3 Mapinduzi ya Zanzibar na Hofu za Wabeberu

Ijapokuwa wanachama wa Chama cha Umma Party walikuwa mara kwa mara wakizungumza juu ya mbinu za mapinduzi lakini wao wenyewe hawakupanga wala hawakujua chochote cha maana juu ya mapinduzi ya Zanzibar. Babu alikuwa bado yupo Dar es Salaam yalipotokea mapinduzi tarehe 12 Januari, 1964.

Usiku wa siku ya Jumamosi tarehe 11 Januari, Karume na Aboud Jumbe ambaye wakati huo alikuwa ndiye kiongozi wa wajumbe wa ASP katika Baraza la Kutunga Sheria, waliliarifu Tawi Mahasusi la makachero kuwa walikuwa na taarifa kuwa zingelitokea vurugu za namna Fulani usiku wa siku hiyo na kwamba wao wala ASP hawahusiki (Shivji, 2008: 47) Ni wazi kuwa Karume alikuwa na wasiwasi kuwa kama mapinduzi yasingelifanikiwa angelilaumiwa, na alikuwa akichukua hadhari ya kujitenganisha na tukio hilo. Kutokana na taarifa hizi J.M.Sulivan, kamishna wa polisi, alipeleka walinzi wachache kwenye nyumba ya Ali Muhsin na kwenye kasri ya Sultani.

‘Machafuko’ ambayo Karume alimuonya kamishna yalitokea saa 8 za usiku na alfajiri ya Jumapili, kwa mashambulizi yaliyofanyika pale bomani Ziwani na kutekwa chumba chake cha silaha. Baadae yalifuata mashambulizi katika kambi ya Mtoni.

Hatua ya kwanza iliyochukuliwa na serikali ya Uingereza kufuatia mashambulizi, mapema tarehe 12 Januari ilikuwa ni kutilia nguvu wito wa serikali ya Zanzibar kwa Nyerere na Kenyatta wa kuongezwa nguvu za vikosi vya polisi na kuitaka Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani kufanya hivyo hivyo. Wasiwasi mkubwa wakati huo ulikuwa juu ya maisha ya Waingereza na mali zao, na siyo kuisaidia serikali ya Zanzibar (ambayo ilionekana kuwa imenywea). Saa chache baadae, Balozi wa Uingereza alituma simu ya upepo iliyoonyesha wasiwasi mkubwa kwenye Ofisi ya vita ya Uingereza akiomba vitumwe vikosi vya jeshi la Uingereza.

Waziri Mkuu ameniomba vipelekwe vikosi vya Uingereza haraka iwezekanavyo kwa minajili ya kuwa maisha na mali za Waingereza vimo au karibu vitakuwa hatarini. Ninaelewa shida ya kikatiba ya kupeleka vikosi vya Uingereza katika nchi iliyo huru, lakini kuna uwezekano wa hali kuwa mbaya zaidi mpaka hapo vikosi vya kuongeza nguvu vitakapofika Zanzibar kwa haraka kutoka Kenya na Tanganyika, nchi ambazo pia serikali ya Zanzibar imeziomba kufanya hivyo. Kama mnahisi kuwa hamuwezi kuitikia wito huu kwa haraka basi kwa uchache fanyeni mpango wa kuwepo kwa usafiri wa ndege hapo Dar es Salaam. (Imenukuliwa kutoka Wilson, 1989: 13)

Usiku ule ule Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilipata habari kuwa vikosi vya Kenya vinaruka kuelekea Zanzibar, kuwa kituo cha NASA hakikuguswa na kuwa kikosi cha pamoja cha majeshi ya Kenya, Tanganyika na Uganda kitapelekwa ‘kurudisha utulivu Zanzibar’. Hata hivyo, juu ya haya, Mkuu wa Majeshi wa Marekani aliagiza manowari USS Manley, iliyokuwepo Mombasa, kwenda Zanzibar. Saa nne baadae USS Manley iliamriwa kurudi, na saa nne tena baadae iliamriwa kurudi tena Zanzibar. Kusema kweli, hakuna Mzungu aliyedhuriwa na hakuna mali iliyomilikiwa na Wazungu iliyoharibiwa wakati wa mapinduzi (Shivji, 2008: 49).

‘Waasi’ kama Waingereza walivyoamua kuwaita, wengi wao walikuwa ni wanachama wa Umoja wa Vijana wa Chama cha ASP, pamoja na idadi kubwa ya vijana wahuni wenye hasira wasiokuwa na ajira, wakisaidiwa na maafisa wa polisi wa zamani waliokuwa na uchungu. Walipata fursa ya awali ya kupambana na polisi wapya ambao walikuwa ndo kwanza wameajiriwa, lakini baada ya muda, wakitumia mbinu za kushitukizia, polisi walianza kuwapiga risasi na kuwaua vijana “waasi” wasiokuwa na uzoefu. Hapo ndipo vijana wa Chama cha Umma Party walipoingia katika medani ya mapambano. Walichukua uongozi, wakiwaonyesha vijana wasiokuwa na uzoefu mbinu na mikakati ya vita vya mjini. Hashil Seif, mjumbe wa Kamati Kuu ya Umoja wa Vijana wa Chama cha Umma Party, ambaye awali alikuwa mwanachama wa Chama cha ZNP na kupata mafunzo ya kijeshi na mafunzo mengine nchini Cuba anakumbuka matukio haya katika mahojiano ya mwaka 1988.

Usiku huo wa awali palikuwa na rabsha kila mahali. Watu wengi hata hawakujua nini walilokuwa wakilifanya. Moja ya mambo ambayo Chama cha Umma Party iliyafanya ilikuwa ni kufahamisha madhumuni ya mapinduzi – haikuwa kuua, kubaka au kuiba lakini kuibadilisha nchi. Baadhi ya watu walisikiliza lakini ni dhahiri kuwa si kila mtu alifanya hivyo.

