwa siku 84 – mgomo mrefu kuliko mgomo mwengine wowote Zanzibar. Mgomo huu ulikuwa na mafanikio makubwa na kumalizika kwa kukubaliwa kwa madai yote ya wafanyakazi (Hadjivayanis na Ferguson, 1991: 209).

Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi la FPTU lilikuwa na magazeti mawili yaliyokuwa yakitoka kwa kawaida mara kwa mara katika miaka ya 1960, la Kiswahili lilokuwa likitoka kila siku lililoitwa Kibarua na la Kiingereza lililoitwa Worker lililokuwa likitoka kila wiki. Magazeti haya yote mawili yalitetea maslahi ya wafanyakazi na wakati huo huo yakiweka msimamo wa kupinga ukoloni na dhidi ya ubeberu wa Marekani. Badawi alifanyakazi katika Idara ya Kimataifa ya FPTU akijenga mahusiano na vyama vya wafanyakazi vya nchi za nje vilivyopenda maendeleo (Mahojiano na Khamis Ameir, 2009).

Nje ya vyama vya wafanyakazi, Chama cha ZNP vile vile kilijenga mtandao mpana wa washirika na kuandaa sera iliyo wazi iliyokuwa na mtazamo wa Umajumui wa Afrika na kupinga ubeberu, iliyounga mkono mapambano ya Mau Mau nchini Kenya, TANU nchini Tanganyika, mapambano dhidi ya Shirikisho la Afrika ya Kati, mapinduzi ya Algeria na mapambano ya kupinga utawala wa Makaburu na vita vya ukombozi vya Kusini mwa Afrika. Mtazamo wake wa kupinga ubeberu ulikipelekea vile vile kujenga mahusiano na mapambano ya Wapalestina na kuunga mkono haki ya Wachina ya kuingia katika Umoja wa Mataifa.

Wakati huo huo Marekani ilizidi kuingiwa na wasiwasi kwa vile chama hicho kilivyozidi kupendwa. Walianza kukituhumu kuwa ni ‘Chama cha Waarabu’ na wakati huo huo wakifuatilia kwa makini maendeleo ya matukio ya Zanzibar. Kuhusu hili, maafisa wa Marekani walijaribu kujenga mahusiano ya karibu na viongozi wa ZNP na wa ASP ambao wangeliweza kuwashawishi, iligharamia ziara za mara kwa mara za jasusi wa CIA anayehusika na vyama vya wafanyakazi, Irving Brown kwa madhumuni ya kuwavutia viongozi wa vyama vya wafanyakazi wa Zanzibar kujiunga na ICFTU na walianzisha kituo cha NASA cha kufuatilia vyombo vya angani Mercury juu ya kuwepo kwa upinzani mkubwa kutoka katika Chama cha ZNP.

Kwa kupitia kituo cha Mercury Shirika la Vyombo vya Anga la Marekani (NASA) lingeliweza kupeleleza siyo visiwa vya Zanzibar tu bali eneo lote la magharibi ya Bahari ya Hindi na Afrika ya Mashariki kwa jumla. Kituo hiki kilikuwa ndiyo mtangulizi wa kuwepo kwa Marekani katika Bahari ya Hindi hivi sasa. Zaidi ya hilo, Marekani ilianza kujenga mtandao wa vibaraka na viduhushi ndani ya Zanzibar (Wilson, 1989: 11).

Ama kwa Waingereza, maelezo ya mtumishi wa serikali wa ngazi ya juu P.A.P Robertson yanatoa mwanga juu ya kukata tamaa kwao wakati huo. Katika mahojiano yaliyonaswa katika kinasa sauti mwaka 1971, Robertson alisema kuwa Babu si kama alikuwa ‘mwiba’ ulioichoma serikali tu bali ni mtu mwovu kuliko wote nchini Zanzibar … gwiji mwovu’ ( ilinukuliwa na Smith, 1971).

