5 Utawala wa Kidikteta wa Karume

Baada ya kuepukana na Babu na wengine kutoka Zanzibar ambao aliwaona kuwa wangeliweza kuwa tishio kwake baada ya muungano, Karume aliwafukuza takriban wasomi wote waliokuwa wajumbe wa Baraza la Mapinduzi na kuanza kuitawala nchi kama kwamba ni eneo lake binafsi la utawala wa kitemi.

Mwezi Februari 1965 zilipitishwa sheria za kuahirisha kwa muda usiojulikana kuitishwa kwa Bunge la Katiba. Miaka minane iliyofuatia ilikuwa ni kipindi cha umwagaji damu mkubwa kisicho na kifani na vitisho na ambacho utawala wa sheria ulipuuzwa, wapinzani waliuawa kinyama, udhalilishaji wa kijinsia na ndoa za kulazimishwa zilizagaa. Vyama vya wafanyakazi na jumuiya zote za wananchi zilipigwa marufuku na harakati za kuingia na kutoka Zanzibar zilidhibitiwa kikamilifu. Chama cha ASP na Serikali ya Zanzibar vilifanywa kuwa ni kitu kimoja. Zaidi ya hayo, kwa kuwa Karume alikuwa na madaraka yasiyokuwa na mipaka, bila ya kuwepo namna yoyote ya uwajibikaji, visiwa vya Zanzibar vilikuwa wazi kwa uporaji uliofanywa na familia ya Karume.

Kama alivyoandika Tahir Qazi alipoichambua Misri ya Mubarak:

Utawala wa kidikteta huzaa tabaka la watu wachache wenye uwezo na kujenga ihramu ya kijamii ambayo madaraka, mali na fursa hujikita kileleni … kwa jina zuri zaidi, Ihramu ya Dhulma. Watawala wa kidikteta kwa msaada wa wafadhili wao wa kigeni hujenga dola tegemezi … Hii inasababisha mgawanyiko muhimu kwa wananchi … kwasababu zilizowazi na zilizofichika. (Qazi, 2011)

Hivi ndivyo ilivyokuwa Zanzibar katika miaka ya baada ya Muungano. Kiuchumu, kijamii na kisiasa Zanzibar ilipitia kipindi cha miaka yake mibaya kabisa ambacho hakijawahi kutokea katika karne nzima. Wananchi walididimia wakati wale wa tabaka la watu wa kati, au wale waliokuwa na ujuzi walitafuta njia ya kuvikimbia visiwa hivyo. Kama Karume angelikuwa kweli mwenye hisia za Kizanzibari, kama wengi wanavyodai, angeliuvuruga mfumo wa jamii ya Zanzibar?

Karume Akabidhi Vibaraka Wake Madaraka ya Jeshi

Akielewa kuwa angelilihitaji jeshi ili kulinda nafasi yake, Karume aliliunda upya jeshi hilo ili kukabidhi madaraka kwa vibaraka wake aliowaamini sana. Katika kipindi cha mara tu baada ya mapinduzi, wanachama wa Chama cha Umma Party ambao walikuwa Cuba walifanyakazi kwa juhudi kubwa ili kulianzisha jeshi la Zanzibar, Jeshi la Ukombozi la Zanzibar. Lakini mamlaka ya kidikteta ya Karume yalipozidi kukua alianza kuwaona watu hawa kuwa ni tishio. Kama Shaaban alivyonambia, ‘Karume alitaka tuwe pembeni. Kwa hivyo mwezi Julai 1964 kati yetu sisi 18 ambao tulipata mafunzo Cuba tulipelekwa Urusi kwa kipindi cha mwaka mmoja’ (mahojiano na Shaaban, 2009).

Waliporudi mwaka 1965, walibaini kuwa wasingeliruhusiwa kurudi Zanzibar. Kama alivyonambia Hamed Hilal:

Lilikuwa jambo la kuchekesha namna tulivyolibaini jambo hili …Tulipowasili kutoka Moscow tuliwekwa hoteli Dar es Salaam. Siku ya pili yake tulikuwa tumeshughulika makao makuu ya jeshi. Hatukuwa na muda wa kuwasiliana na Babu au makomred wengine. Lakini kwa mshangao, kiasi cha saa 2 za usiku tulipoteremka chini kwenye ukumbi wa hoteli, nje ya varanda tuliwaona Babu, Badawi na Saleh Saadalla … Badawi ndiye aliyetoa siri kuwa tulikuwa hatutakiwi Zanzibar. Hili lilithibitishwa kwetu tulipokwenda Zanzibar kwa mapumziko ya wiki mbili na kwenda Ikulu kumsalimia Karume. Alitwambia kuwa ama twende katika ofisi za ubalozi kama waambatanishi wa kijeshi au twende tukafanye kazi bara. Tulichagua pendekezo la pili kwasababu tulitaka kubakia jeshini kwa kuwa hii ndiyo iliyokuwa kazi yetu. (Mahojiano na Hamed Hilal, 2011)

Waligawiwa katika makundi mawili, kundi moja lilipelekwa Tabora na kundi jengine lilipelekwa kwenye kambi ya jeshi ya Nachingwea. Hamed aliendelea:

Lilikuwa ni jambo lililoandaliwa. Ijapokuwa ilikuwa ni jambo la kawaida kwa maafisa wa kijeshi kupangwa katika vikosi mbalimbali baada ya kumaliza mafunzo yao, kwetu sisi, madhumuni makubwa yalikuwa ni kupeleleza na kufuatilia mienendo yetu pamoja na kuzuia mawasiliano kati yetu na wenzetu wengine ambao walikuwa wanachama wa Chama cha Umma Party. Maafisa makachero wa kijeshi walipewa kazi ya kutupeleleza. Walitoa taarifa kuhusu mienendo yetu hapo makao makuu na makao makuu nao walitoa taarifa Zanzibar. (Mahojiano na Hamed Hilal, 2011)

Kundi la Nachingwea la waliokuwa wanachama wa Chama cha Umma Party lilijenga urafiki mkubwa na maafisa wenzao, pamoja na maafisa makachero, na kuweza kuaminiwa. Baadaye, maafisa makachero waliwaambia kuwa wapo pale ili kuwapeleleza na kutoa taarifa kuhusu mwenendo wao. Baada ya miezi michache maafisa hawa wa usalama walibaini kuwa hapajakuwepo na lolote la kutia wasiwasi na kutoa taarifa na upelelezi uliachwa. Lakini waliokuwa wanachama wa Chama cha Umma Party walibakia katika nafasi hizi kwa miaka mingine miwili. Baada ya hapo, kama Hamed alivyonambia, ‘baadhi yetu tulihamishiwa Dar. Hapa tulikutana tena na tulikuwa na Babu takriban kila mwisho wa wiki.’ [1]

Hiki ni kipindi ambacho, kama Shaaban alivyonambia, Karume alipoliunda upya jeshi akiwa pamoja na wajumbe wa kamati ya watu Kumi na Nne kama Seif Bakari na Abdalla Natepe, na Yusuf Himid, aliyefanywa kuwa kamanda. (Ali Mahfoudh aliyekuwa kamanda wa Jeshi la Ukombozi naye pia alihamishiwa bara miezi michache baadae na kupelekwa kwenye mpaka wa Tanzania na Msumbiji kusaidia kuwafunza wapigania uhuru wa Msumbiji.) Shaaban aliniambia:

Wakati huo bado lilikuwepo jeshi la Zanzibar, lakini yalikuwepo mapendekezo kuwa liungane na jeshi la Tanganyika na watu wa Zanzibar hawakujua namna ya kulipinga hilo … Jeshi la Ukombozi lilivunjwa mwaka 1966. Palikuwa na ombwe na baadae kilikuja kipindi cha mauaji …Seif Bakari na wajumbe wa Kamati ya Watu Kumi na Nne waliwaua watu kadha na wengine wengi walitoweka – hata hivi leo hapana anayejua nini kiliwatokea. Na ulikuwepo mchakato ulioendelea wa kuwaondoa watu wote wale waliopenda maendeleo kutoka katika jeshi na kutoka katika serikali ya Zanzibar. (Mahojiano na Shaaban Salim, 2009)

Siku za Machafuko na Dhulma

Katika kipindi hiki, wale waliokuwa madarakani Zanzibar na Tanzania yote kwa jumla waliwaona wajumbe wa Kamati ya Watu Kumi na Nne kuwa ni mashujaa wa kitaifa. Tarehe 12 Januari, 1965 wakati wa sherehe za mwaka wa kwanza wa mapinduzi, gazeti la The Nationalist la Dar es Salaam kwa mfano, lilikuwa na picha zao katike kile kilichoitwa ‘ Picha za watu 14’ walioagizwa na kuongozwa na Abeid Amani Karume, Makamo wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuandaa matayarisho kwa machafuko yaliyomaliza utawala wa Sultani.

Watu hawa sasa waliweza kufanya lolote lile walitakalo bila ya kuchukuliwa hatua yoyote, kama kutia watu gerezani, na kutesa mtu yeyote wamtakae. Uwekaji watu kizuizini bila ya muda maalum, utesaji na mauaji ya kiholela yalikuwa ni mambo ya kawaida. Watu waliuliwa kwa kuikosoa serikali au kwa kuonekana kuwa ni wapinzani au kwa kulipiza kisasi au mara nyengine bila ya sababu yoyote, (mahojiano na Shaaban Salim na Khamis Ameir, 2009). Vilianzishwa vyumba vya kutesea watu katika kila sehemu ya visiwa vya Zanzibar na humo, wanawake na wanaume wasiokuwa na hatia walifanyiwa ukatili wa kinyama. Sehemu iliyokuwa ovu kuliko zote katika sehemu za kutesea ilikuwa ni kwa Bamkwe kama mahali hapo palivyojulikana kwa umaarufu wake. Ilikuwepo ndani ya jela kuu hapo Kiinuwamiguu (Zanzibar Election Watch, 2005: 3).

Chini ya uongozi wa Karume, Kamati ya Watu Kumi na Nne ilijiimarisha kwa kujijengea vikundi vingine vya watu wa vurugu ili viwalinde, miongoni mwao wakiwemo wengi waliopatiwa mafunzo juu ya mbinu za utesaji na maafisa wa shirika la ujasusi la Ujarumani ya Mashariki. Watesaji waliandaliwa katika vikundi, miongoni mwao kikiwemo Kikundi Nambari Nane kilichokuwa maarufu. Kamati ya Demokrasia ya Zanzibar iliwataja kwa majina wengi wa watesaji hawa katika gazeti lake la kila mwezi lililokuwa sehemu ya Zanzibar Election Watch (2005: 3), na kueleza kuwa wengi wao, wakiwemo watu waliowatesa Hashil na Hamed walishika nafasi muhimu katika ofisi za ubalozi wa Tanzania na katika idara za ujasusi na baraza la mawaziri.