Vijana wa Chama cha Umma walipangiwa majukumu na Chama cha ASP, majukumu ambayo wao wenyewe hawakujua namna ya kuyatekeleza. Sisi watatu tuliopata mafunzo Cuba tulipelekwa kwenda kuliteka gereza. Ilikuwa ni shughuli ngumu sana, wale waliojaribu kufanya hivyo kabla yetu waliuliwa lakini sisi tulifanikiwa. Halafu walitwambia tukakiteke kituo cha polisi cha Malindi. Hapa pia watu waliuliwa. Kituo hicho kilikuwa katika eneo la wazi karibu na Mji Mkongwe, karibu na eneo la bandari, kwa hivyo tuliamua kukivamia usiku. Huu ulikuwa ni usiku wa tarehe 12 Januari. Shambulio hilo liliongozwa na kijana mwengine wa chama cha Umma Party, Amour Dugheish.  (Imenukuliwa katika Wilson, 1989: 12)

Hashil alikwenda makao makuu ya kampuni ya simu ya Cable and Wireless, stesheni ya mawasiliano yote na nchi za nje. Ilikuwa katika Mji Mkongwe, eneo la chama cha ZNP kama Hashil anavyokumbuka:

Nilikuwa na watu kumi na mbili chini yangu. Tulijigawa katika makundi mawili na tukaisogelea stesheni tukiwa tumejibadili … Vyovyote vile, tulifanikiwa. Aliyekuwa muhusika mkuu hapo kwenye makao makuu ya kampuni ya simu alikuwa Muingereza. Hatukutaka kumtisha. Alikuwa amevaa nguo za ndani. Tulimwacha achukue suruali yake basi. (Imenukuliwa katika Wilson, 1989: 12)

Tukirudi nyuma hadi wakati huo, ni wazi kuwa Chama cha Umma Party kilikuwa na majukumu matatu muhimu. Mosi, kiliyanusuru mapinduzi – mapinduzi yangelishindwa bila ya chama hicho. Pili, kama Babu alivyoandika, kilisaidia kuyabadili machafuko ya ‘wahuni ambayo kwa kila namna hayakuwa na lengo la kisiasa na kuyafanya yawe machafuko ya umma, mapinduzi yenye kupinga ubeberu … uingiliaji kati wa nguvu za kisoshalisti ulijenga mazingira mazuri zaidi kwa mustakbal wa mategemeo mema ya kimapinduzi na ya kisoshalisti katika kanda yote (Babu, 1991: 245). Na tatu, kwasababu Chama cha Umma Party kiliwajumuisha Waarabu na Wahindi, kilipunguza kiwango cha mgawanyiko wa kikabila na kuzuia mashambulizi dhidi ya Waarabu kuwa ndiyo lengo kuu la machafuko hayo.

Kama Mahmood Mamdani anavyoeleza:

Chama cha Umma Party na kushiriki kwake kikamilifu katika mapinduzi ilikuwa ni hatua ya kwanza katika kuyaelekeza Mapinduzi ya Zanzibar ya 1964 katika njia iliyokuwa tofauti na ile ya ‘Mapinduzi ya Kijamii’ ya Rwanda ya mwaka 1959: pale ambapo mgawanyiko kati ya wanamapinduzi na wanaopinga mapinduzi, ulipojidhihirisha katika sura ya mgawanyiko kati ya Wahutu na Watusi katika Rwanda ya 1959, hali ya mambo ilikuwa kidogo tofauti katika Zanzibar ya 1964. Ni kwasababu ya Babu na Chama cha Umma Party ndiyo maana Waarabu Zanzibar, tofauti na Watusi Rwanda, walikuwa ni kundi lililojiandaa, siyo upande wa waliokuwa nacho tu bali pia upande wa mapinduzi. (Mamdani, 1996)

Hata hivyo, juu ya juhudi zao, wanaharakati wa chama cha Umma hawakufanikiwa kikamilifu katika kuzuia ukatili dhidi ya Waarabu uliotokea kufuatia parapaganda ya kikabila ya miaka mingi ya Chama cha ASP. Bila ya kuingia katika mjadala kuhusu idadi, ni wazi kuwa mauaji yalisambaa pamoja na ubakaji na utekaji nyara wa wanawake wa Kiarabu na wa Kihindi. Haya yalikuwa, na yalionekana kuwa, ni mashambulizi dhidi ya jamii yote ya Waarabu, ambao wengi wao hawakuwa wakandamizaji wala hawakuwa matajiri.

Palikuwa na pazia lililoficha matukio ya mashambulizi dhidi ya wanawake, labda kwasababu nchini Zanzibar, kama ilivyo katika nchi nyingi zenye mfumo dume wa kimwinyi, ubakaji huonekana kuwa ni fedheha ya familia yote. Mwanamke akibakwa familia yote hujiona kuwa imefedheheshwa na kudhalilishwa. Kaka, baba na waume hujiona kuwa wameshindwa (Napoli na Saleh, 2005). Wakati huo huo mfumo dume unatambua kuwa wanaume wa kundi fulani huwamiliki wanawake ‘wao’, na miili ya wanawake hao huwa huru na chini ya satwa ya wanaume hao na si kwa wengine. Hili ndilo lililokuwa jambo kubwa muhimu katika ukatili uliokuwa umewakabili wanawake Zanzibar.