Wasiwasi wa kikabila: Umoja wa Umajumui wa Afrika waingilia kati

Siku zote zimekuwepo tofauti za kisiasa kati ya wafuasi wa siaza za mrengo wa kulia na wafuasi wa siasa za mrengo wa kushoto ndani ya Chama cha ZNP lakini umoja ulizingatiwa kwa makini sana kufuatia mfumo madhubuti wa kidemokrasia wa chama hicho ambao Babu na wafuasi wengine wa siasa za mrengo wa kushoto walifanya bidii kubwa kuujenga miaka ya mwisho ya 1950. Hata hivyo, migogoro ndani ya Chama cha ZNP ilianza kuzidi. Hili halikuwa jambo la kushangaza kufuatia kuwepo kwa utetezi wa maslahi ya matabaka na makundi mbalimbali yaliyojiunga na chama hicho. Sehemu fulani ya wafuasi wa siasa za mrengo wa kulia bado walikuwa watiifu kwa Sultani na walitetea maslahi ya mabwana wamiliki mashamba kwanza, wakati wafuasi wa siasa za mrengo wa kushoto walifanyakazi ya kuwavutia wafanyakazi na wakulima wasiokuwa na ardhi wajiunge na Chama cha ZNP ili kiwakilishe maslahi yao na kukiwezesha chama hicho kuisemea nchi nzima kwa jumla.

Wakati huo, Chama cha ASP nacho vile vile kilikuwa na watu waliokuwa na maslahi mbalimbali ndani ya chama hicho – wafanyakazi, wakulima, mabwana wamiliki mashamba wachache (ijapokuwa walikuwa wachache kulingana na wale waliokuwemo katika Chama cha ZNP) vile vile wafanya biashara na wawakilishi wa wafanyabiashara wakubwa kutoka katika Chama cha Wahindi cha Indian National Association ambao maoni yao yalikuwa na ushawishi mkubwa ndani ya chama hicho. Hata hivyo Chama cha ASP kilikuwa na wasomi wachache sana na kwa hivyo kukifanya kuzidi kutegemea zaidi na zaidi wasomi kutoka kwenye Chama cha TANU katika kufanya uchambuzi wa kisiasa. Hali hii ya kuwa tegemezi kwa Bara kulizidisha mvutano uliokuwepo ndani ya chama hicho kati ya Karume na wale waliomuunga mkono na Washirazi wa Pemba.

Wakati huohuo Chama cha ASP kilianza kuchochea chuki za kikabila. Miezi tisa ya awali ya mwaka wa 1958 iligubikwa na mvutano wa kikabila. Makada wa Chama cha ASP walianza kuwaandama Waarabu waliokiunga mkono Chama cha ZNP, wakipanga mipango ya kususiwa kwa maduka yao ya mashamba jambo lililosababisha mamia ya wenye maduka Waarabu kufunga biashara zao, na kuwatisha Waarabu waliomiliki mashamba madogo madogo. Mabwana wamiliki mashamba wa Kiarabu walilipiza kisasi kwa kuwafukuza wakulima wasiokuwa na ardhi kutoka katika mashamba yao.

Hatimae, mwezi Septemba 1958, masuala ya mvutano kati ya Waarabu na Waafrika visiwani Zanzibar na mgogoro kati ya vyama vikubwa viwili yalizungumzwa kwa muktadha wa Umajumui wa Afrika. Chama cha Umajumui wa Afrika cha Kupigania Uhuru katika Afrika ya Mashariki na ya Kati (PAFMECA) kilipokuwa katika mkutano wake wa uzinduzi wa chama hicho Mwanza, Tanganyika, wajumbe kutoka vyama vyote, cha ZNP na cha ASP walihudhuria. Machafuko ya Zanzibar kati ya wafuasi wa vyama viwili hivyo yalikuwa ni miongoni mwa masuala yaliyojadiliwa. Chama cha ZNP kiliwasilisha nia yake ya kujaribu kujenga chama cha mchanganyiko wa watu wa makabila mbalimbali chenye kupinga ukoloni, wakati chama cha ASP kiliwasilisha msimamo wake wa kutaka kucheleweshwa kwa uhuru kwasababu kilihisi kuwa nchi haikuwa tayari. Hatimae, baada ya kipindi kirefu cha majadiliano, PAFMECA ilitoa agizo kuwa, pale ambapo zaidi ya chama kimoja katika nchi ni mwanachama wa PAFMECA, basi vyama hivyo vishirikiane ndani ya Kamati ya Uhuru itakayokuwa na wajumbe walio viongozi kutoka katika vyama vyote viwili. Hili lilionekana kuwa lingelizuia mpasuko wa ndani ambao wakoloni wangeliutumia.

