8 Uingiliaji Kati wa Marekani Zanzibar na Bara Hivi Sasa

Tokea mwaka 2003, wakati Benjamin Mkapa alipokuwa Rais, serikali ya Tanzania ilikuwa tayari inahusika sana katika vita dhidi ya ugaidi na kwa amri ya Marekani ikifanya vitendo vya utekaji nyara na ‘urudishaji watu usio wa kawaida’. Tukio moja ambalo limejitokeza na ambalo hivi sasa lipo kwenye Tume ya Afrika ya Haki za Binaadamu na Raia ni lile la Al-Asad, raia wa Yemen aliyekuwa akiishi na kufanyakazi Tanzania tokea mwaka 1985. Alikamatwa nyumbani kwake Dar es Salaam mwezi Desemba 2003, na kusokomezwa ndani ya ndege iliyokuwa ikimsubiri na kupelekwa nchini Djibouti ambako hakuwahi kufika hapo kabla katika maisha yake yote. Huko aliwekwa kizuizini ndani ya gereza la siri na kwa mujibu wa Interights kituo cha kimataifa kinacholinda haki za kisheria za binadamu, alihojiwa na kachero wa Wamarekani na kuteswa. Baadaye alipelekwa kiwanja cha ndege ambako alikutana na ‘kikundi cha warudishaji’ – kundi la watu waliovalia mavazi meusi ambao walimvua nguo na kumshambulia, kabla ya kumfunga minyonyoro na kumfunika kitambaa usoni na kumlazimisha kuingia ndani ya ndege nyengine. Aliwekwa kizuizini katika magereza ya siri ya Shirika la Ujasusi la Marekani nchini Afghanistan na Ulaya ya Mashariki na hatimaye kupelekwa Yemen mwaka 2005. Aliachiwa mwaka 2006, bila ya kufunguliwa mashtaka ya kosa lolote linalohusiana na ugaidi. Kwa mujibu wa Solomon Sacco, wakili wa Interights anayeishughulikia kesi hiyo:

Kesi hii ni ya kwanza inayohusu mtu kurudishwa katika Afrika, kufunguliwa katika Tume ya Afrika, lakini hii si kesi ya aina ya pekee kwani ushahidi unaendelea kujitokeza kuhusiana na tabia ya kimataifa ya kurudisha watu. Kesi hii ni sehemu ya madai yanayozidi kukua ya kutambua na kutoa haki kwa watu walioathiriwa kwa kurudishwa ambayo hayataondoka. Nchi – kama Djibouti – zinazoshirikiana na Marekani katika mipango yake ya kurudisha watu, huku zikikiuka sheria zao wenyewe pamoja na Mkataba wa Afrika kwa mchakato huo, inabidi lazima ziwajibishwe na Tume ya Afrika. (Interights, 2011)

Kesi nyengine ambayo pia inaonyesha kuhusika kwa Tanzania katika kurudisha watu kusiko kwa kawaida ni ile ya Laid Saidi, raia wa Algeria. Ni moja ya kesi nyingi zinazoelezewa katika ripoti ya Shirika la Jamii Iliyo Wazi (Open Society Foundation) (2013). Saidi, raia wa Algeria, alikamatwa mwezi Mei 2003 na polisi wa Tanzania, na baada ya kukaa siku tatu gerezani Dar es Salaam alisafirishwa kwa gari hadi kwenye mpaka na Malawi na kukabidhiwa kwa maafisa wa Malawi waliokuwa wamevaa sare. Alikabiliwa na mateso ya kisaikolojia na kudhalilishwa kabla ya kusafirishwa na kupelekwa Afghanistan katika hali ya kutisha. Akiwa Afghanistan alizuiliwa katika magereza matatu ya Shirika la Kijasusi la Marekani pamoja na lile ovu maarufu ‘Gereza la Kiza’ na lile la ‘Shimo la Chumvi’. Kiasi cha mwaka mmoja baadae, alisafirishwa kwa ndege hadi Tunisia ambako aliwekwa kizuizini kwa siku 75 nyengine kabla ya kurudishwa Algeria ambako aliachiwa huru.

Tokea Kikwete aingie madarakani mwezi Desemba 2005, Tanzania imekuwa ni mshiriki mwenye hamasa kubwa zaidi katika ‘vita dhidi ya ugaidi’. Alifafanua msimamo wake katika mkutano wake na balozi wa Marekani Retzer mwezi Mei 2006:

Kikwete, Rais wa Tanzania ameweka wazi kuwa si kama anataka ushirikiano wa hivi sasa juu ya kupambana na ugaidi uendelee tu bali anataka ushirikiano huo upanuliwe zaidi. Ameainisha hasa katika maeneo ya mafunzo na msaada wa kitaalam kutoka katika Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI), Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya Marekani, Wizara ya Fedha, Wizara ya Sheria na mashirika mengine na kusema kuwa anataka kuzipanua program kama hizo. Kabla ya ziara ya Rais Kikwete ya 17-18 Mei, tuliitaka Washington kuandaa mapendekezo yenye kulingana na maslahi ya Rais Kikwete. (Ubalozi wa Marekani, 2006c)

Wakati ambao Kikwete yupo madarakani, mchango wa Afrika Mashariki katika mtandao wa kimataifa wa ’vita vya Marekani dhidi ya ugaidi’ kama inavyobainisha kesi ya Al-Asad, umezidi kushika kasi na miundombinu ya kusimamia kazi ya kupambana na ugaidi ambayo kwa kiwango kikubwa inagharamiwa na nchi za Afrika ya Mashariki zenyewe imeshamirishwa zaidi. Kituo cha Taifa cha Kupambana na Ugaidi cha Yemen kinachukuliwa na Marekani kuwa ndiyo mfano bora katika kazi hii.[1]

Kwa mfano, balozi wa Marekani Mark Green mwezi Februari 2008 aliandika katika ‘maelezo mapya kuhusu suala la ugaidi Tanzania.

Kuanzishwa kwa Kituo cha Taifa cha Kupambana na Ugaidi Tanzania ni suala la kipaumbele kwa Tanzania … Hata hivyo, mipango na muda wa kiutekelezaji wa kituo hicho vinaendelea taratibu sana kwasababu ya ukosefu wa fedha. Ili kuongeza uelewa wa Serikali ya Tanzania juu ya faida za Kituo cha Kitaifa cha Kupambana na Ugaidi, mwezi Oktoba 2007 Ofisi ya Mratibu wa Vita dhidi ya Ugaidi ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, 2001-09) iligharamia safari ya afisa mmoja wa [Idara ya Usalama wa Taifa ya Tanzania] kitengo cha kupambana na ugaidi na afisa mmoja wa Kitengo cha Kupambana na Ugaidi cha Jeshi la Polisi la Taifa ili kukitembelea Kituo cha Taifa cha Kupambana na Ugaidi cha Yemen mjini Sanaa. Kutokana na ziara hii, maafisa wote wawili wametambua juu ya ulazima wa kukikamilisha Kituo cha Taifa cha Kupambana na Ugaidi cha Tanzania, na kuajiri watumishi wake kikamilifu. Hata hivyo, uhaba wa fedha bado umebakia kuwa ni kizingiti. (Ubalozi wa Marekani, 2008c)

Ilipofika mwezi Juni 2009, Marekani ilifurahishwa zaidi na kupiga kifua kwa Tanzania juu ya ‘vita dhidi ya ugaidi’. Kama alivyoripoti Balozi Retzer katika ‘matayarisho ya ziara ya Naibu Waziri Lew nchini Tanzania’:

[Wakati mkakati wa kipaumbele wa kwanza wa Marekani nchini Tanzania ni] kujenga uwezo wa Serikali ya Tanzania wa kupambana na ugaidi na kuendeleza usalama … Serikali ya Tanzania imekuwa ikifanya juhudi za dhati katika kuanzisha kituo chake cha kupambana na ugaidi. Tarehe 4 Disemba mpango wa msaada wa kupambana na ugaidi wa [ Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani] ulizindua warsha ya wiki tatu Dar es Salaam ili kufanya majadiliano ya kina na viongozi wa Tanzania juu ya namna ya kuanzisha na kukipatia vifaa kitengo kama hicho. Ulikuwepo ushiriki wa kikamilifu wa serikali ya Tanzania wakiwemo washiriki kutoka polisi, jeshi, uhamiaji, usalama wa taifa, forodha na benki. Kwa mujibu wa wakufunzi wa Mpango wa Msaada wa Kupambana na Ugaidi walioendesha warsha kama hiyo huko Senegal, Kenya na Chad, maafisa wa Tanzania wameonyesha kwamba ‘wameshaumiliki’ mpango huo kikamilifu na kuwa wapo tayari na wana nia ya kuingia katika juhudi za utekelezaji wake. (Ubalozi wa Marekani, 2009a)

 Udhalilishaji wa Waislamu katika Afrika ya Mashariki unazidi na unahalalishwa kwa kizingizio cha kupambana na ugaidi, huku maafisa wa Marekani wakidai kuwa watu wanaohusika wanahusiana na uripuaji kwa mabomu wa balozi za Marekani mjini Dar es Salaam na Nairobi mwaka 1982.[2] Wakati huo huo kumekuwa na habari za marejeo kadha kuhusiana na mahusiano baina ya watu wa ‘mwambao wa Waswahili’ na mahusiano baina ya watu wa Zanzibar, kupitia Mombasa hadi Somalia. Mahusiano haya kwa sehemu kubwa ni dhaifu, lakini yaliyotokea Somalia yanaweza kuwa ni funzo kwa watu wa Visiwani, hasa katika mukhtadha wa kuwepo uwezekano wa kupatikana mafuta Zanzibar. Huko Somalia pia, mapema katika miaka ya 1990, walichokuwa wakikitafuta Marekani ni mafuta. Takriban thuluthi mbili ya mafuta ya Somalia yaliwekwa kwa ajili ya makampuni makubwa ya mafuta ya Marekani ya Conoco, Amoco, Chevron na Phillips katika kipindi cha kabla ya kupinduliwa rais aliyekuwa kibaraka wa Marekani Mohamed Siad Barre. Ni uwekezaji huu na wala siyo haki za binadamu ambao ndio Marekani waliokuwa wakijaribu kuulinda kwa kisingizio cha ‘uingiliaji kati wa kibinaadamu’ wakati ilipoivamia Somalia mwezi Desemba 1992. Kama alivyotabiri Babu wakati huo, kuwa uvamizi wa Marekani ulikuwa ‘ukitafuta kisingizio cha sheria za kimataifa ili kuiwezesha, siku za mbele, kuingilia kati katika nchi yoyote ile ya Dunia ya Tatu bila ya kushutumiwa … huku ikijificha chini ya maneno (yenye kutilia mkazo) ubinadamu na haki za binadamu’ (Babu, [1993] 2002).