‘Wiki ya Aibu ya Kusikitisha kwa Taifa’

Alfajiri ya tarehe 12 Januari, wakati moshi na vurugu ya mapinduzi bado umetanda hewani, Babu alirudi Zanzibar kutoka Da er Salaam. Alifuatana na Karume, ambaye aliyakimbia machafuko usiku wa manane wa siku ya Jumapili. Baada ya siku mbili majina ya wajumbe wa Baraza la Mapinduzi na wa Baraza la Mawaziri yalipitishwa. Kwenye vyombo vyote hivyo wajumbe wa ASP walikuwa ndio wengi. Kusema kweli, Baraza la Mapinduzi lilikuwa na wajumbe wawili tu kutoka katika Chama cha Umma Party, Babu na Khamis Ameir. Wajumbe wa Baraza jipya la Mawaziri walikuwa ni pamoja na Karume, aliyekuwa Rais; Abdallah Hanga, Makamo wa Rais; Babu, Waziri wa Mambo ya Nje na Biashara; Othman Shariff, Waziri wa Elimu na Utamaduni; Aboud Jumbe, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii; Idrisa Wakil, Waziri wa Kazi na Mawasiliano; Saleh Saadalla, Waziri wa Kilimo; na Abdulazizi Ali Twala na Hassan Nassor Moyo wakiwa Mawaziri Wadogo.

Pemba ilikuwa haikuhusika katika mapinduzi na ilikuwa baada ya wiki moja ndipo mapinduzi yalipojiimarisha huko. Ijapokuwa Ali Sultan Issa alikuwa ndiye msimamizi wa utawala Pemba, ni wazi kuwa hata huko madaraka yalikuwa mikononi mwa Chama cha ASP.

Juu ya nyadhifa chache walizokuwa nazo wanachama wa Chama cha Umma Party, Waingereza na Marekani waliyaona matukio ya Zanzibar kama ‘madaraka yaliyochukuliwa na wakomunisti’ jambo lililowatia wasiwasi mkubwa. Waingereza vile vile hawakufurahi kwasababu, kama alivyokumbuka J.K. Hickman, mwanadiplomasia aliyefanyakazi katika ofisi ya uhusiano ya Jumuiya ya Madola, Idara ya Afrika ya Mashariki:

Waziri wa Mambo ya Nje, Duncan Sands, alikataa katakata kuitambua serikali hii ya mapinduzi kwa namna yoyote ile. Yeye mwenyewe alijiona kuwa na utiifu mkubwa kwa Sultani kwasababu hivi karibuni alitiliana nae saini na hakutaka kufanya jambo lolote ambalo lingelikinzana na mkataba huo, kwa hivyo tulikuwa katika hali ya utata kwa muda mrefu. (Hickman, 1995)

Babu akiwa na Karume: Chanzo: Mohamed Amin/Camerapix
Babu akiwa na Karume: Chanzo: Mohamed Amin/Camerapix

Siku chache zilizofuata zilishuhudia wimbi la mabadilishano ya mawasiliano ya siri baina ya serikali za Uingereza na Marekani na Balozi za Marekani katika Afrika ya Mashariki na mipango iliyoweka wazi kuwa Nyerere amejitokeza kuwa ni rafiki mkubwa wa nchi za Magharibi. Kwa mfano, tarehe 15 Januari Dean Rusk, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani alituma simu za upepo kwa balozi za Marekani za Afrika ya Mashariki zikieleza kuwa wakati Kenya na Uganda zimeitambua serikali ya mapinduzi, Tanganyika haikufanya hivyo. Na labda serikali za Kenya na Uganda zinaweza kushawishiwa na Rais Nyerere kumuunga mkono katika kuipeleka mbele sera hii kuhusu serikali mpya.

Hata hivyo, matukio ya kusisimua yalikuwa yakibisha hodi, mambo ambayo yangelidhihirisha udhaifu wa Nyerere ndani ya nchi na kuzidi kwa utegemezi wake kwa Uingereza na Marekani

Matukio hayo yalianza tarehe 19 Januari pale wanajeshi katika kambi ya Colito, Dar es Salaam, wakiwa wamekasirika kwasababu ya mishahara yao midogo na kubakishwa kwa maafisa wa Kizungu katika vyeo vya juu walipoasi. Uasi huu ulifuatiwa na uasi wa askari polisi na mgomo wa makuli, na kuwepo kwa uwezekano wa vyama vyengine vya wafanyakazi kujiunga na mgomo huo na kupelekea kuwepo kwa mgomo wa nchi nzima. Upinzani wote huu ulidhihirisha hasira waliyokuwanayo Watanganyika wengi juu ya uendelezwaji wa miundo ya kikoloni katika nchi iliyo huru.

Kufuatia upinzani huu, Nyerere alibaki amejifungia Ikulu. Baadaye, usiku wa tarehe 24 Januari alipeleka maombi kwa maandishi kwa serikali ya Uingereza akiomba msaada wa kijeshi dhidi ya wananchi wake mwenyewe wa Tanganyika. Siku ya pili kikosi cha Uingereza kilitua na kuipiga mabomu kambi hiyo na kuushinda uasi. Hatimaye, tarehe 26 Januari, Nyerere alilihutubia Taifa. Hotuba yake, ijapokuwa ilikuwa kwa sauti iliyojaa busara na ya kiualimu, ikihalalisha kwa hasira hatua aliyochukua, ilikuwa inakaribia kukiri udhaifu wake na utegemezi wake kwa nchi za magharibi katika hali ambayo kwa kweli ilikuwa nje ya udhibiti wake:

Nasikia kuna maneno ya kijinga kuwa eti Waingereza wamerudi kuja kuitawala tena Tanganyika. Huu ni upuuzi mtupu … Nchi huru yoyote ile inaweza kuomba msaada kutoka nchi huru nyengine. Kuomba msaada kwa namna hii si kitu cha kujivunia. Sitaki mtu yeyote adhani kuwa nilifurahi kufanya jambo hili. Wiki hii nzima ilikuwa ni wiki ya aibu ya kusikitisha kwa Taifa letu. (Imenukuliwa kutoka Wilson, 1989: 30)

Marekani Inaandaa Mikakati Mipya kwa Afrika

Wakati huo huo, Marekani ikiwa imejawa na wasiwasi kuwa kuna uwezekano kwamba hali ya Zanzibar ina uhusiano na uasi wa Tanganyika, uasi ambao ungeliweza kusambaa Afrika ya Mashariki nzima, iliandaa waraka wa sera mpya kuhusiana na hali ya kutia wasiwasi katika nchi tatu za Afrika ya Mashariki hali ambayo itailazimisha nchi hiyo kuchukua hatua za haraka na kuandaa mpango wa dharura.