Kuanzishwa kwa Kamati ya Uhuru kulileta kipindi cha masikilizano kati ya Chama cha ZNP na cha ASP ikidhihirisha wazi kuwa hapo awali viongozi wa kisiasa walihusika sana katika kuchochea mvutano wa kikabila. Viongozi wa vyama viwili hivyo waliitembelea nchi pamoja, walilaani vitendo vya uhasama wa kikabila na walizungumzia juu ya umuhimu wa umoja na nia yao ya kuunda ‘umoja wa kizalendo kwa Zanzibar’ (Lofchie, 1965: 191). Matukio ya ususiaji wa maduka na ufukuzwaji mashambani yalisita na mivutano ya kikabila ilisita takriban mara moja.

Huu ulikuwa ni wakati ambao Chama cha Umoja wa Umajumui wa Afrika kilikuwa kinazidi kuwa na nguvu – kikaanzisha kipindi cha mshikamano na umoja kati ya mapambano mbalimbali dhidi ya ukoloni katika Afrika. Mwezi Disemba 1958 Mkutano wa Kwanza wa Nchi Zote za Afrika (AAPC) ulifanyika Accra, Ghana.

Katika muhtasari wa kumbukumbu ambazo hakupata muda wa kuziandika, Babu anatueleza kwa ufupi juu ya kipindi hicho cha msisimko. Ujumbe wa Wazanzibari, wakati ukielekea Accra, ulisimama kwa muda hapo Leopoldville ambayo wakati huo ilikuwa Kongo ya Ubeligiji. Katika jiji hili lililogubikwa na ukoloni wa Kibelgiji ujumbe wa Wazanzibari ulipata fursa adhimu ya kukutana na Patrice Lumumba. Baada ya kuuliza uliza kwa hadhari kubwa kwa wafanyakazi katika hoteli yao kuhusu vuguvugu la kisiasa katika nchi hiyo, walifanikiwa na kutoka usiku sana mpaka kwenye klabu ya usiku iliyokuwepo katika eneo la Waafrika katika jiji hilo la kikoloni lililokuwa limegawika kwa misingi ya ubaguzi mkubwa wa kikabila. Huko walikutana na Lumumba na makomred wake ambao mpaka wakati huo kwasababu ya mbinu za Wabeligiji walikuwa wametengwa kabisa na harakati zote za vuguvugu la Umoja wa Umajumui wa Afrika. (Babu, [1987b] 2002: 64).

Kuhudhuria Mkutano wa Nchi Zote za Kiafrika (AAPC) lilikuwa ni tukio lisiloweza kusahaulika kwa wafuasi wa siasa za mrengo wa kushoto wa Chama cha ZNP, kama alivyoandika Babu:

Kukutana na Nkrumah kwa mara ya kwanza lilikuwa ni tukio la msisimko mkubwa … Hili lilifungua mlango wa kukutana na Sekou Toure, shujaa wa Kiafrika wa wakati huo ambaye ndo kwanza amemaliza kupiga kura ya ‘hapana’ dhidi ya ujeuri na utawala wa Wafaransa katika Afrika ya Magharibi. Frantz Fanon alikuwa katika hali ya juu kabisa ya ukakamavu wake na alifanikiwa katika kuibadili mada ya Mkutano wa Nchi Zote za Kiafrika kutoka mapambano ya kupigania uhuru ‘kwa njia ya amani’ na kuwa mapambano ‘kwa namna yoyote ile’. Dk. Moumie wa Chama cha UPC cha Kamerun alikuwa mwenyekiti jasiri wa Kamati ya Siasa ya Mkutano wa Nchi Zote za Kiafrika iliyotengeneza Mkakati wa Afrika wa ukombozi na umoja miongoni mwa vyama vinavyopigania uhuru. (Babu, 1996: 326)

Kama kawaida yake, katika maelezo haya Babu hakueleza mchango wake yeye mwenyewe. Mwanazuoni mashuhuri na Mwanasheria Bereket Habre Selassie alikuwa na kumbukumbu hii kuhusu Babu wakati wa Mkutano wa Nchi Zote za Kiafrika.

Kwa vijana Waafrika kama mimi wakati huo, ulikuwa ni wakati wa kujieleza waziwazi na ambao mara moja unaweza kuelewa na kupata msisimko. Babu aliwasili akiwa kiongozi wa ujumbe wa chama cha siasa cha kimaendeleo cha Wazanzibari. Yeye na Lumumba walituvutia sisi tuliokuwa vijana na tusiokuwa na uzoefu, kwa unyenyekevu wao na umakini wao wa kusikiliza mawazo yetu pamoja na namna walivyotoa maoni yao kwa ujasiri na kubadilishana maarifa yao. Ari hii ya unyenyekevu pamoja na moyo wa kujitolea ulimfanya Babu apendwe na kuwavutia vijana wa Kiafrika. (Habre Selassie, 1996: 333)