Uvamizi wa Somalia, takriban mwaka mmoja kamili baada ya kuporomoka kwa Umoja wa Kisovieti ulikuwa ni mwanzo wa kipindi kipya ambacho kwa kumalizika kwa vita baridi, Marekani ambayo ghafla iliondokewa na adui, ilianza kutafuta na kumlenga adui mwengine – ugaidi wa Kiislamu. Kwa kulingana na hilo ndipo yalipokuja mahubiri kama yale yaliyoanzishwa na Samuel Huntington, aliyeigawa dunia katika utamaduni wa aina nane: Wa Kimagharibi, wa Kikonfuchi, wa Kijapani, wa Kiislamu, wa Kislavu-Orthodox, wa Marekani ya Kusini na labda wa Kiafrika’ (‘labda’ kwasababu hakuwa na hakika kama Waafrika walikuwa na utamaduni) na alidai kuwa ni utamaduni, siyo siasa au uchumi ndio utakaoigawa dunia. Hii ni kwasababu ‘ni wa nchi za magharibi tu ndio wenye kuthamini “ubinafsi, uliberali, utawala wa kikatiba, haki za binadamu, usawa, uhuru, utawala wa sheria, demokrasia, masoko huria”. Kwa hivyo, nchi za magharibi (kusema kweli Marekani) lazima ziwe tayari kuvishughulikia kijeshi vitisho vinavyotokana na staarabu hizi pinzani (Ali, 2002: 299).[3]

Hivi sasa makampuni ya mafuta kwa mara nyengine tena yanatafuta mafuta yenye utajiri mkubwa kwa mfano katika bonde la Dharoor na Bonde la Nugaal wakati vikosi kutoka Marekani, Uingereza, Uhabeshi na ‘walinda amani’ wengine wakiwa katika hali ya utayari wa kuchukua hatua. Nje ya ufukwe wa Somalia, kama walivyoandika Suzanne Dershowitz na James Paul:

Msururu wa manowari zenye nguvu [tokea mwaka 2008] umekuwa ukifanya doria baharini … Zaidi ya mataifa thalathini yamepeleka meli za kivita – pamoja na manowari za kubebea ndege za kivita, manowari za kusindikiza, manowari za ulinzi na vyombo vyengine vyenye silaha nzito – pamoja na ndege nyengine za kisasa kabisa za kijeshi. Kwa maelezo rasmi, vikosi hivi vya baharini vinatoa ulinzi baharini dhidi ya maharamia – Wasomali walio ndani ya mashua ndogo waliozikamata meli za kibiashara na watumishi wao ili kupata fidia kabla ya kuwakomboa mateka wao. Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mara kwa mara limekuwa likiidhinisha harakati za kijeshi baharini huku likitoa tahadhari ya vitisho vya maharamia kutishia kuwepo njia salama kwa meli za kimataifa na ‘vitisho vyao dhidi ya amani ya dunia na usalama katika kanda hiyo. (Dershowitz na Paul, 2012:14)[4]

Jukumu la Kijeshi la Marekani Nchini Tanzania

Bila shaka Tanzania ni tofauti na Somalia. Ni nchi iliyo maarufu kwa ‘utulivu’ wake. Kwa nini tena kuwepo askari jeshi wengi wa Kimarekani katika kila sehemu ya nchi? Nini jukumu lao na ni nani anaewapa ruhusa ya kuwasili na kuondoka? Nyaraka za siri zilizofichuliwa na WikiLeaks zinatudokeza habari za kuvutia.

Kwa mfano, maelezo ya matayarisho ya ziara ya naibu waziri wa nchi za nje Lacob Lew nchini Tanzania yaliyotolewa na ubalozi wa Marekani mwezi Juni 2009 yanaeleza kuwa:

Mwezi Desemba 2006, Serikali ya Tanzania ilitoa idhini ya … kuwepo kwa Kikosi Kazi cha Pamoja Pembe ya Afrika, kuanzisha kuwepo kwa Kikosi cha Shughuli za Kiraia katika mwambao wa Uswahilini. Kikundi cha Shughuli za Kiraia (ambacho tumekipa jina la Kikosi cha Pamoja cha Afrika na Marekani – AFRICOM) kinaendesha miradi ya kibinadamu na kusaidia kujenga uwezo wa shughuli za kiraia na kijeshi katika Jeshi la Wananchi la Tanzania. (Ubalozi wa Marekani, 2009a)

Ikiwa lugha inaufanya ujumbe huu usieleweke, ufafanuzi wa kina unapatikana katika mtandao wa wanadhimu wa pamoja wa jeshi la Marekani. Shughuli za Vikosi vya Kiraia na vya Kijeshi (kama vile ambavyo uwezo wao unavyoongezwa ndani ya jeshi la Tanzania) ni shughuli ambazo mtandao huo unatwambia, pale ambapo jeshi linachukua majukumu ya kiraia ili kuwezesha kufanyika shughuli za kijeshi, kuimarisha na kuyafikia madhumuni ya Marekani. Zinaweza kufanyika katika maeneo ya shughuli yaliyo rafiki, yasiyopendelea upande wowote au hata ya kiadui na kuzihusisha kazi za kijeshi ili ‘kuanzisha, kuendeleza, kushawishi au kuyatumia mahusiano’ na serikali, vyama visivyo vya serikali, mamlaka za wenyeji, na raia wa kawaida, na hata wakati mwengine kufanya ‘shughuli na kazi za serikali za mitaa, mikoa na taifa. Shughuli hizi zinaweza kufanyika kabla ya, wakati wa au baada ya hatua nyengine za kijeshi (wanadhimu wa pamoja wa Jeshi la Marekani, 2008). Madhumuni ya kuanzishwa kwa Shughuli za Kiraia na Kijeshi ndani ya jeshi laTanzania ni kwa ajili ya kulitumia jeshi la Tanzania, serikali na Vyama Visivyo Vya Serikali kurahisisha kufanyika kwa shughuli za kijeshi zinazoendeleza maslahi ya Marekani, na kuchukua kazi na shughuli za serikali ya Tanzania pale na wakati serikali ya Marekani itakapohitaji kufanya hivyo.

Kama ufafanuzi wa Shughuli za Kiraia na za Kijeshi unavyozidi kueleza, ‘katika ngazi ya kimkakati, kiuendeshaji na kimbinu na katika shughuli zote za uendeshaji za kijeshi, shughuli za kijeshi uraiani kimsingi ni vyombo vya kuoanisha vyombo vya kijeshi na visivyokuwa vya kijeshi vyenye uwezo wa kitaifa.’ ‘Changamoto zinazoweza kuwepo ambazo Shughuli za Kijeshi na Kiraia itaweza kuzishughulikia vile vile ni muhimu sana. Changamoto hizi sio tu na zinahusisha ‘migogoro ya kikabila na kidini, tofauti za kiutamaduni na kijamii-uchumi, ugaidi, uasi wa kijeshi, na kusambaa kwa silaha za maangamizi’ bali pia ‘na ushindani unaokua na unyonyaji wa rasilimali zinazopungua.

Kwa maneno mengine, kama ilivyokuwa ‘madhara yanayoambatana na mashambulizi ya mabomu hayo’ ni neno mbadala la upole kwa vifo vya raia, Shughuli za Kiraia na Kijeshi ni neno mbadala la upole kwa shughuli mbalimbali zisizopendeza na za haramu. Shughuli hizo ni pamoja na vitendo kama vile vya upelelezi, utekaji nyara, kurudisha watu, utesaji, kuwepo vituo vya ndege zisizokuwa na rubani na misaada kwa hatua za kijeshi ili kupata rasilimali ambazo Marekani inazitaka kutoka Afrika. Kwa mukhtadha wa ‘rasilimali zinazopungua’ za Afrika ya Mashariki basi ni pamoja na mafuta na gesi. ‘Kuyafikia malengo ya uendeshaji’ ya Marekani ili kuyadhibiti mafuta ni jambo ambalo si kama linalohalalishwa tu bali ni wajibu wa jeshi la Marekani.

Kusema kweli, katika mijadala ya taaluma ya kijeshi, upatikanaji wa mafuta unachukuliwa kuwa ni sawa kwa hali ya sasa na kile kilichokuwa kikijulikana kama ‘mzigo wa mtu mweupe’ wakati wa ukoloni. Kwa maneno mengine, ni wajibu wa jeshi la Marekani, kuwashughulikia Waafrika, hata kama kazi hii haiwapendezi kwa kiasi gani, na kuleta ‘utulivu’ katika nchi zao ili kupata rasilimali inayopungua ya mafuta. Bila shaka, msimamo unaopindukia ule wa kikabila uliomo katika makala ya aliyekuwa Amirijeshi wa Kikosi cha Ulinzi wa Baharini cha Marekani ambaye sasa yupo katika chuo cha kijeshi cha vikosi vyote vya Marekani, yenye kichwa cha habari cha kupendeza cha Chuo cha Mapigano ya Kijeshi ya Kisasa:

Wengi, au wengi sana wa wazalishaji wakubwa wa mafuta wa Afrika – Nigeria, Angola, Kamerun, Gabon na Ginekweta – ni makaro ya ufisadi, umasikini na ufakiri uliokithiri. Lakini ili kuhakikisha upatikanaji wa kudumu wa nishati, masoko ya dunia yanazihitaji nchi hizi ziwe na utulivu wa kiasi fulani. (Coleman, 2009: 19)

Jumuiya ya Afrika ya Mashariki na Vita Dhidi ya Ugaidi

Orodha ya nchi iliyotolewa na Coleman siyo ya hivi sasa kwa kuwa kwa kipindi cha miaka michache iliyopita imebainika wazi kuwa baadhi ya nchi katika Afrika ya Mashariki – Uganda, Kenya na Tanzania vile vile – zina kiasi kikubwa cha mafuta na gesi. Kwa kuelewa hilo, jeshi la Marekani limetengeneza miundo na mikakati kwa ajili ya kuingilia kati, siyo katika nchi moja moja tu bali katika kanda nzima kwa jumla – na nini tena kilicho na manufaa zaidi kwao kuliko kuvitumia ‘vita dhidi ya ugaidi’ ili kuhalalisha na kuimarisha uingiliaji kati wao?

Jumuiya ya Afrika ya Mashariki iliyoundwa mwaka 2000 inatoa fursa ya kuingilia kati kwa ajili ya udhibiti wa Marekani. Kwa juu juu, hili lilikuwa ni jaribio la mwisho la hivi karibuni katika mlolongo wa majaribio ya kuanzisha ushirikiano wa kikanda ambayo yote huko nyuma hayakuwa na mafanikio. Ilipofufuka hapo awali, Jumuiya hiyo ilikuwa inazijumuisha Uganda, Kenya na Tanzania tu. Sasa ina wanachama wapya wawili, Rwanda na Burundi. Kama ilivyokuwa hapo awali, serikali ya Kenya inaonekana kuwa ndiyo yenye nguvu zaidi. Hata hivyo, hiyo haidhuru kwasababu wanachama wengine wakubwa wawili, serikali za Tanzania na Uganda, nazo pia zina shauku moja ya kupeleka mbele maslahi ya Marekani na ya nchi za Ulaya kama ilivyo Kenya. Ni wazi kuwa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki imetoka nje kabisa ya malengo ya Umajumui wa Afrika ambayo mwanzo, wakati wa kufufuliwa kwake iliyaunga mkono. Jukumu lake katika vita dhidi ya ugaidi na kuziwezesha kwake shughuli za Kikosi cha Pamoja cha Afrika na Marekani kumeongezeka kwa haraka sana.