Waraka huo ulianisha vipengele kadha vya kuchukuliwa hatua miongoni mwao ikiwa ni kukilinda kituo cha kufuatilia vyombo vya sayari cha Mercury na kumuimarisha Nyerere, kwasababu ‘Lengo letu kuu ni kuimarisha nafasi ya Nyerere … Nyerere anaweza kuhitaji namna fulani ya mpango mpya ili kuimarisha madaraka yake.’ (Imenukuliwa kutoka Wilson, 1989: 26)

Ili kupata suluhisho kwa tishio hili Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilitayarisha mkakati wenye ncha mbili. Kwanza, uliisukuma Uingereza kupeleka jeshi ili kuvivamia visiwa vya Zanzibar (ule ulioitwa Mpango wa Utekelezaji wa Zanzibar), mpango ambao ilidhaniwa kuwa Karume angeliuunga mkono. Pili ulijaribu kumfanyia hila Karume na wengine wakubali kuwepo kwa muungano chini ya uongozi wa Nyerere mfuasi wa siasa ya ‘wastani’. Zaidi ya hayo, Dean Rusk aliwatumia simu mabalozi wa Marekani waliopo nchini Tanganyika, Uganda na Kenya tarehe 5 Machi akiwaelekeza kuwa wawatake Nyerere, Obote na Kenyatta kumweleza Karume juu ya hatari iliyopo kwa Chama cha ASP kumtegemea Babu, na kupendekeza kuundwa kwa Shirikisho la Zanzibar na Tanganyika.

Tatizo kubwa hapa ni kuwa Karume mwenyewe anamwamini sana na kumtegemea Babu… na Nyerere alisema kuwa Karume anamuhitaji Babu ambaye juu ya usuli wake ni lazima afanye naye kazi… Je itakuwa na maana yoyote kuongea na Nyerere, ambaye hapo awali alikwishakataa na, kumletea wazo la Shirikisho la Zanzibar na Tanganyika ikiwa ni njia mojawapo ya kumuimarisha Karume na kupunguza ushawishi wa Babu? Hatua kama hiyo itamsaidia na Nyerere vile vile katika nafasi yake. (Imenukuliwa katika Wilson, 1989: 48, hati za mlalo zimeengezewa)

Wiki chache kabla ya hapo, ayari mkubwa wa Kimarekani na mchafuzi wa serikali zenye kupenda maendeleo, Frank Carlucci, alifika Zanzibar. Aliwasili moja kwa moja kutokea Congo ambako Shirika la Kijasusi la Marekani lilishiriki kikamilifu katika kumpindua Lumumba, na hii inaonyesha wazi uzito gani Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Marekani ulivyoyapa mapinduzi ya Zanzibar. Congo, kwa wakati huo lilikuwa ndiyo tukio la mwisho katika idadi ya vurugu za Carlucci likiwa limetanguliwa na Brazil na Ureno. Sasa, madhumuni yake, kwa mujibu wa maneno yake mwenyewe yalikuwa ni kuizuia Zanzibar isiwe ‘Cuba ya Afrika ambayo uasi wake ungelisambaa bara zima’ (imenukuliwa katika Wilson, 1987: 41). Yeye na watumishi wengine wa Marekani walijaribu kuiimarisha nafasi ya Karume, wakijaribu kuleta mgawanyiko kati yake na viongozi wengine wa Serikali ya Mapinduzi na kujaribu kujenga uhusiano wa karibu zaidi na Nyerere.

Siku za Awali za Jamhuri ya Watu wa Zanzibar

Juu ya njama zilizokuwa zikifanyika nyuma ya migongo yao, njama ambazo tayari walikuwa na shaka kuwa zilikuwepo lakini hawakuwa na habari kamili, na ukweli kuwa walikuwa na wanachama wao wachache tu ndani ya serikali, Chama cha Umma Party kilifanikiwa kuleta mabadiliko kadha ya kimaendeleo hapo Zanzibar mnamo siku za awali za Jamhuri ya Watu wa Zanzibar. La muhimu zaidi lilikuwa ni mkakati mpya wa kiuchumi ambao ulikuwa ni muhimu sana kwa mustakbal waliouandaa kwa ajili ya Zanzibar. Kwa hilo, Babu alipanga na kuanza kuandaa mfumo wa kuzitumia bidhaa za kusafirisha nchi za nje ili kuleta mabadiliko ya mfumo wa kiuchumi na kuendeleza soko la ndani. Tutaiangalia mipango hii katika sehemu ya mwisho ya sura hii.

Che Guevara na Babu, wakipumzika baada ya Mkutano wa Kwanza wa Maendeleo ya Kibiashara wa Umoja wa Mataifa (UNCTAD), Geneva, Julai 1964. (Mpiga picha hajulikani)
Che Guevara na Babu, wakipumzika baada ya Mkutano wa Kwanza wa Maendeleo ya Kibiashara wa Umoja wa Mataifa (UNCTAD), Geneva, Julai 1964. (Mpiga picha hajulikani)

Wakati huo huo sera mpya ya mambo ya nje iliandaliwa ikisisitiza uhusiano wa kidugu na nchi za kisoshalisti na kuwa na hadhari kubwa kuhusiana na mtazamo wa nchi juu ya kambi ya wabeberu. Ujumbe wa Zanzibar ulichukua jukumu la kuongoza kampeni ya kuiunga mkono Cuba katika Mkutano wa kwanza wa Biashara na Maendeleo wa Umoja wa Mataifa uliofanyika Geneva mwezi Februari 1964 na ulihusika sana katika uundwaji wa ‘Kundi la 77’.[1] ilikuwa katika mkutano huu ndipo yalipoanzishwa kwa mara ya kwanza mahusiano na Che Guevara na viongozi wengine wa Cuba. Mahusiano hayo yalikuwa ndiyo mwanzo wa mahusiano ya kudumu ya muda mrefu kati ya Zanzibar na Cuba.