Wakati wa mkutano huo Kwame Nkrumah na George Padmore waliandaa mkutano mahsusi nyumbani kwa Nkrumah ili kuimarisha umoja kati ya vyama vya ASP na ZNP. Mkutano huo ulihudhuriwa na Ali Muhsin na Karume wakiwakilisha vyama vya ZNP na ASP mutawalia, pia ulihudhuriwa na Babu akiwa katibu wa Kamati ya Ukombozi na Kanyama Chiume wa Chama cha Congress Party cha Malawi akiwa mwakilishi rasmi wa Umoja wa Umajumui wa Afrika kwa Uhuru wa Afrika ya Mashariki na ya Kati – PAFMECA.

Wakati wa mkutano huu, Karume alielezea wasiwasi wake juu ya uwezekano wa kutokea mgawanyiko katika chama chake kwasababu tawi la Pemba lililoongozwa na Mohamed Shamte lilikwishaeleza juu ya chuki yao dhidi ya kufanya kazi na Chama cha ZNP. Mwisho wa mkutano, Ali Muhsin na Karume walitia saini kile kilichoitwa Makubaliano ya Accra. Ndani ya makubaliano hayo walikubaliana kuunga mkono umoja wa ASP/ZNP na kutounga mkono kikundi chochote kitakachojitenga kutoka katika chama chochote kati ya vyama viwili hivyo – pindipo kujitenga huko kutatokea ikiwa ni matokeo ya utekelezaji wa makubaliano hayo ya Kamati ya Uhuru

Muungano wa Tamaa wa Wafuasi wa Siasa za Mrengo wa Kulia

Hata hivyo, kabla haukutimia hata mwaka mmoja baada ya kutia saini Makubaliano ya Accra, vikundi vya Chama cha ASP vilikaidi kuendelea kushiriki katika Kamati ya Uhuru.

Katikati ya mwezi wa Aprili, Umoja wa Umajumui wa Afrika kwa Uhuru wa Afrika ya Mashariki na ya Kati ulifanya mkutano Zanzibar na katika mkutano huo viongozi wa Umoja huo wa Afrika walisihi sana kuwepo kwa umoja. Katika mkutano huo, Nyerere ambaye miaka michache tu iliyopita alisaidia katika kuanzishwa Chama cha ASP kikiwa chama cha upinzani kwa Chama cha ZNP, sasa aliwakosoa Wazanzibari kwa kutokuwa na umoja katika kupigania uhuru. Aliuambia mkutano huo kuwa ‘mazingira ya mabwana na watwana bado yangalipo Zanzibar … 

 

Accra, Mkutano wa Nchi zote za Afrika 1958. Kutoka kushoto kuenda kulia, Kanyama Chiume, Malawi; Joshua Nkomo, Zimbabwe; Hasting Banda, Ma- lawi; Kenneth Kaunda, Zambia; Abdulrahman Mohamed Babu, Zanzibar.
Accra, Mkutano wa Nchi zote za Afrika 1958. Kutoka kushoto kwenda kulia, Kanyama Chiume, Malawi; Joshua Nkomo, Zimbabwe; Hasting Banda, Malawi; Kenneth Kaunda, Zambia; Abdulrahman Mohamed Babu, Zanzibar.

Kisiasa vyama vyote vinakubaliana juu ya lengo moja lakini vinapingana kwasababu ya ukabila’ (Lofchie, 1965; 191). Mabadiliko haya ya mawazo yanadhihirisha wazi juu ya jinsi Nyerere alivyotanabahi kuwa Chama cha ASP (kilichokuwa kikitawaliwa na TANU) kisingeliweza kuiongoza Zanzibar hadi kupatikana kwa uhuru peke yake na kwa hivyo, lazima ishajiishwe uwepo umoja na Chama cha ZNP. Juu ya maelezo haya, wale waliokuwemo ndani ya Chama cha ASP ambao walipinga ushirikiano na ZNP hawakubadili mtazamo wao.