Kwa mfano, mwezi Februari 2008, ripoti ya balozi wa Marekani Mark Green ‘maelezo juu ya masuala ya ugaidi Tanzania’ ilifichua hatua za awali za namna Marekani inavyoitumia Jumuiya ya Afrika ya Mashariki katika vita dhidi ya ugaidi.

Kuna ushirikiano mdogo wa Serikali ya Tanzania na wenziwe katika kanda juu ya masuala ya Kupambana na Ugaidi kwa kupitia Jumuiya ya Afrika ya Mashariki, ambayo sasa inazijumuisha nchi za Kenya, Uganda, Burundi na Rwanda pamoja na Tanzania. Mataifa matano haya yanashirikiana kwa kupitia Programu ya Jumuiya ya Afrika ya Mashariki ya: Mkakati wa Kanda ya Afrika ya Mashariki wa Amani na Usalama … Mwisho wa mwaka 2007 Serikali ya Tanzania ilianzisha uhusiano na Serikali ya Sudan; hata hivyo kiwango cha ushirikiano wa kupambana na Ugaidi hakijulikani. Serikali ya Tanzania imefanyakazi kwa pamoja vile vile na serikali ya Kenya juu ya masuala ya Kupambana na Ugaidi hapo zamani na Tanzania ina nafasi ya kudumu katika ofisi ya Polisi wa Kimataifa iliyopo Nairobi. Zaidi ya hayo, Jeshi la Polisi la Taifa lina mawasiliano mazuri na majirani wao wa kanda wengi na limeshiriki katika programu za kikanda za kupambana na Ugaidi ikiwa ni pamoja na maafisa kutoka nchi za jirani kwa kupitia programu zinazogharamiwa na Serikali ya Marekani katika Chuo cha Kusimamia Sheria za Kimataifa kiliopo Gaborone, Botswana. (Ubalozi wa Marekani, 2008c)

 Ilipofika mwanzo wa mwaka 2010, uhusiano wa Marekani na umoja huu wa kanda uliimarishwa zaidi. Hebu natuyaangalie mawasiliano ya Marekani katika muda wa siku tatu tu za uhai wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki – Tarehe 2,3 na 4 Februari, 2010, na tuone mawasiliano hayo yanafichua nini kuhusu wanasiasa waandamizi wa Afrika ya Mashariki na uhusiano wao mkubwa wa unyenyekevu na Marekani. Katika simu ya kwanza iliyokuwa na kichwa cha habari ‘ Bunge la Afrika ya Mashariki linaweza kuwa ni chombo cha kuyafikia malengo ya Marekani katika kanda hii’ (Ubalozi wa Marekani, 2010a), Balozi Lenhardt aliripoti juu ya mkutano wake na Abdirahim Abdi wa Kenya, aliyekuwa spika wa Bunge la Afrika ya Mashariki, chombo cha Jumuiya ya Afrika ya Mashariki:

Abdi alisema, miswada inayopitishwa na Bunge la Afrika ya Mashariki ina uwezo wa kisheria kwa wanachama wote. Abdi alisema masuala ya mipakani kama vile magendo na usafishaji wa pesa au labda mapambano dhidi ya ugaidi na uhakika wa haki za binadamu, ni maeneo ambayo Bunge la Afrika ya Mashariki linaweza kuwa na jukumu kubwa.

Siku ya pili, Lenhardt aliripoti juu ya mkutano wake na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki, Juma V. Mwapachu – mwanasiasa wa Tanzania aliyeteuliwa na Kikwete kuwa balozi wa hadhi ya juu kabisa na kupewa fursa ya kushika wadhifa huu. Lenhardt aliiarifu Washington kuwa Mwapachu alimwambia kuwa serikali za Afrika ya Mashariki zinashughulikia Mkataba wa Maelewano juu ya ushirikiano wa pamoja wa kijeshi na zitakaribisha mawazo kutoka katika Kikosi cha Pamoja cha Afrika na Marekani, na kuwa ‘wakati serikali za nchi tano za Jumuiya ya Afrika ya Mashariki zina amani wakati huu, historia ya nchi za kanda ya Maziwa Makuu (pamoja na wanachama wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki, Burundi na Rwanda ) imekuwa ni ya machafuko.’ Mwapachu alimwomba msaada Lenhardt ili kuimarisha uhusiano wa kijeshi kati ya Jumuiya ya Afrika ya Mashariki na Jeshi la Pamoja la Afrika na Marekani, ambalo alilielezea kuwa ni ‘kikosi cha kuleta utulivu katika kanda hii’. Lenhardt alisema pia kuwa mara baada ya kusainiwa Mkataba wa Maelewano, Jumuiya ya Afrika ya Mashariki itaweza kushughulikia kuanzishwa kwa uhusiano wa kijeshi na Jeshi la Pamoja la Afrika na Marekani moja kwa moja … Mwapachu angelipenda kuona kuwa kuna ushirikiano zaidi katika maeneo ya kupambana na majeshi ya waasi, ujenzi wa amani na udumishaji amani, kwa kuendesha shughuli za kijeshi baharini na nchi kavu ‘ (Ubalozi wa Marekani, 2010b).

Tarehe 4 Februari, kwa mara nyengine tena Lenhardt amekuwa na habari njema kwa Marekani. Safari hii ni kuhusu Jeshi la Wananchi wa Tanzania ambalo tokea kuteuliwa kwa mkuu mpya wa majeshi ya ulinzi, Jenerali Davis Mwamunyange mwaka 2007 amekuwa ‘akiboresha vifaa vya kijeshi vilivyochakaa vya jeshi hilo na kujihusisha zaidi na masuala ya kikanda na shughuli za kimataifa za kulinda amani na amekuwa karibu na jeshi la Marekani. Kwa mujibu wa Lenhardt, sifa zote zinafaa zimwendee Kikwete, kwasababu:

Wakati Jenerali Mwamunyange akiwa ndiye aliyesimamia mabadiliko haya, itakuwa ni kosa kusema kuwa mabadiliko haya yanatokana na yeye peke yake. Mhamo huu wa kifalsafa ulianza miaka miwili kabla Jakaya Kikwete kuwa Rais wa Tanzania … mnamo siku kumi tokea Jenerali Mwamunyange kuwa kiongozi wa jeshi, mahusiano ya kijeshi kati ya Marekani na Tanzania yalibadilika sana … Katika kipindi cha miezi 18 iliyofuatia ziara za shughuli za kikazi za viongozi waandamizi wa jeshi la Marekani kutoka kwenye Jeshi la Pamoja la Afrika na Marekani, Vikosi vya Jeshi la Wanamaji katika Afrika, Jeshi la Marekani katika Afrika, Vikosi vya Baharini katika Afrika na hasa Kikosi Kazi cha Pamoja katika Pembe ya Afrika, zimesaidia katika kuimarisha zaidi uhusiano kati ya pande mbili. (Ubalozi wa Marekani, 2010c)

Ujenzi wa ‘Vyanzo’ na ‘Nyenzo’

Katika kipindi cha vita baridi, shughuli nyingi za siri za Marekani zilikuwa ni za matumizi ya ‘vitendo vya mauaji ya moja kwa moja’. Vitendo kama hivi vimeimarishwa zaidi ili vitumike katika vita dhidi ya ugaidi, hasa wakati wa utawala wa Obama. Kama lilivyoandika gazeti la The Nation mwezi Juni 2010, vikosi maalum vinavyofanyakazi kwa ajili ya Kikosi cha Pamoja cha Shughuli Maalum vimewekwa wakati wa utawala wa Obama nchini ‘Iran, Jojia, Ukraine, Bolivia, Paraguay, Ecuador, Peru, Yemen, Pakistani na Filipino … nchi za mstari wa mbele kwa vikosi hivi, hivi sasa, kama vyanzo husika vinavyoeleza, ni Yemen na Somalia’ (Scahill, 2010).

Kwa mujibu wa gazeti la Washington Post (kama lilivyonukuliwa na Scahill):

Uwezo wa shughuli maalum ulioombwa na Ikulu ya Marekani umepindukia kiwango cha mashambulizi yanayoweza kufanywa na upande mmoja peke yake na unajumuisha pamoja na hatua za kutoa mafunzo kwa vikosi vya kupambana na ugaidi vya wenyeji na kuendesha nao shughuli za pamoja. Kuna mipango ya kufanya mashambulizi ya kuwahi au ya kulipiza kisasi katika sehemu mbalimbali za dunia. Mashambulizi haya yanakusudiwa kufanyika pale ambapo utagundulika mpango wa kigaidi, au baada ya shambulio linalohusishwa na kundi maalum.

Shughuli hizi za kijeshi, kama zile za wakati wa vita baridi, zinahitaji mitandao ya makachero na namna nyengine kama hizo za ujasusi katika eneo husika. Charles R. Stith, balozi wa Marekani nchini Tanzania kutoka mwaka 1998 hadi 2001, alitilia mkazo umuhimu wa mitandao na vyanzo kama hivyo.

Uwezo wetu wa kuwanasa magaidi katika uripuaji wa mabomu Dar uliongezeka kwa kiasi kikubwa kutokana na uratibu na ushirikiano wa idara za ujasusi za Tanzania na Afrika ya Kusini. Mapambano dhidi ya ugaidi Barani Afrika yanaweza kuendelezwa tu kwa juhudi kama hizo. Wakati huo huo kuna haja ya kuwepo kwa ukusanyaji na ubadilishanaji wa habari za kijasusi kwa kushirikiana na vyombo vya kimataifa na washiriki wenza wa kitaifa. (Stith, 2010: 64)

Kinachohusishwa na shughuli kama hizo za kijasusi ni ufuatiliaji wa Waislamu wenye kuonyesha ishara za upinzani kwa Marekani. Hii ni shughuli iliyozidi kupamba moto baada ya 9/11, kama alivyoandika Mahmood Mamdani:

Baada ya tamko la kuropokwa tu la kuendesha ‘vita vya msalaba’, Rais Bush alianza kutofautisha kati ya ‘Waislamu wazuri’ na ‘Waislamu wabaya’. Kutokana na mtazamo huu ni wazi kabisa kuwa ‘Waislamu wabaya’ ndio wanaohusika hasa na ugaidi [wakati] … ‘Waislamu wazuri’ watakuwa ni wale wenye hamu ya kusafisha majina yao na fikra za kitendo hiki cha uhalifu mwovu na bila ya shaka watatuunga mkono katika vita dhidi ‘yao’. Lakini hii haikuweza kuuficha ujumbe uliokusudiwa wa mahubiri haya: mpaka hapo atakapothibitishwa kuwa ni ‘mzuri’, kila Mwislamu alichukuliwa kuwa ni ‘mbaya’. (Mamdani, 2004: 15)

Marekani na Uingereza wamezidi kuanzisha programu walizozigharamia pesa nyingi ili kujaribu kuwatengeneza ‘Waislamu wazuri’ kama hao ambao wataziunga mkono nchi za magharibi. Mpango wa Mazungumzo ya Wananchi ni mmoja wa miradi kama hiyo. Kama alivyoeleza Karen Hughes, Naibu Waziri wa Shughuli za Serikali mwaka 2006 mpango huo ulikuwa:

Ni mkakati wa dharura … wa kuwatenga na kuwaweka pembeni magaidi wenye vurugu na wenye siasa kali, kukabiliana na itikadi yao ya ukatili na chuki. Lazima tuzikandamize juhudi zao ili kuonyesha kuwa nchi za magharibi hazikinzani na Uislamu kwa kuziwezesha sauti za watu wote wenye kusikilizwa katika jamii na kuonyesha heshima kwa utamaduni wa Waislamu na michango yao. Ndio maana nimetumia muda mwingi nikijaribu kuwafikia Wamarekani Waislamu. (Hughes, 2006)

Kama simu za WikiLeaks zinavyoonyesha, hata hivyo, namna hiyo ya kuwafikia watu haikuwa ikikubaliwa mara zote. Katika tukio moja, Wamarekani Waislamu ambao walikuwa ni sehemu ya program ya Mazungumzo ya Wananchi waliokuwa katika matembezi ‘kwa mshangao walizuiwa wasiingie msikitini jijini Dar es Salaam.’ Walipojaribu kuingia msikitini kundi la watu lilikusanyika na kuwazuia wasiingie huku wakiwapinga kwasababu walikuwa Wamarekani. Baadaye, wageni hao waliambiwa ‘na viongozi wa waislamu wenye siasa za wastani wa Dar es Salaam kwamba ‘vijana wenye siasa kali’ labda Waislamu wenye siasa kali wanaosaidiwa na Iran, ndio waliohusika na tukio hilo (Ubalozi wa Marekani, 2007c).