Yalikuwepo vile vile mabadiliko muhimu ndani ya nchi ambayo yalikuwa ni pamoja na kuundwa upya kwa jeshi la polisi kwa kushirikiana na serikali ya Tanganyika, kuanzishwa kwa Jeshi la Ukombozi la Wananchi na kuondoa marupurupu yote yaliyoigharimu serikali ‘bila ya kujali cheo cha mtu yeyote hata angelikuwa mkubwa namna gani na hata Karume, Rais alikuwa akiendesha gari lake yeye mwenyewe, bila ya kuwa na msafara wa magari mengine, bila ya bendera au mbwembwe za aina yoyote ya msafara ambazo ni mashuhuri katika nchi zinazotawaliwa na ukoloni mambo leo’ (Babu, 1991).

Hata hivyo, hali hii haikudumu kwa muda mrefu. Wasiwasi uliokuwemo ndani ya chama cha ASP kati ya watu kama Othman Shariff na Karume ulizidi na Karume alianza kujichimbia mizizi na kujiimarisha katika nafasi yake kwa msaada wa kikundi kidogo cha ndani ya chama cha wafuasi wa siasa za mrengo wa kulia kilichoitwa Kamati ya Watu Kumi na Nne. Hali hii iliathiri pia uhusiano kati ya ASP na Chama cha Umma Party, ijapokuwa makada wa Chama cha Umma, hasa Babu, walijaribu kuingilia kati ili kuzuia kuongezeka kwa migogoro ndani ya ASP.

Katika hali hiyo, makada wa Chama cha Umma Party walijikuta wakizuiliwa kutekeleza sera zao. Kwa mfano, Khamis aliniambia kuwa:

Shirikisho letu la vyama vya wafanyakazi, FRTU liliiomba serikali kuongeza kima cha chini cha mshahara kutoka shilingi 15 hadi shilingi 20 kwa siku, kiwango ambacho kilikuwa ni afadhali kwa wakati ule. Rais Karume aliniita mimi nikiwa katibu mkuu wa Shirikisho hilo na Mohamed Mfaume akiwa Mwenyekiti wa FRTU na kutupa onyo kali akitutaka kwa hasira kutangaza mbele ya Baraza la Mapinduzi kuwa hatuna imani na serikali. (Tulijua kuwa kama tungelifanya hivyo angelilitumilia hilo dhidi yetu.) Wenzetu wengine walitushauri tukamwone Ikulu wakati wa usiku na kumfahamisha tena kuwa ongezeko la kima cha chini litalijenga Baraza la Mapinduzi na kutoa mvuto zaidi wa kuungwa mkono na wafanyakazi. Tulimkuta Karume akiwa katika hali ya furaha. Alitwambia kuwa yeye alikuwa akiongoza serikali ya wafanyakazi na mambo mengi mazuri yatakuja. Lakini mishahara haikuongezwa na huo ulikuwa ndiyo mwanzo wa kusambaratishwa kwa vyama vya wafanyakazi Zanzibar. (Mahojiano na Khamis Ameir, 2009)

Karume alivipiga marufuku kabisa vyama vya wafanyakazi, Jumuiya za Vijana na Wanawake mwezi Mei 1965. Khamis alitaka kujiuzulu kutoka katika Baraza la Mapinduzi lakini Saleh Sadalla alimshauri asifanye hivyo.

Ilipofika mwezi Machi 1964, Karume alikuwa karibu zaidi na Marekani, ijapokuwa Zanzibar ilikuwa vile vile ikipata msaada kutoka China, Umoja wa Kisovieti na Ujerumani ya Mashariki (nchi ambayo Karume mwenyewe binafsi aliipenda sana). Uhusiano wake na Marekani unaonekana katika tukio jengine kama inavyoelezwa na Khamis.

Tulipotoa tamko kwa niaba ya Shirikisho la Kimapinduzi la Vyama vya Wafanyakazi (FRTU) kupinga ubeberu wa Kimarekani nchini Vietnam, balozi mdogo wa Marekani Petterson alikwenda kwa Karume na kumtishia. Alimwambia kuwa serikali ya Marekani inataka kuisaidia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar lakini vyama vyetu vya wafanyakazi vinaishambulia Marekani na kwa hivyo itakuwa shida kupata msaada ikiwa ‘matusi’ kama hayo yataendelea. (Mahojiano na Khamis Ameir, 2009)

Karume alishikwa na hofu na kuwaita tena Khamis na Mfaume na ‘kuwaonya’ kwa hasira. Ni wazi kuwa mtazamo wake ulibadilika sana tokea katikati ya mwezi Januari wakati yeye binafsi alipohusika na kumfukuza balozi mdogo wa Marekani Fredrick Picard kwa kuingilia mambo ya ndani ya Zanzibar.

‘Mkakati wa Kikabila Watekelezwa Kwenye Miili ya Wanawake’

Udhalilishaji wa kijinsia wa wanawake vijana wa Kiarabu, wa Kishirazi na wa Kihindi uliofanywa na wanasiasa wa ASP ulikuwa ni wa kawaida katika miezi iliyofuatia mapinduzi na ulitekelezwa katika mfumo wa ndoa za kulazimishwa kupitia matumizi mabaya ya makusudi ya sheria mpya.