Mwezi Juni 1959, lilikuwepo jaribio jingine la kuwashawishi wapinzani hawa. Kama inavyofichua ripoti ya kijasusi ya Uingereza ya mwezi June 1959, Karume aliitisha mkutano wa siri Zanzibar na Rashidi Kawawa, wakati huo akiwa mjumbe wa Kamati Kuu ya TANU alihudhuria. Siku tatu za mwanzo, ni maendeleo machache tu yaliyopatikana ambapo wajumbe wa kutoka Pemba Othman Sharif, Mohamed Shamte, Ali Shariff na wengine wakiwa na wasiwasi na haja ya kuwepo ushirikiano na Chama cha ZNP. (Ofisi ya Kumbukumbu za Serikali, 1959: 6). Halafu tena, tarehe 28 Juni, nyaraka hizi za Uingereza zinazidi kuelezea:

Abeid Karume alitoa waraka katika mkutano huo uliotiwa saini na Julius Nyerere na kudai kuwa ni taarifa juu ya sera ya TANU. Inasemekana kuwa ilikubaliwa na wajumbe wa PAFMECA wa Kenya, Uganda na Shirikisho la Afrika ya Kati … Waraka huo ulieleza:

a) Kuwa jumuiya ya Afro-Shirazi haina haja ya kuogopa matokeo yatakayotokana na ushirikiano na Chama cha Nationalist katika harakati za kupatikana kwa uhuru, kwasababu wote wanatambua kwamba Afro-Shirazi ndio wamiliki halali wa Zanzibar;

b) Kuwa jumuiya ya Afro-Shirazi haina haja ya kuogopa matokeo ya upatikanaji wa uhuru mapema kwa misingi ya hali ya kielimu kwasababu Chama cha TANU kitahakikisha kuwa Waafrika wasomi kutoka Zanzibar wanaofanya kazi katika Idara za Serikali za Tanganyika wanarudi kukitumikia Chama cha Afro-Shirazi pale uhuru utakapopatikana;

c) Kuwa hatimaye, baada ya kupatikana uhuru wa Tanganyika na Zanzibar, nchi mbili hizo zitaunganishwa pamoja na kuwa nchi moja ya Jamhuri ya Afrika;

d) Kuwa Chama cha Afro-Shirazi lazima kitambue kuwa jumuiya nyingine za Wazanzibari zina haki za kisiasa;

Waraka huo ulihitimishwa kwa kuwataka Abeid Karume na Othman Shariff kutia saini zao, ikiwa sera hiyo imekubalika, na wote walitia saini zao.

Hali hii ya kuhakikishiwa na TANU iliondoa kabisa kila hofu iliyokuwepo kuhusu matarajio ya kisiasa ya jumuiya ya Afro-Shirazi na ilikubaliwa kuwa … majadiliano ya siku chache zilizopita, pamoja na waraka wa TANU yatakuwa ni siri kubwa.

(Ofisi ya kumbukumbu za Serikali, 1959: 6-7)

Waraka huo ulipata mafanikio yaliyotarajiwa. Wajumbe wote wa kamati ya utendaji ya ASP, ikiwa pamoja na Othman Shariff na Mohamed Shamte, walikula kiapo kuwa hawatauvuruga umoja wa Chama cha ASP.

Ingawa wajumbe kutoka Pemba walikwenda kinyume na kiapo chao mara tu baada ya tukio hilo, hata hivyo mkutano huo umeonekana kuwa ni mmoja kati ya mikutano iliyokuwa na umuhimu mkubwa. Ulipata muhuri wa uthibitisho wa Nyerere kwa dhana ya kuwa Chama cha Afro-Shirazi (na si kikundi kingine chochote) ndio wamiliki halali wa Zanzibar na kuthibitisha ushirikiano wake katika kufikia lengo – kuwa baada ya kupatikana uhuru wa Tanganyika na Zanzibar nchi mbili hizo zitaunganishwa pamoja ili kuwa nchi moja ya Jamhuri ya Afrika. Inaonekana kuwa Uingereza ilihusika na mchakato wote huu.

Ilipofika mwaka 1959 wafuasi wa Chama cha ASP walianza tena kuwashambulia Waarabu, na wakati huo huo wafuasi wa siasa za mrengo wa kulia wa Chama cha ZNP ambao siku zote walikuwa wakiipinga Kamati ya Uhuru, walianza kuchochea chokochoko za kikabila. Katika duru ya pili ya machafuko ya kikabila, mabwanashamba wengi ndani ya Chama cha ZNP walianza kuwafukuza wakulima wasiokuwa na ardhi kutoka katika mashamba yao.