Mwaka 1967 kikundi cha Karume serikalini kilianza kuwalenga wanachama wa ASP waliopenda maendeleo mmoja baada ya mmoja. Watu waliokamatwa kiholela na serikali hiyo walilazimishwa kukiri makosa na kuwaingiza watu hawa na wengine katika makosa kwa kulazimishwa. Mfano mmoja, Kepten Ahmada, mwanachama wa Chama cha Umma Party, alilazimishwa kuwataja watu 19 – wengi wao wakiwa walioikosoa serikali hiyo – kuhusika na mpango wa kubuniwa wa kumpindua Karume. (Ilikuwa ni Ahmada na Humud Mohamed, ambaye pia ni mwanachama wa Chama cha Umma ndio inasemekana waliomwua Karume mwaka 1972.)

Wanachama wa ASP waliotajwa walishitakiwa na kushutumiwa hadharani na baadae kufungwa na kuuliwa bila ya hata kupelekwa mahakamani. Abdulaziz Twala, aliyekuwa waziri wa fedha na kuwahi kuwa kiongozi wa vyama vya wafanyakazi aliuliwa, kadhalika na Saleh Sadalla. Mwaka 1968 Hanga na Othman Shariff, nao pia waliuawa kinyama. Kama alivyobaini mke wa Hanga Lily Golden, mwanahistoria na mwanaharakati wa kisiasa mwenye asili ya Kirusi- Kiafrika na Kimarekani kwenye nyaraka za siri alizozipata, Hanga alipigwa risasi katika masafa ya karibu na mwili wake uliokatwa vipande vipande kutoswa katika Bahari ya Hindi. (Free Library, 2009).

Kama Shaaban alivyokumbuka, kipindi hicho pia kilishuhudia mfululizo wa kufukuzwa na kufungwa gerezani wale waliopenda maendeleo na ilikuwa katika kipindi hiki ambapo Badawi na Ali Sultan wote wawili walifukuzwa. Ilikuwa katika kipindi hiki vile vile ambapo uongozi wa ASP, ukihofu hali ya Babu kuungwa mkono na wengi visiwani, ndipo walipotaka kuwa naye pia afukuzwe na Nyerere kutoka katika nafasi yake ya uwaziri na kurejeshwa Zanzibar kama alivyofanyiwa Hanga hapo awali. Lakini Nyerere, labda kwa kujua nini ambacho kingelitokea, alikataa.

Mwaka 1969, ili kumwezesha kuepukana na wapinzani wake wote, Karume na vibaraka wake walifanya mabadiliko makubwa ya mfumo wa mahakama. Mahakama za chini ziliondolewa na nafasi yake kuchukuliwa na Mahakama za Wananchi. Mahakama hizi ziliongozwa na watu watatu, mwenyekiti na wengine wawili walioteuliwa na rais, walifanya kazi ‘pale rais alipopenda’. Majaji hawa walikuwa, bila ya shaka yoyote, watu wasiosoma na wasioelewa chochote kuhusu sheria au taratibu za kisheria. Kama wengi wa wafuasi wa Karume waliokuwa waumini wa siasa za mrengo wa kulia, walikuwa ni watu waliotaka kulipiza kisasi na waliotoa hukumu za kesi kwa ukatili. Waliamua juu ya taratibu za mahakama bila ya kupingwa na mtu yeyote kwa kuwa mawakili hawakuruhusiwa kuingia katika mahakama hizo. Kama alivyokumbuka Khamis, “Watu wengi walikamatwa na kupotea. Walikuwa wanaweza kukutia ndani. Halafu watakwambia, unawaona wale watu wanaotembea kule nje? Wale ni watu wazuri. Wewe upo hapa kwasababu una hatia .” Mahakama za wananchi zilibaki kuwa ndiyo muhimili wa mfumo wa sheria mpaka katika miaka ya 1980 (Mahojiano na Khamis Ameir, 2009).

Khamis anakumbuka kuwa alikuwa ni yeye tu peke yake miongoni mwa waliokuwa wanachama wa Chama cha Umma Party ambaye alibaki katika Baraza la Mapinduzi.

Mara nyingi walitaka kunitoa. Lilikuwepo tukio lililohusu mishahara ya wafanyakazi, halafu suala la vita vya Vietnam na wakati fulani Karume alisema, ‘Tumepata habari kuwa unawapa kazi Waarabu.’ Halafu mtu mmoja kutoka katika ofisi yake alisimama kunitetea na kusema, ‘Hapana, siyo yeye …’ halafu jambo la mwisho lilikuwa, ‘Wewe Mwarabu – wa damu mchanganyiko. Wewe ni mchanganyiko wa nani na nani?’ Nilimtazama nikasema, ‘Kutoka katika kabila yako.’ Karume alitoka Malawi, na bibi yangu alitoka Malawi. Nilimwambia hayo. Alinitazama halafu alibadili mada. Baada ya hapo matatizo yote yalimalizika. Kila wakati ambao iliundwa kamati, husema, ‘Mwingizeni Khamis!’ Wakati mwengine mimi husema, ‘Siwezi kuwemo katika kamati hiyo, hao wanaiibia serikali.’ Atashikilia, ‘Lazima uwemo humo!” (Mahojiano na Khamis, 2009)