Juu ya yote haya, wanadiplomasia wa Kimarekani wanadhani kuwa huko visiwani wamefanikiwa katika eneo hili. Mwezi Juni 2009 katika ‘maandalizi ya ziara ya Jacob Lew’ ulisisitizwa umuhimu wa kupata ‘Baraka’ za wananchi: ‘Kazi yetu Pemba – kisiwa chenye Waislamu wengi na mfano mzuri wa mkakati huu’, ilielezwa. ‘Tumeunganisha shughuli za miradi ya kudumisha utamaduni, kukarabati misikiti ya kihistoria, miradi ya kujitolea ili kuboresha maisha ya watu vijijini na mradi mkubwa wa Shirika la Misaada la Marekani wa kudhibiti malaria na programu za elimu.’ (Ubalozi wa Marekani 2009 a)

‘Vijana Imara’ na Serikali ya Umoja wa Kitaifa

Huko Zanzibar, kama ilivyo mwahali mwengine, kuzidi kwa ubaguzi dhidi ya Waislamu duniani kote, na mashambulizi ya nchi za Magharibi katika nchi zenye Waisilamu wengi, na ukatili wanaofanyiwa Waislamu katika nchi hizi na nchi nyengine kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi, yamechangia katika kuwafanya Waislamu wajitambue. Zaidi ya hayo, hapa pia kuna mbinu zinazotumika kila wakati kuonyesha, hasa kwa ajili ya watalii, kuwa biashara ya utumwa asili yake inahusiana na Uislamu na Waarabu.

Ni utambulisho huu wa Waislamu, hasa miongoni mwa vijana (ndio unaosababisha kuwepo, kwa mujibu wa maneno ya Wamarekani wenyewe ‘vijana wakakamavu wa Kiislamu’), ambao Marekani inawaogopa hivi sasa. Ni kuwepo kwa mchanganyiko wa ‘vijana wakakamavu wa Kiislamu, ukosefu wa ajira na kutoridhika na maisha ambako kwa miaka mingi kumekuwa kukilinganishwa na hali ya ‘kuwa na siasa kali’ na hata ugaidi, ndiko kunakosababisha kuwepo kwa sera za dharura mbalimbali za kidiplomasia na za nchi za nje za Marekani.

Kwa mfano, Michael Retzer, mwanasiasa wa Chama cha Republican na balozi wa Marekani nchini Tanzania aliingiwa na wasiwasi kuhusiana na habari zifuatazo ambazo alizituma kwa simu ya upepo Washington tarehe 24 April, 2006:

Washabiki vijana mia tatu wa Chama cha Wananchi (CUF) walimzunguka kiongozi wa chama chao, Maalim Seif Hamad wakitaka majibu … Wakionyesha kukata kwao tamaa na kutaka jibu kutoka kwa Hamad, vijana hawa waliokasirika waliutaharakisha mchakato wa kutafuta maridhiano uliokuwa ukisuasua Zanzibar pamoja na pengo la uongozi ndani ya Chama cha CUF … Uongozi wa Chama cha CUF una mpango gani? Na iko wapi ahadi ya Rais Kikwete ya kuleta maridhiano? (Ubalozi wa Marekani, 2006b)

Retzer aliendelea kueleza kuwa alifanya uchunguzi zaidi kwa kufanya mikutano ya siri na ‘watazamaji wa kuaminika wa siasa za Zanzibar’ ili kuelewa zaidi juu ya masuala haya. Dk. Rwekaza Mukandala, mkurugenzi wa Asasi Isiyokuwa ya Kiserikali ya Utafiti na Elimu ya Demokrasia Tanzania (REDET) alikuwa ni mmoja wa watu hao. Retzer aliripoti juu ya maoni yake kuwa ‘vijana wa CUF wanakosa uvumilivu na wanatafuta uongozi ‘ ingawa Hamad alikuwa bado akipendwa, hasa Pemba. ‘Kuna Wapemba ambao ni watiifu mno kwa Hamad kiasi kwamba wanadai kuiona sura yake kwenye mwezi!’

Juu ya kuhakikishiwa na Dk. Mukandala kuwa uwezekano wa vijana hao wasioridhika kujitenga na Chama cha CUF ni mdogo, Retzer bado alikuwa na wasiwasi kama alivyoandika katika ripoti yake kuwa ‘kutokuchukuliwa hatua huku na kukosekana kwa mkakati wa kisiasa, pamoja na kuripuka kwa hasira za vijana kunahitaji kuangaliwa kwa makini’. REDET ilimweleza balozi kuwa jibu la matatizo hayo ni kuwepo kwa ‘elimu ya vijana na mafunzo ya uongozi ikiwa ni mkakati wa muda mrefu wa kuandaa viongozi wa baadae’. Mukandala alimwambia kuwa hili ni jambo ambalo Marekani inaweza kusaidia, kwa kukipatia kizazi kijacho cha viongozi wa Zanzibar nyenzo za ujuzi wa kushauriana na wa kushughulikia migogoro. Ni wazi kuwa REDET ilifurahi kushirikishwa katika kutoa kizazi kijacho cha viongozi wa Zanzibar wanaoipendelea Marekani. Retzer aliripoti kuwa alikuwa na nia ya kuandaa programu ya ziara ya kundi la wageni wa kimataifa mwaka unaofuata kwa viongozi vijana wa CUF na CCM.

Kama ilivyofichua WikiLeaks, Marekani ina hamu ya kuwepo kwa serikali ya umoja wa kitaifa ya Tanzania itakayoijumuisha CUF. Hii si kama itawanyanyua viongozi wa sasa tu, kuondoa uwezekano wa kuwa na vijana wenye siasa kali na kuleta ‘utulivu’, bali serikali kama hiyo vile vile itakuwa na fursa ya kuiwezesha Marekani kushirikiana na viongozi na wafuasi wa CUF. Kwa mujibu wa mtoaji habari mwengine, Dk. Ndumbaro kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na rafiki mkubwa wa Dk. Mukandala kwenye REDET, ni rahisi kufanyakazi pamoja na wanachama wa CUF ‘kwani CCM bado inalazimika kutengeneza mazingira mazuri ili sekta binafsi istawi … wafanyabiashara wengi na wachuuzi ni wafuasi wakubwa wa CUF’.

Mambo yalikwenda taratibu katika mukhtadha huu, hata hivyo, baada ya mwaka mmoja, Retzer ambaye alikuwa akizidi kukosa uvumilivu aliendelea kuisukuma CCM kuelekea kwenye maridhiano. Waziri wa mambo ya nje wa Tanzania Bernard Membe alimuhakikishia kuwa CCM, ikiongozwa na Rais Kikwete, ‘inafanyakazi usiku na mchana’ kulitatua suala hili, ijapokuwa bado vipo vikwazo viwili huko mbele: Kamati Kuu ya CCM na kukubali kwa Rais Karume kutekeleza makubaliano yoyote ya usuluhishi yatakayofikiwa’ (Ubalozi wa Marekani, 2007a).[5]

Tarehe 18 Julai 2008, Ubalozi wa Marekani Dar es Salaam ulifanya majumuisho ya sera yake katika waraka ulioitwa Mwongozo wa Zanzibar: suala, kwa nini tunajali na lipi tulifanyalo kuhusu suala hilo’ (2008a). Katika lugha ambayo inafanana na ile ya nyaraka za siri za miaka ya 1960 zilizohusiana na ushawishi wa kikomunisti kutoka Zanzibar kuenea katika bara lote la Afrika, mwongozo huo ulieleza wasiwasi wa Marekani juu ya siasa ya Uisilamu ya Zanzibar ambayo inaweza kuenea katika sehemu nyengine za bara hili:

Mapambano dhidi ya ugaidi: Wazanzibari ni miongoni mwa wanachama wa al-Qaeda waliohusika na shambulio la mwaka 1998 la ubalozi huu. Kuna makundi ya wanaowaunga mkono wenye siasa kali katika kanda yote ya utamaduni wa Mswahili (mwambao wa Kenya na Tanzania, Zanzibar na visiwa vya Komoro vinavyozungumza lugha ya Kiswahili). Kuna uwezekano mkubwa zaidi kwa magaidi kuwaingiza katika ugaidi vijana wa Kiisilamu kutoka Zanzibar kuliko mahali pengine popote katika kanda ya utamaduni wa Mswahili kutokana na kuwepo kundi kubwa la watu wasiokuwa na ajira, waliokata tamaa, wasiokuwa na matumaini, waliokasirika na waliotengwa. Mahusiano ya kifamilia na ya kibiashara katika ulimwengu wa Waswahili ni ya namna ambayo athari za tukio lolote mahali pamoja linaweza kuathiri mahali pengine katika kanda nzima. Kuongezeka kwa imani ya siasa kali Zanzibar kutaiambukiza kanda yote. Kinyume chake, usuluhishi utasababisha kuwepo kwa utawala ulio bora, na kuongezeka kwa neema kutapunguza ushawishi wa itikadi ya siasa kali katika kanda yote. (Ubalozi wa Marekani, 2008a, herufi mlalo ni zangu)

Wakati katika miaka ya 1960 ‘utulivu katika kanda’ (ambao ulikuwa na maana ya mazingira ya salama kwa mtaji wa nchi za Magharibi) ulikuwa upatikane kwa kuiingiza Zanzibar katika Tanzania, na kuimarisha nafasi ya Nyerere, katika miaka ya hivi karibuni inaonyesha ni kwa ajili ya kumuimarisha Kikwete na kuanzishwa kwa serikali ya CUF-CCM Zanzibar ili kuzima ukakamavu wa vijana wa Zanzibar ambao wameainishwa kuwa wanaoweza kuwa magaidi wa Kiisilamu.