Katika kipindi cha miezi michache tu, mwezi Disemba 1959, ule mgawanyiko ambao Karume aliogopa kutokea, ulitokea. Kundi la Pemba la chama, likidhibitiwa na Washirazi waliokuwa na ushawishi mkubwa – wakulima matajiri, wafanyabiashara, wenye maduka na wamiliki wa magari ya abiria, wakiongozwa na Mohamed Shamte ambaye alikuwa ni mmoja miongoni mwa wale waliokuwa wakipinga kwa nguvu zote ushirikiano na Waarabu, walikiacha Chama cha ASP na kuanzisha chama kipya; chama cha Zanzibar and Pemba People’s Party (ZPPP)

Wakati huo huo, wafuasi wa siasa za mrengo wa kulia ndani ya Chama cha ZNP walionyesha hali yao halisi, waliyavunja Makubaliano ya Accra na kushirikiana kwa hamu kubwa na ZPPP ili kujenga umoja. Shamte, bila ya kujali, aliuacha msimamo wake wa awali na kulikubali shauri hilo.

Mgawanyiko ndani ya Chama cha ASP ulitokea wakati mbaya sana kwa wafuasi wa siasa za mrengo wa kushoto. Kamati ya Uhuru ilikuwa katika mapumziko na Babu, katibu wake alikuwa safarini Cairo kufanya mazungumzo ya kufungua ofisi ya ZNP. Alipanga kwenda China vile vile kwa ziara rasmi ya kuonana na uongozi wa juu kabisa wa Chama cha Kikomunisti cha China, safari ambayo hakuweza kuivunja. Kama alivyoandika hapo baadae, Babu alishtushwa na unafiki wa uongozi wa ZNP:

Kazi yetu ngumu ya kujenga umoja wa watu wa Zanzibar ghafla ilivurugika. Kama kwamba hali hii haikuwa mbaya vya kutosha, habari za kushtua zaidi zilikuja kutoka katika chama changu mimi mwenyewe, kuwa Chama cha ZNP kimeukaribisha mgawanyiko huo na kuwa viongozi wetu wanashirikiana kikamilifu na viongozi wa ZPPP katika kukipinga Chama cha ASP…. Tulikuwa tunashuhudia mwisho wa umoja wetu tulioulea kwa hadhari kubwa kati ya vyama vyetu. Ulikuwa ni ushindi kwa wapinga maendeleo wa kutoka katika vyama vyote viwili na kumalizika kwa utulivu wa kisiasa wa Zanzibar. (Babu, 1995: 5)

Kipindi hiki muhimu katika historia ya Zanzibar kilikumbwa na mambo mengi, lakini kubwa katika yote ni mabadiliko ya wanachama katika vyama. Wakati nchi ikikaribia uchaguzi na kufuatiwa na mamlaka ya serikali ya ndani, idadi ya wanachama wa vyama vyote viwili na hasa Chama cha ZNP ilizidi kuongezeka. Wanachama wapya wa ZNP mara nyingi walikuwa ni watumishi wa serikalini ambao sasa waliona mustakbali wao mpya katika siasa ni amali yao. Kujiingiza kwao kuliwaimarisha kwa kiwango kikubwa wafuasi wa siasa za mrengo wa kulia ndani ya chama na kuwafanya kuwa wapinzani wakubwa wa siasa za ukomunisti. Baada ya utumishi wa muda mrefu katika serikali ya kikoloni, na wakiwa na wasiwasi na ushawishi wa Bara kuwa labda utawapokonya kazi walizokuwa wakizitarajia, waliuona ushirikiano na Chama cha ZPPP kuwa ndiyo fursa yao ya kushinda uchaguzi utakaowapelekea kupata nafasi muhimu serikalini.

Ama kwa Chama cha ZPPP, viongozi wake wengi walikuwa wakulima matajiri na wasomi kutoka Pemba (ambao walihisi wametengwa kwasababu ya ushawishi wa wasomi kutoka bara ndani ya ASP). Sasa Zanzibar ikashuhudia vichekesho vya viongozi wa zamani wa ASP waliokuwa na chuki na hofu dhidi ya Waarabu wakijiunga kwa hamu na wale waliokuwa wakiwaepuka, kwasababu za maslahi ya kibinafsi.