 Kwa watu wengi wa Zanzibar, jambo baya kabisa wakati wa utawala wa Karume lilikuwa ni upungufu mkubwa wa chakula uliosababishwa na sera zake. Uchumi ulikuwa haukubadilishwa au kufanywa kuwa wa kisasa. Ulibaki kutegemea zao la karafuu kwa ajili ya kusafirisha nchi za nje na kuwa katika hatari ya kupanda na kushuka kwa bei katika soko la dunia. Lakini lililokuwa baya zaidi ni kuwa mapato yaliyopatikana kutokana na mauzo ya karafuu yalifichwa ili watu wa Zanzibar waendelee kupata shida hata wakati ambapo bei ya karafuu ilikuwa juu. Pesa zilifichwa katika tawi la London la benki ya Mosko ya Norodny Bank, wakati huo huo uagizaji wa chakula ulipigwa marufuku.

Ilipofika mwaka 1972 madhila ya watu yalikuwa makubwa kiasi ambacho, kama anavyoandika Chase:

Upinzani uliojificha kwa muda mrefu dhidi ya utawala wa Chama cha ASP ulianza kuwa na sura ya kuungwa mkono na umma wote. Kwa mara ya kwanza tokea mwaka 1967 ulipokuwepo ’mpango wa kumpindua Karume’. Kwasababu ya upinzani huo serikali ya Karume iliandaa mpango mwengine wa kuwafukuza wale waliowadhani kuwa ni wapinzani, hasa wale ambao jukumu lao la kihistoria liliwafanya kuonekana kuwa watarajiwa wa kuungwa mkono na umma. (Chase, 1976: 19)

Mnamo mwezi Februari mwaka huo Karume alipeleka ujumbe mzito Dar es Salaam kudai kuwa Babu arudishwe pamoja na wengine waliokuwa wanachama wa Chama cha Umma Party ambao walikuwa bara. Madai haya yalitokana na kuwa utawala wa Karume Zanzibar kila ulivyozidi kuwa ni wa kidhalimu, Babu alijitokeza kuwa ni mpinzani mkubwa wa serikali ya ASP.

Mara hii Nyerere alikataa tena kumrudisha Babu lakini alikubali suluhisho la kumfukuza kutoka katika wadhifa wake. Namna ya kumfukuza kwake inadhihirisha kuwa Nyerere alitaka kushirikiana na Karume katika jaribio la kutaka kumdhalilisha Babu hadharani. Bila ya sababu yoyote, alimtaka awe naibu waziri wa mambo ya nje chini ya John Malecela na kuongoza ujumbe wa Tanzania katika mkutano wa Baraza la Mawaziri la Umoja wa Nchi Huru za Afrika. Wakati Babu akiwa nje ya nchi akihudhuria mkutano huu, ghafla na mbele ya hadhara alifukuzwa kutoka katika wadhifa wake wa waziri wa mambo ya uchumi na mipango ya maendeleo. (Babu, 1996: 331)

Kuuliwa kwa Karume na Baada ya Hapo

Ilikuwa katika mazingira haya ya njama za hali ya juu za serikali, hali ya ukandamizaji uliokithiri visiwani Zanzibar na hasira za wananchi zilizozidi kupanda, ndipo Karume alipouawa tarehe 7 April, 1972. Watu wawili waliomwua Karume wote walikuwa wanachama wa zamani wa Chama cha Umma, Luteni Humud Mohamed, ambaye risasi zake ndizo hasa zilizomwua Karume na Kepten Ahmada. Kila mmoja wao alikuwa na sababu zake binafsi za kumwua Karume. Baba yake Humud aliuliwa akiwa gerezani, na inatuhumuiwa kuwa ilikuwa ni kwa amri ya Karume, na Ahmada aliteswa na serikali ya Karume mateso yaliyomsababisha atoe tuhuma za uongo. Humud na Ahmada, na watu wengine wawili ambao inasemekana walihusika na mauaji hayo, waliuliwa na polisi kufuatia kifo cha Karume.

Wakati Wazanzibari wengi inawezekana kuwa walifurahia, angalau kwa siri, kifo cha Karume, kilipelekea kuwepo kwa hali ambayo vibaraka ambao Karume aliwaamini sana na waliokuwa na vurugu kubwa wakiongozwa na Seif Bakari ndio waliokuwa kundi pekee lililokuwa na madaraka visiwani.

Hatimaye Aboud Jumbe aliteuliwa kuwa rais mwengine wa Zanzibar. Alikuwa ndiye mtu mwafaka aliyeteuliwa kwanza kwasababu alikubalika kwa kundi la Bakari na pili kwasababu hakuchukiwa sana na wananchi ukimlinganisha na wengi wengine waliokuwemo katika serikali ya Karume. Alikuwa ni mmoja miongoni mwa wasomi wachache waliovumiliwa na Karume, alikuwa mwerevu wa kutojali hata uonevu na ukatili wa dhahiri. Sasa alitumia werevu wake katika kutafuta suluhisho na makubaliano na serikali. Haya yalimwezesha pia kuimarisha nafasi yake, kuidhibiti na hatimaye kujikita kikamilifu katika madaraka yake.

Kikundi cha Seif Bakari kilichukua madaraka mara tu baada ya Karume kuuwawa na watu 1,100 walikamatwa na kutiwa gerezani katika siku chache zilizofuata. Miongoni mwao walikuwemo wengi waliokuwa wanachama na washabiki wa Chama cha Umma Party na wanachama wa ASP – wale waliodhaniwa kuwa wapinzani wa serikali ya Karume na kwa hivyo kuchukuliwa kuwa ni wapinzani wa kisiasa wa kikundi hicho.

Yaliyotokea kuanzia hapo mpaka kuanza kwa ile iliyoitwa Kesi ya Uhaini yalikuwa katika vipindi vinne vilivyofuatana. Cha kwanza kilikuwa ni cha kuwakamata na kuwahoji wale waliokuwepo kizuizini Zanzibar na ‘kukiri’ kwao baada ya mateso makubwa na baadhi ya wakati kwa maumivu ya kifo. Cha pili ni kile cha kubuniwa kwa mpango mkubwa uliotokana na ushahidi unaotokana na ‘kukiri’ kwao huko. Madhumuni ya ‘mpango’ huo ambao unadhaniwa kuwa uliongozwa na Babu na Chama cha Umma Party, yanadaiwa kuwa yalikuwa ni kumwua Karume na baadae kuchukua madaraka visiwani. Cha tatu, ni pale watu walipokuwa wakilazimishwa kukiri na ‘mpango’ huo kubuniwa kilikuwa ni kukamatwa kwa Babu na baadhi ya waliokuwa wanachama wa Chama cha Umma bara. Cha mwisho kilikuwa ni kuhojiwa kwa watu hawa, kuhojiwa ambako kuliandamana na mateso ya wawili kati yao, Hashil Seif Hashil na Hamed Hilal (mahojiano na Hamed Hilal, 2011).

Khamis alikamatwa tarehe 18 April, 1972, akiwa kada wa mwisho wa Chama cha Umma kukamatwa Zanzibar baada ya mauaji. Alikuwa ni yeye pekee aliyebakia katika Baraza la Mapinduzi na kama alivyonieleza ‘ ni rais tu ndiye aliyeweza kutia saini ili mjumbe wa Baraza la Mapinduzi akamatwe. Kwa hivyo, mara baada ya Jumbe kuwa rais, nilikamatwa na kutiwa gerezani ambako niliwakuta makomred wenzangu wengine huko!’ (mahojiano na Khamis Ameir, 2009).

Alipofika gerezani Khamis aliyakuta mateso yakimsubiri. Walifanyiwa vitendo vya utesaji wa kinyama hadi watu watatu – Musa Abdalla Ali, kwa umaarufu wake akijulikana kwa jina la ‘Meki’, Luteni Ali Othman na Abbas Mohamed, wote hao wakiwa ni watu waliokuwa wanachama wa Chama cha Umma Party – walikufa hata kabla ya kesi kuanza. Wengine, miongoni mwao wakiwemo Saleh Ali na Mohamed Saghir, walikufa mara baadae. Chumba cha kuhojiwa, kwa mujibu wa maelezo ya mshitakiwa mmoja, ‘kilifanana na machinjio yaliyotapakaa damu ya binadamu’ (Chase 1976: 24). Mateso mengine yaliyofanyika yalikuwa ni pamoja na ukatili wa kijinsia, kulazimishwa kusimama huku mtu akiwa amefukiwa hadi shingoni katika mchanga au matope, ukatili wa kisaikolojia: kuwekwa katika chumba cha mahabusu nyoka waliotolewa meno, mahabusu kuvyetuliwa risasi kutoka kila upande, kuning’inizwa kwenye kamba iliyozungushwa shingoni na kutegewa kwa namna ambayo isingeliweza kuua (mahojiano na Khamis Ameir, 2009).

Mara kadha mwaka 1972, ‘Dourado [mwanasheria Mkuu Wolfgang Dourado aliyekuwa mwendesha mashtaka ] akija katika chumba cha kuhojiwa’, Khamis aliniambia, ‘husoma maelezo yaliyoandikwa na baadae kusema, “Inabidi mumkamue zaidi mtu huyu”, yaani mateso zaidi. Mahakamani alisema, “mikono yao ilisokotwa tu, basi,” kusema kweli, maelezo ya Dourado juu ya mada hii yanastahili kunukuliwa yote kwa ukamilifu. Yanaonyesha mtazamo wa matukio yanayofanana na hayo ya hivi sasa katika kesi za wale walioshtakiwa kwa mujibu wa sheria za ugaidi za Uingereza na Marekani. Hapa pia, matumizi ya ushahidi uliopatikana kwa njia ya mateso ni jambo la kawaida.

Wakati wa kesi, wale waliokubali makosa katika maelezo yao waliyakataa makosa hayo. Walieleza kuwa maelezo hayo yalipatikana kwa namna isiyo sahihi na kwa hivyo hayakuwa maelezo yaliyotolewa kwa hiari. Kwasababu, ya namna ya hali ilivyokuwa wakati wakutoa maelezo hayo walilazimishwa kukiri makosa na kutunga uongo na wakati mwengine maafisa wa upelelezi waliyaongezea maelezo yao ili kuipa kesi uzito mkubwa zaidi dhidi yao. Swali linalojitokeza kwanza ni kuwa, maelezo haya yanakubalika kisheria? Jibu fupi kwa swali hili ni kwamba kwa kuwa hayatakubalika chini ya mifumo mingine ya sheria, mfumo wetu hauna kizuizi cha kuzuia kukubalika kwa maelezo kama hayo. Mheshimiwa ataona kuwa ninakiri kwamba umekuwapo usokotaji wa mkono kidogo (utumiaji wa nguvu) ili maelezo haya yapatikane. (Chase, 1976: 24)

Kamatakamata, Kuweka Gerezani na Mateso Bara

Baada ya takriban mwaka mmoja wa mahojiano ya kikatili yaliyoambatana na mateso kwa wale waliotiwa gerezani, serikali hatimaye iliyapata matilaba yake ya kuwafanya wahojiwa ‘wakiri’. Kabla ya hapo, siku sita tu baada ya mauaji, makada wote wa kile kilichokuwa Chama cha Umma Party ambao wakiishi bara, pamoja na Babu, walikamatwa na kuwekwa gerezani.

Wakati akikamatwa, Babu alikwishajua kuwa alikuwa hatarini, kwasababu wakati wa maziko ya Karume, tarehe 10 April, tayari zilikuwepo dalili za nini kingelitokea. Edington Kisasi, kamishna wa polisi, alimwambia Mohammed Sahnun, Mualgeria aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika aliyekuja kuhudhuria maziko hayo, ‘tutampata Babu, akiwa hai au amekufa’ (Babu: 1975; 1). Sahnun alishtuka na alipowasili Dar es Salaam wakati akirudi Algeria, alimtumia ujumbe Babu akimweleza kuhusu tishio hilo ovu. Hapo hapo, Babu alimwarifu Makamu wa Rais, Rashid Kawawa na kumtaka achukue hatua zinazofaa. Alitaka vile vile kumwona Nyerere, lakini ombi lake, kama Babu alivyokumbuka, lilikataliwa kwa utovu wa adabu mkubwa (Babu, 1975: 2).

Kukamatwa ambako Babu alikwisha tahadharishwa nako kulikuwa kwa namna ya kikatili. Kama alivyoandika katika barua aliyoituma kwa Tume ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa:

Tarehe 13 April, saa tisa alfajiri, nyumba yangu ilizungukwa na polisi wa kijeshi. Wakiwa na silaha nyingi na kwa mtindo ule ule wa Kigestapo walisukuma mlango wa nyumba yangu kwa jina la sheria na utulivu, walinikamata na kunifunga pingu, na kuzielekeza kichwani kwangu bunduki zao za rashasha zilizokuwa na risasi ndani.

… Ijapokuwa sikuonyeshwa hati yoyote ya kukamatwa au hati ya kunisachi, au kuelezwa kikosi hiki cha kinyama kilikuwa ni kwa ajili ya nini, hata hivyo, kikundi cha makachero kiliingia ndani wakiwa pamoja na wanajeshi waliokuwa na silaha na kuanza kuvurugavuruga kila kitu ndani ya nyumba yangu na kuchukua kitu chochote ambacho walidhani wanakitaka …Wakati wakiendelea kuvuruga kila kitu ndani ya nyumba yangu waliniamuru nitoke nje … huku nikiiacha familia yangu iliyokuwa katika hofu. Sikuwa na chaguo lolote. Walikwishanifunga pingu kwa hivyo waliniburura na kunitoa nje ya nyumba, kwa mabavu na kunivurumisha ndani ya gari lililokuwa likisubiri, ndani yake wakiwemo wanajeshi zaidi waliokuwa na silaha. (Babu, 1975: 2)

Alipelekwa katika gereza la Ukonga ambako kwa muda wa wiki mbili aliwekwa peke yake kabla ya kuhamishiwa gereza la Tabora kupitia gereza la Dodoma huku akiwa amefungwa minyororo. Gerezani Tabora, Babu alitupwa katika ‘chumba cha wale waliohukumiwa kifo’ karibu na chumba cha kunyongea. Alikaa hapo kwa muda wa miezi kumi ambayo saba katika hiyo akiwa ametengwa katika hali ya upweke. Katika kipindi chote hiki hakuambiwa sababu ya kuwekwa kwake kizuizini ijapokuwa kwa mujibu wa Sheria ya Kuweka Watu Kizuizini alikuwa na haki hiyo, kama zipo chache nyengine kwa vile sheria hii ya kikoloni (ambayo bado imo katika vitabu vya sheria vya Tanzania ) inawanyima wale waliofungwa jela chini ya sheria hiyo takriban haki zote za kiraia.

Siku hiyo hiyo, makada wote waliokuwa bara wa kile kilichokuwa Chama cha Umma Party, walikamatwa vile vile. Hamed Hilal, aliyekuwepo Dar es Salaam, alikamatwa pamoja na mke wake Fatma. Walipelekwa gereza la Keko ambako maafisa wengine wa jeshi kutoka Zanzibar waliokuwa wakifanyakazi bara walikuwa tayari wamekwishawekwa ndani. Hamed alinambia:

Walikuwemo wanawake wanne wa Kizanzibari waliokamatwa katika kipindi hiki. Mke wa Humud, Fathiya Humud aliachiwa baada ya miezi mitatu kwasababu ya uja uzito, na wengine, pamoja na mke wangu waliachiwa baada ya miaka miwili. Mke wangu alirudi katika hospitali ya jeshi ambako alikuwa akifanyakazi lakini aliambiwa kwamba ‘kwasababu za kiusalama’ asingeliweza kuajiriwa tena. Hata hivyo, aliweza kupata kazi katika zahanati ya mtu binafsi mpaka alipokwenda Dubai pamoja na watoto wetu na mama yake aliyekuwa akiwaangalia wakati akiwa gerezani. Ilikuwa baada ya kuachiwa kwangu ndipo nilipomuona mke wangu alipokuja kunitembelea kwa mwezi mmoja. (Mahojiano na Hamed Hilal, 2011)

Kuwekwa gerezani kwa wanawake hawa, ambao ni wazi kabisa hawakuwa na uhusiano wowote na mauaji, kulionyeha kwa mara nyengine tena chuki ya serikali ya Zanzibar dhidi ya wanawake wa Kiarabu na chuki yake dhidi ya Waarabu. Ukiukwaji huu wa wazi na wa kikatili wa haki za binadamu ambao wanawake kama Fatma Hilal na Fathiya Humud walihukumiwa kwasababu ya vitendo vya waume wao (Fathiya aliwekwa gerezani hali akiwa ana mimba na mumewe amefariki) uliachiwa upite hivi hivi bila ya hata neno moja la kukaripia kutoka kwa Nyerere. Maelezo yake ya mwaka 1969 (aliyoyatoa alipozungumzia vita vya Biafra) kuwa ‘kama hatukujifunza kuikosoa dhuluma ndani ya bara letu, tutajikuta tunauvumilia ufashisti katika Afrika, ilimradi tu unafanywa na serikali za Afrika dhidi ya wananchi wa Afrika’ (Pomerance, 1982) yalidhihirisha ya kuwa ni zoezi la kujibeza mwenyewe.

Lilikuwepo jaribio la kulifanya zoezi hili la ukamataji kuwa ni siri kwasababu pale alipoulizwa na waandishi wa magazeti kutoka nchi za nje, waziri wa mambo ya ndani aliyefanya ukamataji huo alikataa katakata kuwa Babu alikamatwa (Babu, 1975: 2). Ni wazi kuwa Nyerere aliona aibu, lakini kama ilivyokuwa kila mara, hakufanya lolote na kutochukua hatua kwake kulimfanya awe mshiriki wa kikamilifu katika ukatili huu.

Mke wa Babu, Ashura na watoto wao waliruhusiwa kumtembelea Tabora, ijapokuwa gharama na muda wa kwenda huko kuliwazuia kuweza kwenda huko kila mara isipokuwa kwa mara chache tu. Kwa kupitia kwao, alijua kuhusu kukamatwa kwa mamia ya wengine Zanzibar na taarifa za mateso ya kutisha.

Mwezi Machi 1973, makada wote wa Chama cha Umma, pamoja na Babu walihamishiwa katika gereza ovu la ulinzi wa hali ya juu la Ukonga nje ya Dar es Salaam. Kwa mara nyengine tena waliwekwa katika chumba cha wale waliohukumiwa kifo. Mazingira katika gereza la Ukonga yalikuwa ni ya kukatisha tamaa kabisa na vile alivyotendewa Babu, aliyekuwa waziri, na makomred wake, wengine wakiwa maafisa wa jeshi wa vyeo vya juu haikuwa tofauti na vile walivyotendewa wahalifu wa kawaida. Labda kama wangelikuwa wameshtakiwa kwa kuitia nchi katika umasikini basi pengine wangelitendewa vizuri zaidi na Ukonga ingelikarabatiwa na kuwekwa vyumba maalumu vya Watu Muhimu Sana, kama ilivyokuwa mwaka 2008 wakati wa matayarisho ya kesi ya waliokuwa mawaziri na watumishi wa serikali walioshtakiwa kwa uporaji wa kiasi kikubwa cha fedha (Jamiiforum, 2008).

Ilikuwa katika kipindi hiki ambapo Jumbe na Hassan Nassor Moyo, waziri wa nchi wa Zanzibar walipofika bara na kumwona Nyerere ili awaruhusu maofisa wanaosaili kutoka Zanzibar wafanye upelelezi bara. Hashil Seif aliuelezea ‘upelelezi’ huo katika mazungumzo yaliyoandaliwa katika Mkutano wa Sita wa Waarabu na Wazungu juu ya Haki za Binadamu, Berlin tarehe 12 Mei, 2011:

Nilichukuliwa kutoka katika chumba changu cha gerezani na kundi la watesaji kutoka Zanzibar. Nilizibwa macho na kufungwa pingu. Baada ya muda nilibaini kuwa sikuwa peke yangu. [Hamed Hilal naye pia alikuwa amechukuliwa kutoka katika gereza la Keko.]

Walituchukua kutoka gerezani kiasi cha saa nne usiku na kutupeleka katika nyumba iliyopo, mahali fulani Dar es Salaam ambapo ndipo wanapowatesa watu. Baada ya kuwasili walitutia katika vyumba mbalimbali.

Kuta zilikuwa zimetapakaa damu ya binadamu. Walikuwepo kiasi cha watesaji wanane. Walitumia waya za umeme, fimbo za mianzi na mipera kutupigia … Nyuso za vitisho za watesaji wetu zilinikumbusha wanyama waliojeruhiwa waliokoswa na risasi ya binadamu. Walisisitiza kuwa mimi ndiye niliyemwua makamu wa rais Karume ili kuipundua serikali halali ya ASP. (Maandishi ya mazungumzo katika Mkutano wa Sita wa Waarabu na Wazungu juu ya Haki za Binadamu, Berlin, tarehe 12 Mei, 2011)

Hashil alionyeshwa picha za waliowekwa kizuizini kutoka Zanzibar, wengi wao walikuwa wamemtaja baada ya kuteswa. Baadaye, wote wawili, yeye na Hamed walilazimishwa kutia saini maelezo ya kukiri na walipokataa mateso yalianza tena.

Mmoja baada ya mmoja, kila mtesaji alikuwa na zamu yake ya kunipiga kwa waya za umeme mpaka nilishindwa kusimama kabisa na kuanguka chini nikiwa nimezimia huku damu ikinichuruzika mwilini. Waliendelea kusema ‘utajua nini kilichomtoa kanga manyoya’. Waliyarudia maneno hayo wakati wakiendelea kunitesa, mengine mnaweza kufikiria wenyewe. Wakati wakinitesa, nilijihisi kama niliyezama ndani ya moto. Walinitaka nikae juu ya kiti, walinivua shati langu kwa hiyo nilikuwa tumbo wazi na walianza kunitesa mpaka nikapoteza fahamu na kuanguka sakafuni. (Maandishi ya mazungumzo katika Mkutano wa Sita wa Waarabu na Wazungu juu ya Haki za Binadamu, Berlin, tarehe 12 Mei, 2011)

Hashil alitishiwa kubakwa, na ijapokuwa watesaji hawakufikia hatua ya kufanya hivyo, au kumfanyia unyanyasaji wowote wa kijinsia, ubakaji wa wanaume ulikuwa ni jambo la kawaida katika mfumo wa mateso na vitisho vya serikali ya Zanzibar katika kipindi hiki na kilichofuata baadae. Kwa mfano, mwaka 2001 Napoli na Saleh wanaelezea juu ya kampeni endelevu ya kuwashambulia wanaharakati wapinzani ambapo ukatili wa kijinsia ulitumiwa dhidi ya wote wanawake na wanaume kisiwani Pemba (Napoli na Saleh, 2005: 167).

Hata hivyo, unyama wa watu waliopelekwa na serikali ya Zanzibar kumtesa Hashil ulishuhudiwa na wenzao wa bara, na hata maafisa usalama na wasaili hawa wakakamavu kutoka Dar es Salaam walishitushwa na kile walichokiona. Walimwarifu mkurugenzi wa usalama wa Taifa wa Tanzania na yeye alimpigia simu Nyerere na kumwelezea kwa urefu juu ya matukio haya akitilia mkazo kuwa kama utesaji huu haukusimamishwa waathiriwa wanaweza kufa.

Nyerere aliamrisha kuwa utesaji usimame. Akiwa amejaribu kuficha ukweIi juu ya kutiwa kwao gerezani kwa vyombo vya habari vya nchi za nje na wanadiplomasia, alitishika na uwezekano wa kumtaka aelezee juu ya vifo vya makada hawa wa kilichokuwa Chama cha Umma. Vile vile aliamrisha kuwa kuanzia wakati huo wapelelezi waliopatiwa mafunzo ndio pekee wawahoji walio kizuizini. Aliamrisha vile vile kuwa watesaji wakamatwe na waadhibiwe. Kwa hakika walitiwa ndani lakini kwa mujibu wa Hashil, ‘waliachiliwa baada ya wiki chache, wakati mimi nilirudishwa gerezani ambako nilitumia miaka sita ya maisha yangu’ (Mahojiano na Hashil Seif, 2012).

Ni wazi kuwa nia ya serikali ya Zanzibar ilikuwa ni kuwaweka watu hawa gerezani maisha. Kama Hamed alivyonambia:

Kwa muda wote huu mpaka kesi ilipomalizika hatukuambiwa sababu ya kukamatwa kwetu. Wakati Hassan Nassor Moyo alipolitembelea gereza la Dodoma akiwa waziri wa mambo ya ndani, tulimuuliza kwanini tulitiwa gerezani. Alitwambia ‘Hamjui sababu? Mtaoza hapa milele.’ (Mahojiano na Hamed, 2011)

Kuhoji kuliendelea lakini wapelelezi weledi kutoka bara hawakuweza kupata lolote la kumtia mtu hatiani. Kabla ya mauaji washtakiwa walikwenda kuvua samaki. Hapajakuwepo na silaha ndani ya mashua yao – isipokuwa chakula tu! Kila kitu kilionyesha kuwa hawakuwa na hatia lakini hilo halikuwa na umuhimu kwasababu wale waliokuwa madarakani walichodhamiria ilikuwa ni kuendesha kesi ya maonyesho ili kuwasingizia ubaya washtakiwa na kuonyesha kuwa kuanzia sasa na kuendelea, wapinzani wote watasagwasagwa kikatili.


  1. Hamed alipelekwa Tabora pamoja na Salim Saleh, Ahmed Mohamed Habibi (Tony) na Yussuf Baalawy. Kundi la Nachingwea walikuwemo Shaaban Salim, Suleiman Mohamed (Sisi), Amour Dugheish, Abdulla Juma na Haji Othman.

License

Tishio la Ukombozi Copyright © 2016 by Amrit Wilson. All Rights Reserved.

Share This Book

Feedback/Errata

Comments are closed.