Utulivu katika kanda: Rais Kikwete ana takriban miaka mitatu sasa katika kile kinachoonekana uwezekano wa kuwa madarakani kwa kipindi cha miaka kumi. Tanzania imekuwa na mafanikio fulani katika kujiletea mabadiliko na ni mchangiaji mkuu katika kuwepo utulivu katika kanda. Ni muhimu kwa maslahi ya Marekani kuwa kipindi cha urais wa Kikwete kinakuwa na mafanikio na kuwa anaendelea kuheshimu ajenda ya mabadiliko ya kiuchumi na kiutawala. Ametangaza hadharani kuwa kipaumbele chake katika kipindi cha utawala wake ni maelewano ya watu wa Zanzibar. Kushindwa kulifikia lengo hilo kutautia dosari msimamo wa kisiasa wa rais na kuiacha Zanzibar iendelee kuitia doa sifa nzuri ya kimataifa ya Tanzania. (Ubalozi wa Marekani, 2008a, herufi mlalo ni zangu)

Ili kuyatekeleza malengo haya na mengine, ubalozi wa Marekani ulikuwa na jukumu la kuwashajiisha Wazanzibari na serikali ya Muungano kufikia mwafaka wa kisiasa. Na waraka huo unaeleza, Marekani ilikuwa na uwezo wa kufanya hivyo kwa kuwa ‘mipango yake mipana ya misaada kutoka mashirika mbalimbali visiwani Zanzibar … inatuweka katika nafasi nzuri mbele ya watu wa Zanzibar na viongozi wa kisiasa wa kambi zote mbili, huku ikitupa fursa ya kuyazungumzia masuala ya kisiasa ya Zanzibar kama marafiki wa kweli wa watu wa visiwani’.

Wanadiplomasia na Wafadhili Wanajaribu Kucheza Mchezo Mchafu

Hata hivyo, njia ya kuelekea kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa ilikuwa imejaa vikwazo na mambo ya kukatisha tamaa kwa Marekani. Ilipofika mwezi Januari 2009 Ubalozi wa Marekani ulibaini kuwa Kikwete alionekana kubadili mtazamo wake. Katika hotuba yake aliyoitoa kwenye mkutano wa hadhara Zanzibar ‘majigambo yake juu ya uongozi wa Karume katika kuleta maendeleo ya Zanzibar yalikuwa ya kilaghai…. kwa wapinzani waliokuwa wakisikiliza na kusubiri kusikia tamko lolote juu ya mwafaka, kuwaita “walevi” hakukusaidia kitu’ (Ubalozi wa Marekani, 2009d).

Ili kujua maoni ya CUF, maafisa wa Marekani walizungumza na mtu waliokuwa karibu naye. Mshauri wa mambo ya nje wa CUF, Ismail Jussa ambaye alikuwa ni mshiriki wa ‘Programu ya Marekani ya Wageni wa Kimataifa’. Jussa aliwambia watumishi wa ubalozi kuwa Kikwete hivi karibuni amebadili lafdhi yake, akitumia lugha ya kikorombwezo cha vitani cha wale wanamapinduzi waliofanya vitendo vya kikatili vya kuadhibu watu Pemba; kuwa yeye na Seif Hamad ndio ‘watu pekee wenye siasa za wastani’ waliobakia ndani ya Chama cha CUF na heshima yao, baada ya mfululizo wa majaribio yasiyofanikiwa ‘inakaribia kupotea’; na kuwa Juma Duni, Naibu Katibu Mkuu wa CUF ‘ni mtu asiyekubali usuluhishi na ndiye atakayekifanya Chama cha CUF kuchukua msimamo mkali zaidi’. Jussa alisisitiza kuwa panahitaji iwepo tume ya kimataifa ya namna fulani itakayohakikisha kupatikana kwa ushindi wa CUF baada ya uchaguzi ulio huru na wa haki. ‘Baada ya kuchukua madaraka’, Jussa alisema, ‘CUF “itasafisha nyumba” (Ubalozi wa Marekani, 2009e).

Wakati katika awamu zilizopita wanadiplomasia walikuwa wakieleza wasiwasi wao na kuzungumzia mikakati yao na waandishi wa habari wa ngazi za juu kama vile Colin Legum, hivi sasa wanaonekana kuzungumzia mambo yanayowapa wasiwasi na wafadhili. Wikileaks inatupa fununu juu ya mambo yanayowaudhi, wasiwasi wao na tabia ya kuamrisha ya kundi la wanadiplomasia na wafadhili la mtandao mpana na wa ngazi za juu wa Marekani na Ulaya ambao wamehusika na kulazimisha kuwepo kwa uchaguzi wa haki ikiwa ndiyo hatua ya kwanza ya kuelekea kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya visiwa hivi vidogo.[6]

Kwa mfano, mkutano mmoja kama huo (ulizungumzia katika ubalozi wa Marekani, 2009f chini ya kichwa cha habari ‘Zanzibar: wafadhili wataka kuwepo msimamo mmoja juu ya uchaguzi, mwafaka wa kisiasa’), ulihudhuriwa na mabalozi na mabalozi wadogo kutoka Uingereza, Norway, Finland, Ufaransa, Ujerumani, Uholanzi, Canada, Japan, Ubeligiji, Ireland, Italy, Hispania, Uswisi na Tume ya Ulaya, mwakilishi wa Umoja wa Mataifa nchini, wawakilishi kutoka Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa na DFID ya Uingereza; mabalozi wadogo wa kisiasa kutoka Denmark, Norway, Sweden, Uingereza na Canada; na afisa wa ubalozi wa Marekani anayeshughulikia mambo ya Zanzibar. (Inatubidi tushangae kwa nini Zanzibar ni muhimu kwa wawakilishi wote hawa wa nchi za magharibi.) Katika tukio hili, kama alivyoripoti balozi mdogo wa Marekani Mushingi:

Balozi wa Uholanzi aliyekuwa karibu kuondoka Van Kesteren aliwataka wajumbe kucheza ‘mchezo mchafu.’ Wafadhili waandike barua ya pamoja kwa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ikiwa na masharti machache yaliyokubaliwa ambayo itabidi yatekelezwe katika kipindi maalum, yumkini Novemba au Disemba 2009. Kama masharti haya hayakutekelezwa, wafadhili ‘watajitoa’ katika kulipia au kusaidia kufanyika kwa uchaguzi, na kuuita kuwa ni wa udanganyifu … Sweden ilimalizia kwa kusema kuwa ‘Kikwete ndiye mwenye ufunguo wa mabadiliko yoyote mapana au ya msimamo wa visiwani. (Ubalozi wa Marekani, 2009f)

Wiki chache baadae lilitokea jambo kuhusiana na uandikishwaji wa wapiga kura huko Pemba ambalo liliitia wasiwasi Norway. Simu za WikiLeaks zinafichua namna gani tukio hili liliwapelekea wanadiplomasia wajaribu ‘kucheza mchezo mchafu’ na CCM Zanzibar, mchezo ambao matokeo yake hayakuwa mazuri katika nyanja za kidiplomasia. Siku hiyo, wafuasi kadha wa Chama cha CUF wakielekea nyumbani baada ya mgomo wa amani uliofanikiwa dhidi ya uandikishwaji wa wapiga kura, uliotayarishwa na chama chao, walishambuliwa na Kikosi Maalumu cha Polisi, waliopiga risasi hewani kabla ya kuwafurusha na kuwakamata watu wawili na kumpiga mwengine mmoja vibaya sana. Wakifadhaika kuwa hili lingeliweza kusababisha machafuko ya vijana, kuvurugika kwa uchaguzi na kumalizika kwa mategemeo yao ya kuwepo Serikali ya Umoja wa Kitaifa, ‘Marafiki wa kundi la wanadiplomasia na wafadhili la 2010’ walitoa tamko, ambalo likitaka kufuatwa kwa viwango vya kimataifa na mchakato wa kidemokrasia katika mchakato wote wa uchaguzi wa 2010, likitilia mkazo hasa Zanzibar. Hata hivyo, kama ubalozi wa Marekani ulivyoiarifu Washington, Karume alijibu kwa dharau:

Wanadiplomasia waliitwa na kuambiwa kuwa Karume amekataa yale yaliyoelezwa katika taarifa ya pamoja kuwa Serikali ya Muungano inahusika kwa namna yoyote na mchakato wa kuandikisha wapiga kura na kutoa vitambulisho uliokuwa ukiendelea Zanzibar … Karume alieleza kuwa taarifa ya pamoja inatokana na ukosefu wa uelewa wa Marafiki hao. (Ubalozi wa Marekani, 2009g)

Marafiki walirudi nyuma. Kama ubalozi wa Marekani ulivyoieleza Washington, waliamua kuendelea kuichagiza Serikali ya Muungano na Rais Kikwete kudumisha amani na utulivu Zanzibar, na CUF kuepuka kuchukua hatua zisizo za kidemokrasia na vurugu. Na kukubaliana pia kuwa wafanye shughuli zao kwa hadhari ili kuepuka kuonekana kuwa wanafanya mambo yao kwa niaba ya CUF (na hasa kuepuka kuifanya CUF kuona hivyo), kwa kuwa ‘utegemezi wa CUF juu ya maoni ya kimataifa kunaweza kuwa ndiyo tishio la kulaaniwa vitendo vyao wenyewe na hilo kuwa ni nguvu kubwa kwetu’ (Ubalozi wa Marekani, 2009h)).

Katika kipindi cha miaka miwili iliyofuata, mchakato wa kuzisukuma CCM na CUF uliendelea na baada ya heka heka nyingi, uchaguzi ulifanyika kwa amani mwaka 2010 ukiwa wa kiasi fulani kinachoweza kukubalika cha uwazi. Uchaguzi huo hatimaye ulipelekea kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Nini serikali hii itaweza kufanya ni jambo ambalo inabidi kusubiri na kuona lakini kitu kimoja ni cha uhakika: kutokana na matukio yaliyofuatia, Marekani inaweza kuwa bado haifurahii kiwango cha ‘utulivu’uliopo.

Zanzibar na Mustakbal Wake

Kikwete yuko tayari kuihakikishia tena Marekani kuwa yupo moja kwa moja chini ya miguu yao, na kuwa Tanzania, (Bara na Zanzibar) chini ya uongozi wake itayaweka mbele maslahi ya Marekani juu ya maslahi mengine yoyote. Hata hivyo, huko Visiwani mambo kidogo hayaeleweki kuhusiana na hilo, kwasababu ya kuzidi kuwepo hali iliyo dhahiri ya kutoridhika na uhusiano uliopo kati ya Zanzibar na Bara.

Mwezi Septemba 2009, niliweza kufanya mahojiano na Juma Duni, wakati huo akiwa Naibu Katibu Mkuu wa CUF na ambaye mwenzake Ismail Jussa alimwelezea kwa wanadiplomasia wa Marekani kuwa ‘asiyetaka usuluhishi’ na ‘mwenye siasa kali’. Duni, mwenye ustadi wa kujieleza kwa ufasaha mkubwa (ambaye sasa ni waziri wa afya katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa na asiyezungumza sana kuhusu Muungano) aliainisha kutawaliwa na Bara kuwa ndiyo moja ya mambo ambayo yanakipa wasiwasi mkubwa chama chake.

Mwanzoni, baada ya Muungano, tulikuwa na mambo ya Muungano 11 tu sasa yapo 23. Kila muda unavyokwenda, serikali ya Zanzibar inazidi kudhoofu. Kwa mfano, kama waziri wa Jamhuri ya Tanzania atakwenda Marekani na kuzungumza mambo ya kilimo, wanamsikiliza. Kama waziri wa Zanzibar atazungumza kuhusu kilimo wanasema ’Wewe ni nani? Waziri alikuwepo hapa siku chache zilizopita na tulikubaliana naye juu ya misaada na mikopo.’ Misaada na mikopo hiyo haiji hapa [Zanzibar] inakwenda Bara. Kwa hivyo wanaitumia Jamhuri ya Muungano kwa maslahi ya Tanganyika. Wafadhili hushughulika na wao wakiwa Jamhuri ya Muungano. Zanzibar inakuwa kama manispaa. Tunakwenda kwao na kuomba kibali chao badala ya kuwa sehemu sawa ya muungano.

Duni alikuwa na wasiwasi vilevile na masuala ya fedha:

Kabla ya mapinduzi ilikuwepo Bodi ya Sarafu ya Afrika ya Mashariki. Zanzibar ilikuwa mwanachama pamoja na Tanganyika, Uganda na Kenya. Tulikutana tukiwa nchi nne. Kwa kutumia njia za kikatiba na kisheria waliiondoa Zanzibar na kuchukua mali zetu zote. Walizitumia pesa hizo kuanzisha Benki Kuu ya Tanzania. Tungelidhani kuwa Benki Kuu ya Tanzania ni ya Watanzania wote na tungelishughulikiwa kwa usawa wakati wa kwenda kutaka ruzuku au mikopo au misaada ya fedha ya muda mfupi. Lakini haturuhusiwi kwenda kwenye benki hiyo, inatubidi twende kwa Waziri wa Fedha. Inambidi kwanza akubali na halafu aiagize Benki. Kwa hivyo, Benki si yetu … Kwa kipindi cha miaka arobaini iliyopita tumekuwa tukitoa hoja kuwa sisi ni wanahisa, tuna haki kwasababu ya mali mliyoichukua kutoka kwetu … Vile vile wameongeza fedha za kigeni – jambo ambalo hapo awali halikuwa la Muungano. (Mahojiano na Juma Duni, 2009)

Madai ya Zanzibar kutaka kuwa na uhuru zaidi kwa miaka mingi yamekuwa yakipamba moto Visiwani ambako watu wengi wana hasira juu ya kutawaliwa kwao na Bara. Lakini taratibu mjadala miongoni mwa watu umezidi kuongezeka. Baadhi ya wafadhili na serikali zilizolazimisha kuwepo kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa wameeleza kuwa hata wao wanapendelea Zanzibar kuwa na uhuru zaidi. Kwa mfano, katika makala yenye kichwa cha habari ‘ Maelezo juu ya namna ya kutoa msaada wa kimkakati katika kipindi cha mpito kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar’, Taasisi ya Sheria za Kimataifa na Sera, asasi ya sheria isiyokuwa ya kiserikali ambayo ipo karibu na serikali ya Norway, yalieleza kuwa uchumi wa Zanzibar kwa kiasi kikubwa unadhibitiwa na Muungano na kwa miaka 47 Muungano umefanya machache sana kuchochea ukuaji wa uchumi na kuondoa shida za wananchi visiwani (imenukuliwa kutoka kwa Rashid, 2011: 15). Taasisi hiyo inaeleza kwa namna isiyokuwa ya wazi kuwa Zanzibar inaweza kujiendeleza yenyewe. Hapa, ujumbe ni kuwa uhuru zaidi ndiyo suluhisho.

Wakati huo huo, CUF na baadhi ya viongozi wa CCM wamekuwa wakisinikiza kuwa gesi na mafuta viwe chini ya udhibiti wa Zanzibar, na mwezi Oktoba 2012, hatimaye yalifikiwa makubaliano ya muda, yumkini vile vile chini ya shinikizo la makampuni ya mafuta na gesi. Mwezi Oktoba 2012 Zanzibar ilianza mchakato wa kuandaa mipango ya kisheria na kiasasi ya kusimamia mafuta na gesi yake (Bariyo, 2012)

Ikiwa mkataba utaridhiwa na yatapatikana mafuta yatakayokuwa na tija kiuchumi, hili litauathiri vipi mustakabali wa Zanzibar? Je, serikali itaweza kuuepuka mtego ambao umekuwa ni wa kawaida katika mikataba na kampuni za mafuta, kama vile kukataa kwao kulipa chochote isipokuwa sehemu kiduchu ya faida na posho ndogo kwa hasara itakayopatikana pindi ikitokea ajali? Ajali kama hizo zimekuwa ni jambo la kawaida katika Afrika, ajali ambazo husababisha hasara kubwa za kimazingira na kuwang’oa watu katika makazi yao ya kawaida. Kwa mfano Tullow Oil ambayo tayari inafanya shughuli zake Tanzania, ilikuwa na uvujaji mkubwa wa mafuta nchini Ghana mwaka 2009 na 2010 (Platform, 2012); Chevron Texaco ilimwaga mafuta kutoka katika kisima chake kilichopo baharini kaskazini magharibi ya Angola mwezi Juni 2002 na kuchafua mazingira ya fukwe na kuwafanya wavuvi kushindwa kufanyakazi (Habari za BBC, 2002); na Statoil ambayo inatarajiwa kuwa mshiriki mkubwa Bara na Zanzibar hivi karibuni ilimwaga kiasi kikubwa cha mafuta katika mbuga za Urusi (Staalesen, 2012), Shell, ambayo hivi sasa inatafuta mafuta katika bahari inayoizunguka Zanzibar, ni ahasi katika umwagaji wake wa mafuta na yenye kujulikana kwa uchafuzi wa mazingira ya ardhi ya watu wa Ogoni katika bonde la Niger. Ushahidi uliofichuliwa mwaka 2010 pia umeituhumu Shell na kuhusika kwake katika upatikanaji wa fedha na vifaa kwa jeshi la Nigeria na Luteni Kanali Okuntimo [Mnaigeria] ambaye aliwaua wazee wanne wa Ogoni, tukio lililosababisha kuuliwa kwa kiongozi wa watu wa Ogoni Ken Sero-Wiwa (Rowell na Lubbers, 2010).

Kuna swali vile vile la je! Ni nani hasa atakayenufaika nchini Zanzibar. Takriban katika kila nchi yenye utajiri wa mafuta katika Afrika limejitokeza miongoni mwa wanasiasa tabaka la walanguzi mafisadi wenye utajiri mkubwa na ambao wamekuwa wakishirikiana na mashirika makubwa kuzima na kunyamazisha upinzani. Hadi sasa, juu ya kutokuwepo hali ya usawa kwa kiwango cha hali ya juu katika nchi, suala la kurekebisha hali kwa mgawanyo sawa wa rasilmali miongoni mwa watu wa Zanzibar halionekani kuwemo katika ajenda ya CUF wala ya CCM.

Huku ahadi ya gesi na mafuta ikiwa inaning’inia hewani kama mazigazi, mustakabal wa Muungano umekuwa ni mada ya mjadala mkali ndani ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Na ni kwasababu hii ndiyo maana serikali ya Tanzania hatimae imeanzisha jaribio la kutafuta maoni ya wananchi juu ya aina ya Muungano ambao wangelipenda uwepo. Mashauriano haya yatafuatiwa na Mapitio ya Katiba katika kikao cha Bunge cha mwaka 2013. Mwenyekiti wa Tume ya Mapitio ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, mara kwa mara amekuwa akisema kuwa Watanzania wawe huru kutoa maoni yao juu ya Muungano (Mugarula, 2012). Hata hivyo, katika kuonyesha demokrasia katika mtindo wa Zanzibar, makamo wa pili wa rais Seif Ali Idi, mwanachama wa CCM, ametangaza kinagaubaga kuwa ‘Muungano huu upo kwa kudumu’, na waziri mkuu Mizengo Pinda, pia mwanachama wa CCM, ametangaza kuwa ‘Muungano hautavunjika’ (Dodoma, 2012).

Sio kama msimamo rasmi wa viongozi wa CCM wa Zanzibar haukubadilika, haupindiki na ni tofauti kabisa na ule wa CUF tu, chama hicho, vilevile hakiwavumilii wapinzani miongoni mwa wanachama wake. Mansoor Yusuf Himid, mwanachama wa CCM na waziri wa kilimo na utalii, ambaye tarehe 14 Julai 2012 alisema kuwa mfumo wa serikali mbili katika Muungano kati ya Zanzibar na Tanganyika ‘umepitwa na wakati’ na hatokubali suala la gesi na mafuta libakie katika orodha ya mambo ya muungano, alifukuzwa na Rais Shein kuwa mjumbe wa Baraza la Mapinduzi (Yusuf, 2012).

Huku viongozi wa CUF na CCM wakiwa katika malumbano makali baina yao wenyewe kwa wenyewe ndani ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa, madai ya kutaka Zanzibar iwe dola huru yametolewa kwa nguvu kubwa na chama kilichoandikishwa kuwa ni Asasi Isiyokuwa ya Kiserikali, Umoja wa Mpango wa Kuwaandaa Waisilamu, ‘Uamsho’. Umoja huu uliwavutia Wamarekani tokea mwaka 2005 (Ubalozi wa Marekani, 2005a), huku Michael Owen, naibu wa ubalozi wa Marekani na balozi mdogo Dar es Salaam, akiuelezea umoja huo kuwa ‘wenye kelele zaidi miongoni mwa vyama vidogo vya wenye siasa kali Zanzibar … kinachojumuisha mashehe vijana wachache wenye mtazamo wa Kiwahabi wa Saudia … Chama cha CCM kinauona Uamsho kuwa ni kivuli cha chama cha upinzani cha CUF. Owen aliendelea kuelezea ni vipi:

Kiasi cha mwaka mmoja uliopita, wakati mfululizo wa miripuko ilipoutikisa mji mkongwe wa Zanzibar, watumishi kadha wa serikali ya Zanzibar, waliihusisha hadharani Uamsho na Chama cha CUF, na kuwalaumu wote wawili kwa mashambulizi hayo. Wanaharakati kadha kutoka katika Asasi hiyo Isiyokuwa ya Kiserikali na ya siasa walikamatwa, lakini wote baadae waliachiwa bila ya kufunguliwa mashtaka … Tuhuma za serikali dhidi ya Uamsho ni sehemu ya mtindo wa muda mrefu, ambao hutumiwa na CCM kujaribu kuionyesha CUF kuwa ni sehemu ya vurugu zinazofanywa na Waislamu wenye siasa kali. Uamsho yenyewe inaweza kuwa ndiyo inayoipatia serikali ya Zanzibar njia mwafaka ya kumpata yule wa kumwandama kwa misingi ya kuwa na siasa kali. (Ubalozi wa Marekani, 2005a)

Ilipofika 2012 Uamsho haikuwa asasi ndogo tena. Mikutano yake ya hadhara iliwavutia maelfu ya watu na ilikuwa ikichukua msimamo wa kisiasa kwa uwazi kabisa, ikifanya kampeni dhidi ya Muungano na kuulaumu kwa kuifilisi Zanzibar kiuchumi. Vijana wasiokuwa na ajira na wasioona mustakabali wowote mbele yao na wenye kukasirishwa na hali inayoonakana wazi wazi ya kukosekana usawa wanavutiwa na kundi hili kwa wingi. Serikali imejibu hayo kwa kuzidisha ukandamizaji.

Mwishoni mwa mwezi Mei 2012, kanisa kubwa lililokuwepo nje ya mji mkongwe lilivamiwa na kundi la watu wenye hasira na kuunguzwa vibaya. Mara moja lawama ilitupiwa kikundi hiki, juu ya viongozi wake kukanusha vikali kuhusika kwa namna yoyote. Haikutimia hata miezi miwili baadae wakati ilipozama meli iliyokuwa ikisafiri kati ya Dar es Salaam na Zanzibar ambayo ilisababisha vifo vya watu wanaokisiwa kuwa 145 na serikali kulaumiwa kwa kushindwa kwake kusimamia kanuni za usalama, lilitokea tukio jengine kubwa. Waombolezaji ambao baadhi yao walikuwa wafuasi wa Uamsho walikusanyika nje ya msikiti ili kuwaombea dua marehemu na hapo walivamiwa na polisi, wakarushiwa mabomu ya kutoa machozi, kupigwa na kukamatwa (Reuters, 2012).

Mnamo wiki ya mwisho ya mwezi Oktoba 2012, Sheikh Farid Hadi, kiongozi wa kidini wa Uamsho alipotea kwa muda wa siku tatu. Hasira za wafuasi wake zilizagaa barabarani. Kilichofuatia hapo yalikuwa ni mabomu ya kutoa machozi, mapigano ya barabarani na watu zaidi ya mia moja walikamatwa. Polisi walisema kuwa hawakujua lolote kuhusu mahali alipokuwepo, lakini Hadi alipotokea tena, alisema kuwa alifungwa kitambaa machoni, alipelekwa mahali asipopajua na kuhojiwa kuhusu mipango ya baadae ya Uamsho na kuhusu ziara zake za mara kwa mara huko Oman na nchi nyengine za Kiarabu (Zakaria, 2012). Wakati huo huo, Uamsho tayari ilikuwa ikielezwa katika vyombo vya habari, bila ya ushahidi wowote, kuwa ina uhusiano na Somalia au hata na Boko Haram, kundi la Waisilamu linalohusika na vita vikubwa vya kidini nchini Nigeria (Jorgic, 2012).

Kwa hivyo, nini hasa siasa za Uamsho kwa upana wake? Inasema nini kuhusu mafuta, biashara kubwa, umoja wa Visiwani na mgawanyo wa rasilmali? Katika mahojiano kwa njia ya barua pepe mwezi Julai 2012, msemaji mmoja aliniambia kuwa anadhani kuwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ni hatua chanya kwasababu ‘inawezesha kuwepo kwa ushirikiano miongoni mwa Wazanzibari’. Katika vyama viwili vikubwa vya siasa, Chama cha CUF kimekuwa ‘kimya sana baada ya kujiunga na serikali hiyo’ na Chama cha CCM kilikuwa ni chama kinachoporomoka ‘kwasababu hakiwakilishi maslahi ya wananchi wa Zanzibar’. Juu ya suala la mafuta, Uamsho inataka kuwa mashauriano yote ‘yawe ya wazi na yashughulikiwe na Wazanzibari’. Ama kuhusu maendeleo ya baadae ya Zanzibar, asasi hiyo inaiona Brunei kuwa ni ‘ruwaza’ kwasababu, msemaji huyo aliendelea kuniambia, Brunei ni nchi ya amani sana ambayo inayatumia [mafuta na gesi] kwa maendeleo ya wananchi wao.

Nini kilichosababisha kuwepo kwa dira hii kwa mustakbal wa Zanzibar? Kusema kweli, Zanzibar ina mambo machache yanayofanana na Brunei, ambayo ni nchi ya kihafidhina ya Kiislamu inayotawaliwa na mfalme, ambayo Wamalay wa nchi hiyo wanaishi kwa jasho la wafanyakazi wasiokuwa raia. Labda matumaini haya yanaonyesha ukosefu wa taarifa. Labda kuna dhana pia, kwa mbali, kutoka kwa wale wafuasi wa zamani wa siasa za mrengo wa kulia na waumini wa itikadi ya Chama cha ZNP ambayo inawaona wanachama na wafuasi wa Chama cha ASP kuwa ni wa kutoka nje na si Wazanzibari. Kwa namna yoyote ile, kuwepo kwa nguvu za Uamsho hakuwezi kupingika na pia namna ya kuungwa mkono kwake, hasa katika jamii iliyogawanyika kati ya Waarabu na Waafrika na katika mgawanyiko wa kitabaka vilevile.

Wakati kitabu hiki kinakwenda kwa mchapaji, serikali imeishambulia tena asasi ya Uamsho. Sheikh Farid Hadi na viongozi wengine wa asasi hiyo wamekamatwa na wapo gerezani, ambako wamekuwa wakidhalilishwa na kunyimwa haki za msingi za kidini – kwa mfano, wakilazimishwa kunyoa ndevu na kunyimwa fursa ya kusali sala zao za fardhi. Wakati huo huo imeundwa kamati mpya ya watu sita ili kuendeleza mjadala huu. Kwa namna yoyote ile, wajumbe wake wanaunga mkono kuendelezwa kwa kampeni ya kuwa na Zanzibar iliyo huru iliyounganishwa kwa mkataba na Tanganyika iliyo huru (Machira, 2012). Miongoni mwa wajumbe wake wengi ni wale ambao Marekani inawakubali: Ismail Jussa, aliyeshiriki katika Mpango wa Marekani wa Wageni wa Kimataifa, Eddy Riyami, mfanya biashara mashuhuri; Hassan Nassor Moyo (CCM) ambaye mchango wake katika miaka ya 1960 na 1970 nimeueleza katika kurasa za nyuma na aliyekuwa waziri Yusuf Himid.

Ambaye hayumo katika kamati lakini yupo karibu sana na kamati hiyo ni Salim Rashid ambaye hapo awali alikuwa mwanachama wa Chama cha Umma lakini baadae alibadili sana mtazamo wake na kusaidia kutayarisha, miongoni mwa mambo mengine, mpango wa mabadiliko ya kuleta mfumo huria uliofuatwa na Zanzibar mwaka 1984. Maoni ya Rashid juu ya mustakbal wa Zanzibar yamo katika makala ambayo yamekuwa kama ndiyo ilani ya mfumo huria mambo leo kwa ajili ya kamati hii na wanasiasa wengine wanaoshinikiza kuwepo kwa Zanzibar iliyo huru (Rashid, 2011). Katika makala hayo anapendekeza ziwepo fursa za kupata mikopo mikubwa inayolipika na ya riba ndogo kwa sekta binafsi na wataalam kutoka nje ili kuiendeleza Zanzibar kuweza kuwa eneo huru lililojikita hasa katika shughuli za kibenki, biashara kwa makampuni ya nje, bima, teknolojia ya habari na mawasiliano, utalii na shughuli nyengine za kifedha ‘La muhimu’ aliandika, ni kuwa mipango yote ya maendeleo na miradi mengine inatekelezwa kwa mashauriano makubwa na ushiriki mkubwa wa wataalamu mahiri wenye sifa wa kimataifa wenye kuheshimika duniani … waliofanya shughuli za kuzishauri serikali zinazotambulika na kufuatilika tokea huko nyuma (Rashid 2011 : 3). Kwa maneno mengine anazungumzia washauri kutoka katika Shirika la Fedha la Kimataifa, Benki ya Dunia na serikali za nchi za magharibi ambazo zinazishauri nchi zinazopendelea Marekani katika bara lote la Afrika, na ambao Rashid angelipenda kuwaona wakiwa na dhamana ya kuinyonya ardhi ya Zanzibar na watu wake. Rashid alipendekeza kuwa Zanzibar ishirikiane na Norway na Qatar kuhusiana na mafuta na gesi yake. Baada ya kuwashukuru wafadhili wakubwa wote, alimaliza kwa kuutaja hasa, mchango wa Marekani: ‘Marekani ikiwa ndiye mfadhili mkuu wa Zanzibar inaweza kutoa mchango wa kimkakati kwa kushirikiana na wafadhili wengine katika kuubadili uchumi wetu na mtindo wa maisha ya watu wetu’ (Rashid, 2011: 18).

Zanzibar itapata uhuru gani kama itakuwa na utiifu wa kiasi hicho kwa Marekani, ambayo huko nyuma ilihusika chini kwa chini kuleta Muungano? Zanzibar yenye kung’aa, chini ya mfumo huria mambo leo, ikiwa huru au isiwe huru, itautia utajiri mkubwa sana katika mikono ya wanasiasa wachache na walanguzi na kuyafanya maisha kuwa magumu zaidi kwa kila mtu, na hasa kwa wale wanaoishi katika maeneo masikini ya Visiwa hivyo. ‘Vijana wasioridhika na ambao wamekasirika’ walioainishwa na wanadiplomasia wa Kimarekani, ambao idadi yao imezidi kukua na ambao wengi wao sasa wanaiunga mkono asasi ya Uamsho, hawatakuwa wadau katika hali hiyo.

Babu angelifikiri nini juu ya mijadala hii? Mwaka 1994 aliandika juu ya hali ya Muungano na uwezekano wa kuwepo mabadiliko. Naye pia alitaka kuwepo kwa Zanzibar iliyo huru iliyoungana na Bara kwa njia ya mkataba kwasababu, aliendelea kuandika, uhusiano wa hivi sasa ‘umeifanya Bara kujifanya kuwa … mlinzi wa mojawapo ya serikali mbaya sana ya kipinga maendeleo na yenye mtizamo finyu wenye kuangalia nyuma … Iliyozuia maendeleo ya elimu na uchumi ya wananchi’ (Babu, 1994: 32). Alieleza kuwa Muungano umeinyima Zanzibar haki ya kujadiliana na kuingia katika makubaliano ya kiuchumi ambayo yangelikuwa na maslahi kwa Zanzibar pekee na si lazima kwa Bara, na kuiweka Zanzibar ‘chini ya uongozi wa chama cha siasa ambacho dira yake inaishia kwenye mitazamo ya wasiwasi wa kiusalama iliyopotoshwa na isiyoona mbali katika masuala ya maendeleo ya kiuchumi’ (Babu 1994: 32).

Udhibiti wa serikali kuu wa sarafu ya Zanzibar, Babu alieleza, umeinyima Zanzibar haki ya kuwa na sera huru ya fedha na sarafu yenye kufaa kwa mikakati yake yenyewe ya maendeleo. ‘kimbilio lisilokuwa na mpango kwenda kwenye mitambo ya uchapaji ili kuchapa fedha za kulipia upungufu usiokwisha wa Bara, siku zote umekuwa ukiingiza Zanzibar katika mifumko ya bei ambayo haikusababishwa na wao wenyewe na kuipa shida Zanzibar kuweza kuanza mipango yoyote ya kiuchumi na kijamii … Zanzibar lazima iwe na haki ya kujiamulia mambo yake wenyewe, kufanyakazi kwa ajili ya kuleta maslahi yaliyo bora zaidi kwa watu wa Zanzibar’ (Babu, 1994: 32).

Babu alikuwa na dira gani ya maendeleo ya kiuchumi ambayo ingeliyafikia maslahi haya? Mwaka 1996, wakati alipofariki, mafuta yaliyokuwepo Zanzibar hayakuonekana kuwa na tija kiuchumi, kwa hivyo hakuandika kuhusu mchango wa mafuta hayo kwa maendeleo ya Visiwani. Hata hivyo, mtazamo wake kuhusu maendeleo unaonesha kuwa asingelipenda kuona kuwa udhibiti wa mafuta hayo unakabidhiwa kwa ujumla wake kwa makampuni ya kimataifa. Aidha angelisisitiza kuwa sera ya uchimbaji huru wa kitaifa wa gesi na mafuta upo sio Venezuela tu bali pia Bolivia na Argentina. Nchi hizi zimetumia mafuta na gesi kwa kujiletea maendeleo makubwa ya kisiasa na kiuchumi. Nchini Bolivia kwa mfano, katika kipindi cha miaka minne baina ya mwaka 2004 na 2009 hali ya kutokujua kusoma na kuandika iliondoshwa, kiwango cha vifo vya watoto kilipunguzwa kutoka 52.1 hadi 43.4 kwa kila vizazi hai 1,000 na utaratibu wa malipo ya kiinua mgongo ulianzishwa. Ardhi na madaraka yaligawiwa upya kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 500. Mengi ya haya yalilipiwa kwa mapato ya mirabaha kutoka katika mafuta na gesi (Taylor, 2009: tradingeconomics, 2013).

Chapter8_1
Badawi Qullattein, Hashil Seif Hashil na Khamis Ameir Zanzibar, juni 28, 2011 Chanzo: Mailys Chauvin

Dira ya Babu kuhusu Zanzibar ambayo ameiandika na kuijadili katika makala ya majarida mbalimbali (angalia kwa mfano Babu, 1994) ililenga kwa watu wake, ardhi yake na mahali ilipo kimkakati. Siku zote akiwa myakinifu, aliweza kuona kuwa Zanzibar ingelibidi iufufue uchumi wake baada ya uharibifu ulioletwa katika miaka ya Muungano, na kubadili vipaumbele vyake vya kiuchumi na kuvielekeza upya katika kukidhi mahitaji ya wananchi. Alitaka kuwepo kwa uchumi uliopangwa na uliofungamanishwa na mahitaji ya ndani ambao utajumuisha maendeleo ya sekta mbili tu zinazozalisha rasilmali mpya – kilimo na viwanda. Mengine yote – bima, biashara, utalii na kadhalika – ‘vinategemea rasilmali inayozidi kukua kila siku inayozalishwa na sekta mbili hizi muhimu. Yoyote katika hizi ikiwa na matatizo, uchumi wote unakuwa na matatizo kwasababu ndio vigezo vya uchumi halisi.’ Ili kuufufua uchumi huu halisi, Babu aliandika, ilikuwa ni muhimu, kwanza kuijenga upya miundombinu ( Zanzibar haikuwa na bado haina mfumo wa kisasa wa ugavi wa maji, mfumo wa maji machafu au mfumo wa uhakika wa ugavi wa umeme), na sehemu kubwa ya mikopo kutoka nje inabidi ielekezwe kwa ajili ya shughuli hizi. Pili, kilimo, hasa uzalishaji wa chakula, lakini vile vile uzalishaji wa mazao ambayo si ya chakula lazima viwe vya kisasa, siyo kwa kuleta makampuni ya kimataifa kama inavyofanyika Tanzania Bara lakini kwa kuwasaidia wazalishaji wananchi na kuwapa vivutio.

Tatu, viwanda vya ujenzi na ujenzi wa nyumba ama na serikali au watu binafsi kwa ajili ya wananchi lazima vipewe kipaumbele. Hii siyo kama itasababisha kuwepo kwa nyumba za bei nafuu tu lakini pia itasababisha kuanzishwa kwa viwanda vya kuzalisha saruji na chokaa, viwanda vya mbao na useremala, utengenezaji wa nyaya, vifaa vya kuezekea na bidhaa nyengine za viwanda vya kisasa vya ujenzi na tena kuingia pia katika ujenzi wa barabara, reli, mifereji ya umwagiliaji na kadhalika. Utaratibu huu utazalisha pia maelfu ya ajira mpya kila mwaka – utaongeza uwezo wa matumizi ya kifedha wa wananchi na kukuza soko la ndani. Kwa hivyo, uzalishaji utakuwa ni kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya watu wa Zanzibar na siyo kwa ajili ya kusafirisha bidhaa nchi za nje tu.

Serikali, Babu aliandika, lazima ianze kuchukua hatua za kuwashajiisha wajasiriamali wananchi ambao uwekezaji wao wa hivi sasa katika biashara unaweza kuelekezwa katika shughuli zenye faida zaidi za viwanda vya kutengenezea vitu huku wakisaidiwa, kama itakuwepo haja, na kiasi fulani cha vifaa na fedha kutoka nchi za nje.

Kwa mukhtadha wa mtazamo huu, ni wazi kuwa huko ndiko ambako mapato ya siku za mbele kutokana na mafuta yanakoweza kuelekezwa kwa ajili ya uwekezaji – kwa ajili ya uzalishaji wa ndani na kuendeleza soko la ndani, na hatimaye kutengeneza bidhaa za viwandani ambazo zitaweza kusafirishwa nchi za nje kwa ushindani katika nchi nyengine za Afrika ya Mashariki, Afrika ya Kati na Kusini mwa Afrika na katika nchi za Ghuba na za Bahari ya Sham, kaskazini.

Dira ya Babu, inatoa hoja kuhusu Zanzibar ambayo ingeliweza kuwa. Lakini pia inaweza kuwa ni Zanzibar ya siku za mbele. Katika hali ya kushindwa kwa mfumo huria mambo leo na mateso ya unyonyaji wa kikatili wa ubepari unaoporomoka, mawazo kama ya Babu hivi sasa yana umuhimu mkubwa zaidi kuliko wakati mwengine wowote wa hapo kabla. Yanadurusiwa tena na wale wote wanaotaka ukombozi kutokana na ubeberu na haki ya kiuchumi. Labda hapo baadae yatasaidia kuwepo kwa Zanzibar ya kisoshalisti iliyo tofauti. Na kama kwa juu juu tu, Zanzibar imebadilika, kama unavyoonyesha waraka niliounukuu katika kitabu hiki, leo, katika maendeleo ya kisiasa ya kila siku, na mara nyingi yakisimamiwa na kuangaliwa kama ilivyokuwa katika miaka ya vita baridi, na wawakilishi wa kijeshi na kiuchumi – walio tayari kuingilia kati moja kwa moja ikiwa njia nyengine yoyote itashindwa. Maoni ya Babu, yaliyoandikwa miaka 40 iliyopita katika sehemu za mwisho ya utangulizi wake katika kitabu cha Walter Rodney How Europe Underdeveloped Africa, bado yanafaa hadi hivi leo:

Ikiwa kwa kuangalia tulikotoka tumeweza kuyajua ya hivi sasa, ili kuyajua ya siku za mbele lazima tuangalie tulikotoka na tulipo hivi sasa. Vitendo vyetu ni lazima vilingane na uzoefu wetu halisi, na tusizipe fursa dhana za matakwa na matumaini ya kishirikina kidhanifu – tukitaka na tukiwa na matumaini kuwa zimwi lililokuwa likituandama katika kipindi chote cha historia yetu, siku moja litageuka na kuwa kondoo. Halitageuka. (Babu, [1971] 2002)


  1. Ilikuwa ni huko Yemen ambako mwezi September 2011, ndege zisizokuwa na rubani za Kimarekani ziliwalenga na kuwaua raia wa Marekani, Anwar Awlaki na Samir Khan. Wiki mbili baadae, katika hali ambayo mpaka sasa haikuelezwa, mtoto wa kiume wa miaka 16 wa Awlaki, Abdulrahman, raia mwengine wa Marekani, aliuliwa vile vile kwa shambulio la ndege isiyokuwa na rubani. Imedaiwa kuwa Rais Obama atapewa madaraka ya kuwalenga raia wake mwenyewe, kuwaua bila ya mashtaka yoyote au mchakato wowote wa kisheria, mbali na uwanja wowote ule wa mapigano (Greenwald, 2013).
  2. Mashambulizi haya yalifanywa kwa wakati mmoja huko Nairobi na Dar es Salaam, na kuua mamia ya watu. Inaaminiwa kuwa huo ulikuwa ni ulipizaji wa kisasi kwa Marekani kwa kujihusisha na kuwarudisha, na kuwatesa wanachama wanne wa chama cha Misri cha Jihadi ya Kiislamu waliokamatwa Albania.
  3. Wakati huo huo Marekani ilianza kuvunja sheria za kimataifa moja baada ya nyengine, ikipuuza matakwa ya Umoja wa Mataifa na kujitoa katika mikataba husika ya kimataifa. Kama alivyoandika Mahmood Mamdani, ‘Marekani kuibuka kuwa ndiyo taifa kubwa lenye nguvu pekee duniani kumekwenda sambamba na madai yake ya kutaka isihusishwe na utawala wowote wa kisheria wa kimataifa’ (2005: 208).
  4. Kama Dershowitz na Paul walivyoeleza, ‘Hata hivyo, wakati huo huo wajumbe wa Baraza wameshindwa kuchukua hatua dhidi ya uhalifu mkubwa wa baharini katika bahari hiyo hiyo: meli za uvuvi za kigeni zilizokuwa zikiiba utajiri wa baharini wa Somalia, pamoja na meli za kigeni zilizotupa taka za sumu nje ya fukwe za Somalia’.
  5. Karume, kama Marekani walivyoeleza sehemu nyengine, alielezewa katika simu nyengine kuwa hakutaka uwepo mwafaka kwasababu ya ‘mambo nyeti ya kihistoria akiwa mtoto wa mapinduzi’ (Ubalozi wa Marekani, 2009l).
  6. Kusema kweli, Daftari la Kudumu la Wapiga kura kwa kiwango kikubwa liliwapendelea CCM. Wakati wa uchaguzi wa 2005 kabla ofisi za kupigia kura hazikufunguliwa ofisi ya CUF walipewa orodha ya muda ambayo haikufuata alfabeti wala haikuorodhesha majimbo, na hii ilikuwa ndiyo orodha pekee iliyokuwepo kwa miaka kadha baadae.

License

Tishio la Ukombozi Copyright © 2016 by Amrit Wilson. All Rights Reserved.

Share This Book

Feedback/Errata

Comments are closed.