Kuondoka kwa wasomi kutoka Pemba kulikiwacha chama cha ASP kikawa hakina kabisa wasomi Wazanzibari, na inawezekana kuwa kwasababu hiyo uongozi wa chama hicho ulizidi kuitegemea TANU na Chama cha Wahindi (hasa Wahindi wafanyabiashara matajiri kutoka Pemba ambao walikuwa na ushawishi mkubwa ndani ya chama) kwa misaada na ushauri

Mikakati ya Wafuasi wa Siasa za Mrengo wa Kushoto Katika Mazingira ya Kupinga Maendeleo

Katika kipindi hiki cha kutoelewana na kuzuka kwa vitendo vya uhasama vya mara kwa mara kutoka kwa wafuasi wa siasa za mrengo wa kulia wa chama na serikali ya kikoloni, wafuasi wa siasa za mrengo wa kushoto walifikiria mikakati mbalimbali iliyoyumkinika. Kutokana na mtazamo wao wa kuwa ukoloni ndiyo mgogoro wao mkubwa, hawakuyaona mapambano dhidi ya Chama cha ASP kuwa ndiyo muhimu, hasa kwa kuwa chama hicho wakati huo kilikubali kushiriki kikamilifu katika mapambano ya kupigania uhuru. Hii iliwafanya baadhi yao kufikiri kuwa ingelikuwa vyema kama wao wote kwa ujumla wao wangelijiunga na Chama cha ASP. Lakini wengi wao waliamini kuwa ni muhimu kubaki katika Chama cha ZNP, chama ambacho wao wenyewe walifanyakazi kwa bidii kukianzisha, na kupambana sana ili kukirudisha katika mkondo wa kimapinduzi.

Mapambano ya kiitikadi katika kipindi hiki yalifuata mfumo wa uchambuzi wa Kimarx uliojengwa juu ya muundo wa matabaka, lakini uchambuzi huu haukuwa wa kutoka kwenye vitabu. Ulikuwa ni matokeo ya mahusiano ya kimigogoro yaliyojengeka kati ya nadharia na uzoefu wa vitendo. Kwa mfano, kuhusiana na tatizo la kuwaandaa wafanyakazi wa mjini ambao walikuwa na uhusiano mkubwa na Bara, Babu alieleza kuwa mshikamano wao wa kitabaka na wafanyakazi wengine haukuwa na uhakika na ulikuwa na shida ya kuweza kuendelea. Kwa mfano walikuwa ni kikwazo katika mapambano kati ya wafanyakazi wenyeji na waajiri. ‘Kuunga mkono kwao Chama cha ASP kwanza kulikuwa na nia ya kujilinda; na uzalendo wao ulikuwa ni wa kikabila zaidi kuliko wa kisiasa. Utiifu wao kwanza ulikuwa kwa Chama cha TANU na kwa nadra tu kwa Chama cha ASP’ (Babu, 1991: 234). Wafuasi wa siasa za mrengo wa kushoto, wakiwa hawakujihusisha nao moja kwa moja, ilibidi wawaonyeshe mshabihiano uliokuwepo kati ya mapambano ya tabaka la wafanyakazi wa Zanzibar na wa Bara na kuwa tofauti zake zinatokana na mazingira tofauti tu visiwani Zanzibar. Kwa maneno mengine, ilibidi wawaelimishe juu ya nadharia na harakati za mapambano ya kitabaka.

Ama kwa wafanyakazi wazawa, wakiwa wamekabiliwa na tishio la kupoteza ajira na nafasi zao kuchukuliwa na wafanyakazi kutoka Bara, walijenga uhasama mkubwa dhidi ya wabara; na kwa mantiki hiyo kuwa hatarini na kuathiriwa na propaganda za wafuasi wa siasa za mrengo wa kulia wa ZNP na ZPPP dhidi ya wabara. Hii ingelizidisha mripuko wa uadui wa kikabila ambao tayari ulikwishakuwepo na kutumiwa na wakoloni.

Walikuwepo vile vile wakulima waliokuwa wanachama wa Chama cha ZNP ambao ndio walioweka msingi wa chama hicho. Sio wote walioelewa juu ya mgogoro ndani ya chama na wafuasi wa siasa za mrengo wa kushoto walikuwa katika mtihani mkubwa. Kuuzungumzia mgogoro huo rasmi hadharani kungelikidhoofisha chama na jambo hilo lingelitumiwa na wakoloni. Kwa upande mwengine, wakati mapambano ya kimapinduzi yakipamba moto ilikuwa ni muhimu kuwa wanachama hawajikuti katika hali ya kushitukizwa.

Haya ndiyo mapambano ya kiitikadi ambayo wafuasi wa siasa za mrengo wa kushoto walikuwa wakipambana nayo. Je, wangelibidi wajitoe kutoka katika Chama cha ZNP na kuanzisha chama kingine wakati huu? Je, ilikuwa ni kosa kuendelea kuwemo ndani ya Chama cha ZNP katika kipindi hiki?