Ukweli kuwa juu ya tafiti mbalimbali za kihistoria zilizofanywa kuhusu mapinduzi na matokeo yake yaliyofuatia, na kuwa wanataaluma wachache sana waliogusia kwa kina juu ya mada hii inaonyesha, labda namna gani mambo yanayowahusu wanawake yalivyoachwa kwa makusudi. Kazi ya Salma Maoulidi si ya kawaida. Yeye anazungumzia juu ya upotoshaji na matumizi mabaya ya Sheria ya Usawa, Upatanishi wa Wananchi wa Zanzibar Na. 6 ya 1964 iliyopitishwa baada ya mapinduzi, akieleza kuwa:

Sheria hii inadai kujaribu kuondoa vipingamizi vya kikabila na kitabaka ‘kwa kuwaruhusu wale wapendanao ambao wamekuwa wakikabiliana na upinzani usiokuwa na msingi kutoka kwa familia zao kuweza kuoana kiserikali bila ya idhini ya walezi halali [… Kusema kweli, ilianzisha] mkakati mkubwa wa kikabila uliotekelezwa kwenye miili ya wanawake…. [na kutumiwa kuwa ni njia ambayo wanaume wazee, wengi wao wakiwa wameshaoa, kuwawinda vigori ‘bikra’ ili kutosheleza njaa yao ya ngono au kulipiza kisasi kwa yaliyopita. Wajumbe wa Baraza la Mapinduzi ndio walioongoza kwa kutoa mfano, wengi wao wakiwaoa kwa nguvu wanawake ambao huko nyuma wasingeliweza kuwapata, hasa wasichana wa Kiarabu na wa Kihindi na baadhi ya wanawake kutoka katika familia mashuhuri za Washirazi. (Maoulidi, 2011)

Katika kpindi chote hiki Nyerere hakujitokeza hadharani na kusema lolote kuhusiana na mada hii. Visiwani Zanzibar, sera hizi bado zikitukuzwa hadharani mpaka hivi karibuni yaani mwezi April 2010 na Hassan Nassor Moyo ambaye alikuwa Mweyekiti wa kwanza wa Umoja wa Vijana wa ASP na baadae waziri wa nchi (Naluyaga, 2010).

Vurugu zilizofuata baada ya mapinduzi zimeacha kovu kubwa. Ukabila ulikuwa ndiyo kitu muhimu katika maisha ya kila siku ya siasa za Zanzibar. Serikalini, katika miezi iliyofuatia mapinduzi, kama Khamis alivyonambia:

Zilikuwepo sera za kikabila katika kila ngazi …Waarabu wengi waliondoka na kwenda Oman au Kenya – wale waliobaki hawakuwa na hali nzuri ya kiuchumi, kwa hivyo usingeliweza kuwanyoshea kidole ukasema kuwa walikuwa wakiwanyonya Waafrika … Mpaka hivi leo unaweza kuuhisi ukabila huo, ijapokuwa umepungua kidogo. Mpaka hivi sasa, hakuna Mwarabu au Muhindi hata mmoja jeshini. Serikalini wapo Wahindi wachache sana. Walijaribu kuufanya utumishi serikalini kuwa ni wa Waafrika pekee na hii ilileta matatizo. Palikuwa na ufisadi na idara za serikali zilijaa watoto wa viongozi ambao hawakuwa na ujuzi na hawakuwa na nidhamu, hawakuwa wakenda kazini kwa wakati. Na utumishi kimsingi uliporomoka. Wahindi wachache matajiri walibaki na wao walikuwa wafuasi wakubwa wa ASP. (Mahojiano na Khamis Ameir, 2009)

Kufa kwa Mfumo wa Sheria

Kama palikuwepo na utata wa kiasilia katika sheria mpya inayoathiri ndoa ambayo ingeliweza kutumiwa vibaya, basi hilo ni kweli vile vile kwa namna nyingi kwa baadhi ya sheria nyengine zilizopitishwa na serikali mpya ambazo zilionyesha mgongano kati ya wanachama wengi wa ASP na wanachama wachache wa Chama cha Umma Party

Nyingi ya sheria hizi ziliandikwa na Thomas Franck, mwanasheria aliyekuwa mshauri wa ASP wakati wa mkutano wa Jumba la Lancaster na aliekuwa karibu na serikali ya kikoloni. Franck mara nyingi amekuwa akifanyakazi kwa kushirikiana na Jumba la Lancaster katika kutengeneza mifumo ya sheria kwa nchi kama Zimbabwe na Sierra Leone na alikuwa mshauri wa sheria wa Kenya, Mauritius na Chad. Nchi hizi ziliibuka kutoka katika ukoloni huku zikizishikilia sheria kandamizi walizozirithi kutoka katika serikali za kikoloni. Alikuwa karibu sana na Marekani kiasi kwamba George Ball alieleza kwa kumsifu katika simu ya upepo ya siri kuwa Franck ‘amekataa kwa mafanikio kuandika sheria na kuingiza Jamhuri ya Watu katika jina la Serikali’ (imenukuliwa na Wilson, 1989: 46)

Sheria mpya za Zanzibar zilionekana kuanzisha serikali ya kidemokrasia iliyoendeshwa kwa misingi ya utawala wa sheria, ikiwa na mahakama iliyo huru na kutangaza kuwa Baraza la Katiba la Watu wa Zanzibar lingeliitishwa ifikapo Januari 1965 kutangaza rasmi Katiba ya Zanzibar. Lakini sheria zilizopitishwa kati ya mwezi Januari 1964 na Machi 1964 hazikuwa za kidemokrasia kabisa. Kwa mfano, Sheria ya Mahakama Kuu, kama alivyoandika Shivji.

Imeanzisha Mahakama Kuu kuwa ndiyo ‘mahakama ya juu kabisa ya kumbukumbu, na ila kama itaelekezwa vyengine na Rais, itakuwa na madaraka yote ya mahakama kama hiyo’……[hii] kusema kweli … imeanzisha mfumo wa sheria kwa mtindo wa sheria zisizoandikwa. Lakini lilikuwemo jambo moja la pekee. Rais angeliweza kuamua vinginevyo, na baadae …. Mfumo wa sheria ulipunguziwa madaraka yake kwa uamuzi wa Rais. (Shivji, 2008: 59)

Takriban sheria zote zilizopitishwa kati ya Januari 31 na Machi 25 zilithibitisha madaraka kamili ya Rais. Sheria ya Kuweka Kizuizini ilimpa madaraka ya kumfunga jela mtu yeyote kwa muda wowote aliopenda, kama alidhani kuwa mtu huyo anatenda au alikuwa na uwezekano wa kutenda kwa namna ambayo inahatarisha amani na utaratibu mzuri wa usalama wa serikali. Sheria nyengine zilimpa madaraka Rais kuyaamuru majeshi na kuteua mawaziri kama alivyoona inafaa, kufilisi na kuchukua mali ‘kwa maslahi ya taifa’ bila ya fidia kama akidhani kuwa kufanya hivyo hakutomsababishia shida asiyostahili mwenye mali hiyo (Shivji, 2008: 60).

Kufutwa kwa Chama cha Umma Party

Kwa Chama cha Umma, kupitishwa kwa sheria hizi, uzuiaji wa mara kwa mara wa hatua za kuleta maendeleo, tofauti za wazi kati ya uongozi wa ASP na wanachama wa Chama cha Umma waliokuwemo serikalini na kuzidi kwa madaraka ya watu waliokuwa wamemzunguka Karume (kamati ya kinyama na ya kikatili iliyoitwa Kamati ya Watu Kumi na Nne ambayo wajumbe wake walikuwa wanachama wa Umoja wa Vijana wa ASP) zilikuwa ni dalili mbaya. Wanachama wa Chama cha Umma Party walijua kuwa vyama vyengine vyote vya siasa vilipigwa marufuku na kama migogoro ya wazi ingelijitokeza Chama Cha Umma Party nacho kingeliweza kupigwa marufuku vile vile. Walijua pia kuwa kama chama chao kingelipigwa marufuku tena hawakuwa na namna yoyote ya kufanyakazi chini kwa chini.

Katika barua aliyomwandikia Karim Essack mwaka 1982, Babu aliyaeleza zaidi matatizo haya kwa ujumla wake:

Ili kufanyakazi chini kwa chini katika hali ya nchi zetu unahitaji: (a) vituo vikubwa vya sehemu za mijini vinavyoungwa mkono na wananchi, (b) kuungwa mkono na wakulima wengi ambao kwa kiasi fulani wanauamini uongozi wa wafanyakazi na (c) chama kilichokuwa tayari na miundombinu ya mijini na mashambani … kufanyakazi chini kwa chini bila ya kuwa katika mazingira haya … ni kuyafanya mapambano hayo kuwa na jukumu hasi la ‘magenge yenye kutangatanga huku na kule’. (Babu, [1982a] 2002: 278)

Katika hali hii, akiwa ametingwa baina ya machaguo mawili haya magumu, Babu, akiwa si mtu mwenye ‘kuendekeza dunia ya njozi’ ilimbidi afanye uamuzi makini. Chama cha Umma Party kilifutwa tarehe 8 Machi 1964. Hii ilionekana kuwa ndiyo njia pekee kwa wafuasi wa sera za mrengo wa kushoto kuweza kuendelea kufanyakazi na kutekeleza madhumuni yao Zanzibar. Ijapokuwa chama hicho kilifutwa rasmi, wanachama wa Chama cha Umma Party waliendelea kufanyakazi wakiwa ni kundi la kisiasa, lakini siyo chama cha siasa. Ikiwa kwa upande mmoja kufutwa kwa chama hicho kulimpa Karume udhibiti mkubwa zaidi wa kiserikali juu ya wanachama hao, kwa upande mwengine kuliwapa vile vile wale waliokuwa wanachama wa chama cha Umma Party nafasi kubwa ya kufanya shughuli ndani ya vyama vya wafanyakazi na jumuiya nyengine za wananchi ambazo zilikuwa hazikupigwa marufuku kwa zaidi ya mwaka mmoja baadae. Chase (1976: 17) anaeleza kuwa kufutwa kwa Chama cha Umma Party vile vile kulikuwa na faida za wazi kwa wafuasi wa siasa za mrengo wa kushoto kwa kuwa kuliwafungulia milango ya kuweza kufanyakazi kwa ushirikiano wa karibu zaidi ‘kati ya wale waliokuwa wanachama wa Chama cha Umma Party na wafuasi wa sera za mrengo wa kushoto wa Chama cha ASP’. Matokeo yake ya muda mrefu hayakulikhalisi kundi la Karume ndani ya ASP na ‘huu ni ukweli ambao Karume aliyekuwa mwerevu aliutambua, kwa hivyo muda mfupi baada ya hilo ‘aliwahimiza’ kwa bidii viongozi wakuu wa Chama cha Umma kuondoka Zanzibar’ (Chase, 1976: 17).

Zanzibar Ambayo Ingelikuwa

Hata katika hali hii ya wasiwasi, wanachama wa Chama cha Umma waliendelea kujaribu kuendeleza ajenda yao waliyokuwa wakiipigania. Mfano mkubwa ulikuwa ni katika medani ya kiuchumi. Katika medani hii, Babu akiwa waziri wa mambo ya nje na biashara alichukua hatua za awali zilizokuwa muhimu sana katika kuitekeleza dira yake ya Zanzibar iliyokuwa huru kiuchumi.

Hoja zake zilikuwa, mosi kuwa Zanzibar ilikuwa na fursa ya kuweza kuachana moja kwa moja na ukoloni, na pili, ni kuwa wakati huo visiwa hivyo vilikuwa na rasilmali nyingi – watu waliokuwa na ujuzi na ustaarabu pamoja na raslimali ya ndani ya nchi. Ikiwa na raslimali hizi muhimu, sekta mbili za uchumi za kuzalisha ‘utajiri mpya’ – kilimo na viwanda- zingeliweza kuhuishwa. Vitu vyengine vyote- shughuli za kibenki, bima, biashara, utalii, huduma za jamii, soko la ndani vilizitegema sekta mbili hizi muhimu.

Katika mipango ya uchumi mpya, Babu alianzisha mahusiano na China – nchi ambayo si kama iliweza kukabiliana na hali ya kutoendelea na unyonyaji wa kibeberu tu bali kwa wakati huo ilikuwa nchi pekee ya dunia ya tatu iliyojenga uchumi ulioimarika bila ya kutegemea raslimali kutoka nje. Katika mahojiano ya 1988 Babu alieleza:

Wachina walitoa ripoti ya kuvutia iliyokuwa na madhumuni ya kuujenga upya uchumi wa Zanzibar. Walitwambia msitaifishe kiholela, shughulikieni mambo makubwa tu. Serikali lazima idhibiti usafirishaji nje wa karafuu na mbata kwasababu hizi ndizo bidhaa kuu za kusafirisha nchi za nje na idhibiti uagizaji wa sukari na mchele kwasababu hayo ndiyo mazao makuu ya kutoka nje. Vyengine waachieni wafanyabiashara binafsi na wafanyabiashara wadogo wadogo. Walituonya kuhusu utaifishaji usiokuwa na msingi. (Baadaye tuliyaona hayo kuwa ni kweli, kwasababu kwa majaribio ya utaifishaji, Tanzania ilijikuta katika janga la kiuchumi.) … Wachina walishauri ujenzi wa uchumi uliofungamana ndani na kujengwa upya hatua kwa hatua ili taratibu kuacha kuwa tegemezi kwa karafuu na mazao mengine ya kilimo na kuzalisha chakula zaidi … walishauri vile vile ujenzi wa viwanda vya hapa nchini. Zanzibar tayari ilikuwa na viwanda vichache vilivyokuwa na tija – kwa mfano tulitengeneza sabuni – sasa tulianza kufikiria kutengeneza vitambaa kwa kutumia pamba kutoka bara. (Imenukuliwa kutoka kwa Wilson, 1989: 59)

Mpango huo ulikuwa uanzwe kutekelezwa haraka. Mnamo wiki za kwanza za mwezi April, Babu alikwenda Indonesia, wakati huo nchi hiyo ikiwa ndiyo mwagizaji mkuu wa karafuu kutoka Zanzibar. Ulikubaliwa mpango wa pande tatu wa biashara na viwanda na serikali ya Indonesia. Kwa mujibu wa mpango huo Zanzibar ingeliipatia Indonesia karafuu za thamani fulani itakayokubaliwa, Indonesia ingeliipatia Ujarumani (Jamhuri ya Kidemokrasi ya Ujarumani) mali ghafi ya thamani hiyo hiyo, na Ujarumani ingeliipatia Zanzibar mitambo ili kuanzisha viwanda mbalimbali – vya vitambaa, nyumba na ujenzi, mafuta ya kupikia, usagishaji, mashine za viwanda na mashine nyengine ili kuendeleza na kuufanya usindikaji wa karafuu uwe wa kisasa. Mabadilishano hayo yalikuwa yawe kwa thamani sawa na bei yenye kulingana na bei ya soko la dunia kwa bidhaa ambazo nchi hizo zingelibadilishana. Kwa namna hii ujuzi uliokuwepo ungelitumiwa na maelfu ya ajira zingelizalishwa na wakati huo huo ikiendelezwa teknolojia ya kisasa na kuisaidia Zanzibar kuwa na kilimo cha kisasa. Hayo yote hayakuwa, kama Babu alivyoandika baadae:

Wakati tukisherehekea habari njema tulizokuwa tuzipeleke nyumbani kuhusu mustakbali wa kimaendeleo ambao tungeliuanzisha – afan aleyk! kama muujiza zilitufikia habari za kuundwa kwa Muungano kati ya Zanzibar na Tanganyika. Tulipofika nyumbani hali ilikuwa kama vile yametokea makupuzi ya serikali; hali ilikuwa ya wasiwasi na takriban kila kitu kilikuwa kimebadilika; palienea hali ya kuwepo kwa hisia za waliowashindi na walioshindwa katika nyuso za kila mmoja. Kwa kifupi kila kitu kilikuwa kinyumenyume na wazi kabisa kutoka kwenye mapinduzi na kuingia katika hali ya kupinga mapinduzi. Haikuwa na maana ya kuzungumza juu ya habari njema kutoka Indonesia kwasababu ilionekana wazi kuwa hapajakuwepo na uwezekano wa mpango huo kuweza kutekelezwa kama ilivyopangwa. Kwanza, kwasababu kuundwa kwa muungano kulitunyang’anya mamlaka yetu ya kujitawala ya kuingia katika makubaliano kama hayo yanayotufunga; pili, vipaumbele vilivyosababishwa na hali hiyo mpya vilikuwa ni tofauti kabisa; na tatu kwasababu watumishi, katika ngazi za kisiasa na kiutawala, waliparaganywa na hawakuweza tena kudhibiti mwendelezo uliokuwa muhimu kwa shughuli kama hiyo. Matumaini yote yalififia; fursa kubwa ya kihistoria ilipotezwa. (Babu, 1994: 31)


  1. Kundi la nchi 77 ndiyo chama kikubwa cha kiserikali cha nchi za Kusini mwa dunia katika Umoja wa Mataifa. Kinaziwezesha nchi za Kusini kuelezea na kuendeleza maslahi yao ya pamoja ya kiuchumi na kuimarisha uwezo wao wa kujadili kwa umoja masuali yote ya kiuchumi ya kimataifa ndani ya mfumo wa Umoja wa Mataifa, na kuendeleza ushirikiano miongoni mwa nchi za kusini kwa ajili ya maendeleo yao.

License

Tishio la Ukombozi Copyright © 2016 by Amrit Wilson. All Rights Reserved.

Share This Book

Feedback/Errata

Comments are closed.