Wakati mtu angelishawishika kufikiri hivyo, na kudhani kuwa chama cha Umma Party kama kingelikuwa kimeanzishwa wakati huo, basi kingelikuwa na muda wa kujiimarisha angalau kwa miezi michache zaidi kabla ya uhuru, na siasa za Zanzibar zingelichukua mkondo tofauti kabisa, lakini hali halisi ya kisiasa ya wakati huo haikuonyesha ishara yoyote kuwa hilo lingeliwezekana.

Chini ya utawala wa kikoloni, hasa wakati wa vita baridi kiwango cha ukandamizaji dhidi ya wafuasi wa siasa za mrengo wa kushoto kililifanya hilo kuwa ni la taabu sana na isingeliwezekana kwa chama cha mrengo wa kushoto kuwepo. Wanasiasa binafsi waliokuwa waumini wa siasa za mrengo wa kushoto ilibidi waendeshe harakati zao ndani ya chama cha kizalendo kinachopinga ukoloni na kudhihirisha kwa tabia zao, uaminifu na moyo wa kujitolea, sifa za wazi za uongozi kama huo. Hili ndilo lililoweka msingi wa ujenzi wa uongozi wa Kimarx wa baadae. Hii ndiyo maana kujitoa katika Chama cha ZNP na kuanzisha chama cha Umma Party haukuwa uamuzi rahisi, na ndiyo maana wafuasi wa siasa za mrengo wa kushoto hawakuchukua hatua hiyo katika kipindi hiki. Babu alieleza juu ya baadhi ya masuala yanayohusiana na uamuzi huo katika barua aliyomwandikia Karim Essak (angalia Babu, [1982a] 2002).

Vile vile, shughuli za wafuasi wa siasa za mrengo wa kushoto zilizidi kuwa ngumu kwasababu ya kupungua kwa kasi kubwa, ule utulivu mdogo wa wasiwasi wa kikabila uliokuwepo. Mara baada ya mgawanyiko ndani ya Chama cha ASP, kampeni nyengine ya kikabila dhidi ya Waarabu ilianza. Wafuasi wa siasa za mrengo wa kulia wa Chama cha ZNP, ambacho wakati huo kilikuwa na sauti kubwa, walijibu kwa kutoa hotuba dhidi ya Waafrika, wakati chama cha ZPPP kilianza kupiga propaganda dhidi ya wabara.


  1. Kiasi cha watumwa 23,000 walikuwa wakisafirishwa kutoka Zanzibar katikati ya miaka ya -1860 – ijapokuwa hii ni chini ya nusu ya wastani wa kila mwaka wa biashara ya utumwa katika Bahari ya Atlantik kwa zaidi ya miaka 200. Angalia Hickman, Sheriff na Alibhai- Brown (2010: 180)
  2. Makala katika gazeti la Al Falaq la tarehe 23 Septemba 1953 yalieleza kuwa’ uchaguzi kwa wote ... bila ya kujali maslahi ya kila jamii ... ndicho kitu kinachotakiwa na taifa la Wazanzibari ... yalieIeza kuwa bado hatuna sifa ya kuwa na uwakilishi wa kweli —. Upumbavu ulioje!’ (Makavazi ya Taifa ya Zanzibar).
  3. Wakulima wa tabaka la kati, kama wakulima matajiri, ni wakulima ambao ama wanamiliki ardhi yao yote, au sehemu ya ardhi hiyo na nyengine kuikodisha. Hata hivyo, wakulima matajiri wanamiliki ardhi zaidi na zana bora zaidi za kilimo, na wakati wakulima wa tabaka la kati hupata mapato yao hasa kutokana na jasho lao wenyewe na hawawanyonyi wengine, wakulima matajiri hutegemea kwa kiasi fulani au hata kwa jumla katika kuwanyonya wengine, ama kwa kukodi vibarua au kwa kukodisha ardhi.
  4. Mara baada ya kurudi Zanzibar, Babu alikuwa vile vile mwandishi wa Afrika ya Mashariki wa Shirika la Habari la China- Xinhua.
  5. Baadhi ya wanachama wa Chama cha Umma Party baadae walibadili msimamo wao wa kisiasa na mmoja wao ni Salim Ahmed Salim, aliyejiunga na CCM na kushika nyadhifa mbalimbali za ngazi za juu katika serikali ya Tanzania.

License

Tishio la Ukombozi Copyright © 2016 by Amrit Wilson. All Rights Reserved.

Share This Book

Feedback/Errata

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *