2 Waingereza Wakabidhi Madaraka kwa Sultani na Washirika Wake

Waingereza, Umoja wa ZNP na ZPPP, na Michezo Michafu

 Viongozi wa vyama vya umoja mpya wa ZNP na ZPPP sasa walielemea zaidi upande wa mkono wa kulia na kuwa karibu zaidi na Sultani kuliko Chama cha ZNP kilivyowahi kufanya wakati kikiwa peke yake. Uchaguzi mwengine ulifanyika mwezi Januari 1961 na kipindi cha kabla ya uchaguzi huo kilikumbwa na kampeni kubwa za kikabila zilizoendeshwa na vyama vyote viwili vikubwa Chama cha ASP na Umoja wa ZNP na ZPPP.

Matokeo ya uchaguzi hayakuweza kutoa uamuzi wowote wa maana, wawakilishi 22 waliochaguliwa waligawika nusu kwa nusu kati ya wagombea wa kambi mbili. Kwa kuwa hakuna upande wowote uliokuwa na wingi katika Baraza la Kutunga Sheria, iliundwa serikali ya muda na uchaguzi mwengine ulifanyika mwezi Juni mwaka huo huo. Waingereza, wakiwa na shauku ya kutaka muungano wa wafuasi wa siasa za mrengo wa kulia wa ZNP na ZPPP ushinde waliunda jimbo jipya la uchaguzi la Pemba Kusini ilikuepuka uwezekano wowote wa kutokea mlingano, na matokeo yake uchaguzi uliofuata wa mwezi Juni 1961 ulitoa ushindi walioutaka. Hata hivyo, uchaguzi huo ulifuatiwa na machafuko mjini na mashamba Zanzibar, machafuko ambayo serikali ilishindwa kuyadhibiti. Kiasi cha watu 60 hadi 100 wengi wao wakiwa kutoka katika familia za Waarabu wenye kumiliki maduka ikiwa ni pamoja na wanawake wengi na watoto, walipoteza maisha na takriban 400 walijeruhiwa. Waingereza walitangaza Hali ya Hatari na kuleta majeshi kuendesha doria visiwani kwa muda wa miezi 20 iliyofuata (Lofchie, 1965: 212).

Hata hivyo, hata katika kipindi hicho, vyama havikukubaliana. Chama cha ASP kilitaka kwanza, serikali ya ndani icheleweshwe, na pili, katika kipindi hiki uchaguzi mwengine ufanyike kabla ya kutokea mabadiliko yoyote. Ilionekana kuwepo hali ya kukwama kabisa.

Hamed Hilal anakikumbuka kipindi hicho. Kipindi ambacho alikuwa anakwenda Uingereza kusoma na kwa vile hakuwa na pesa za kutosha kulipia nauli ya meli, alisafiri kwa njia ya nchi kavu. Alisafiri kupitia barani kwa kupitia Dar es Salaam, Mombasa, Nairobi, Kampala, Juba, Sudan ya Kusini, Asyut, Misri na baadae Kairo. Hapa, safari yake ya kwenda Uingereza ilikwama kwasababu Ali Sultan ambaye alikuwa akifanyakazi katika ofisi ya Chama cha ZNP Cairo alimtaka Hamed akae nyumbani kwake ili amsaidie kazi. ‘Baadaye makomred wengine waliwasili, aliniambia ‘Shaaban Salim, Ahmada Shafi na Abdalla Juma, wote walipitia njia ya mbugani. Baada ya uchaguzi wa Januari 1961 baadhi yetu tulipata mafunzo ya kijeshi kwa muda wa mwezi mmoja – hususan katika nyanja za mbinu za kufanya uharibifu.’

Shaaban aliielezea hali ya kisiasa nchini Misri wakati huo. Mapambano yaliyokuwa yakiendeshwa na Nasser yalikuwa yakiendelea na mambo mengi yalikuwa yakibadilika. Miaka michache tu kabla ya hapo (mwaka 1956) Nasser aliitaifisha Kampuni ya Mfereji wa Suez na mapambano ya kupinga ubeberu yalikuwa yakiendelea nchi nzima. Serikali ya Misri ilikuwa ikigawa upya ardhi na kuandaa mipango ya ujenzi wa viwanda.

Baada ya muda mfupi wa mafunzo ya kijeshi, Shaaban anakumbuka jinsi Ali Sultan alivyowaambia. “Badala ya kwenda Ulaya kuna masomo mengine muhimu zaidi huko Zanzibar!” na walirudi visiwani.

Kulikuwa na michezo michafu mingi iliyokuwa ikiendelea baada ya uchaguzi wa mwaka 1961. Kwa mfano, ijapokuwa ilikubaliwa kuwa baada ya uchaguzi ilikuwa turudi Misri ili kumaliza mafunzo yetu, Ali Muhsin alipinga. Aliwapeleka watu wake mwenyewe waliokubaliana na siasa zake za mrengo wa kulia na ambao aliwadhibiti. Baadae Ali Sultani aliwasiliana na Wacuba na walikubali kutupatia mafunzo nchini Cuba. Tulikwenda Cuba lakini wakati tukiwa huko, Babu alikamatwa kwa kufanya uchochezi, alihukumiwa kwenda jela kwa muda wa miezi 18 na kupigwa faini ya pesa nyingi sana. Baadhi yetu, vijana makada, pia tulishtakiwa kwa ‘kuleta makala za uchochezi’ na kadhalika. Ali Muhsin alijaribu kutuzuia tusifanye kampeni ya kudai Babu aachiliwe. Alisema kuwa hakujakuwa na haja ya kufanya hivyo. Lakini tulifanya kampeni kubwa. (Mahojiano na Shaaban, 2009)

Kukamatwa kwa Babu mapema mwezi Januari 1962 zilikuwa ni juhudi za dhahiri za kuudhoofisha mrengo wa kushoto kama kundi lililojiandaa. Vijana wa ZNP ambao walikamatwa pamoja na Babu, baadae waliachiwa lakini Babu alibakia ndani.

Waingereza na muungano wa ZNP na ZPPP walikula njama za kuwadhalilisha na kuwashambulia wafuasi wa siasa za mrengo wa kushoto. Ali Sultani ambaye aliwakosoa waziwazi Ali Muhsin na Shamte, alifukuzwa kutoka katika Chama cha ZNP, na Shamte alijaribu bila ya mafanikio kutaka afukuzwe pia kutoka katika FPTU. Kama Khamis anavyokumbuka, ulikuwa ni wakati wa kila aina ya michezo michafu. Katika tukio moja muhimu ambalo lilielezwa na Ali Sultan (Burgess, 2009: 79), furushi la makaratasi lilirushwa kwenye kitanda chake kwa kupitia kwenye dirisha la nyumba yake lililokuwa wazi. Zilikuwa ni barua ambazo eti zilitiwa saini na yeye na zilizokuwa zipelekwe kwa mtoto wa Sultani, kwa Ali Muhsin, kwa Shamte na kwa Karume akiwa kiongozi wa upinzani. Barua hizo zilieleza kuwa Ali Sultani na kundi lake la Makomred watawaua.

Ali Sultan, kwa haraka alikimbilia kwenye ofisi ya FPTU na kuwaonyesha barua hizo Badawi na Khamis waliokuwa wakifanyakazi hapo. Walimwambia azichome moto haraka. Hata wakati barua hizo zikiwa jivu, zilipatikana habari kuwa polisi wameizunguka nyumba yake na wamo katika harakati za kutaka kuipekua.

Kipi Kinachomfanya Mtu awe na Kosa la Kufanya Uchochezi?

Kesi ya Babu iliyopelekea afungwe miezi 18 ni wazi kabisa kuwa ilikuwa ni kesi kubwa katika mahakama na ilisababisha kuwepo kwa rundo la maandiko na simu za siri za upepo za Waingereza.

Kiserikali, shitaka la uchochezi lilifunguliwa kwasababu zilizokuwa dhaifu sana. Kwa maneno ya waraka mmoja wa Waingereza (Ofisi ya Nyaraka za Serikali 1962b) juu ya kesi ya uchochezi ya Babu : ‘ Abdulrahman Mohamed Babu anashtakiwa kwa uchochezi kufuatia maelezo yaliyotokea katika ZaNews siku ya tarehe 29 Desemba kuwa machafuko yaliandaliwa kabla na kupangwa na Chama cha ASP kwa ruhusa ya serikali ya “kikoloni” ’. Kwa kuwa maelezo haya yasingeliweza kuchukuliwa kuwa ni tishio kwa serikali, sababu hasa za kukamatwa kwake ni tofauti kabisa. Vyombo vya ujasusi vya Uingereza vimekuwa vikimmurika tokea siku za nyuma wakati alipokuwa Uingereza. Kwa mfano, Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza, ilieleza tarehe 23 Februari, 1962:

Muhusika ana historia ndefu ya harakati za kikomunisti kuanzia mwaka 1951 …inaaminiwa kuwa ni mwanachama wa Chama cha Kikomunisti cha Uingereza na … Amekuwa akitoa mihadhara katika chuo chao huko Hastings juu ya ‘Matatizo ya Ubeberu’ … Kwa haraka amejenga mahusiano na WFTU na vyama vyengine vya Kikomunisti … Amekuwa mwandishi mkuu wa Afrika ya Mashariki wa Shirika la Habari la China, mhariri wa ZaNews, gazeti la uchochezi lililopendelea Ukomunisti kwa nguvu zote na muhimu zaidi Katibu Mkuu wa Chama cha ZNP … Amekuwa mstari wa mbele katika kuianzisha ofisi ya Kairo ya Chama cha ZNP ikiwa ndiyo kituo cha kupitia wanafunzi wanaosafiri kwenda kwenye nchi zilizo nyuma ya pazia la chuma … muhusika alihudhuria mkutano wa kupinga bomu la atomic nchini Japan mwezi Julai 1961, na kuunga mkono kwa nguvu zake zote azimio lililotaka kuwa hapana nchi yoyote katika nchi zilizohudhuria mkutano huo itakayoruhusu kuwepo balozi za Marekani au vituo vyake vya kijeshi katika nchi zao. Mara baada ya kurejea lilifanywa jaribio lisilofanikiwa la kuchoma moto ubalozi wa Marekani wa Zanzibar. (Ofisi ya Nyaraka za Serikali, 1962b)

(Jaribio hilo lisilofanikiwa’ lilikuwa ni tendo la hujuma isiyofanikiwa ya kufanya uharibifu la baadhi ya vijana wa Chama cha ZNP ambao walihusika vile vile na kikundi kidogo kilichojitegemea au pia kikundi cha muda tu cha kundi linalopinga ubeberu lililoitwa Kikundi cha Wanaharakati cha Zanzibar.)

Waraka huo huo pia umeeleza kuwa: ‘Muhusika ana wafuasi wengi miongoni mwa vijana wa chama cha ZNP na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi la Federation of Progressive Trade Unions linalokiunga mkono Chama cha ZNP na inajulikana kuwa na uhusiano wa siri na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi la Zanzibar and Pemba Federation of Labour linalokiunga mkono Chama cha ASP.

Babu alifanya mpango na mwanasheria mwenye siasa kali Ralph Milner ili amtetee lakini Waingereza walimzuia Milner asiingie Zanzibar. Waziri wa Nchi Mwenye kushughulikia Makoloni alieleza katika simu ya upepo aliyomtumia Kaimu Balozi wa Uingereza, ‘habari za kuaminika zilizopatikana hapa zinaonyesha kuwa bado Milner ni mwanachama aliye katika harakati za Chama cha Kikomunisti’ (Ofisi ya Nyaraka za Serikali, 1962b).

Kanti Kotecha aliyekuwa mwendesha mashitaka wa serikali katika Mahakama ya Rufaa, aliniambia katika mahojiano mwezi Novemba 2010 kuwa kesi ya Babu kwanza iliendeshwa katika Mahakama Kuu ya Zanzibar ambapo hapakuwepo na jopo la watu waliochaguliwa kusikiliza kesi na kutoa ushauri kwa hakim bila ya kupendelea Mahakamani. Aliendelea:

Hapa ndipo Babu alipoonekana kuwa ana hatia na kuhukumiwa kwenda jela kwa miezi tisa. Baadaye kesi hiyo ilikatiwa rufaa katika Mahakama ya Rufaa ya Afrika ya Mashariki. Babu alimwajiri mwanasheria mashuhuri, O’Donovan kutoka London [ambaye labda alikuwa ni mbadala wa Milner] ili amwakilishe katika rufaa yake. Niliiwakilisha serial. … Sikuwa na shaka yoyote akilini mwangu kuwa alikuwa na hatia kwa mujibu wa sheria. Bila shaka, sheria za uchochezi za zama hizo ziliipendelea sana serikali. Nadhani mambo yamebaki hivyo hivyo chini ya serikali huru. Majaji wote watatu katika Mahakama ya Rufaa walikuwa Waingereza. Wote walikuwa na kauli moja katika uamuzi wao. Hapajakuwepo na maoni tofauti.

Akielezea mtazamo wake mwenyewe, Kotecha aliongeza:

Kosa ambalo watafiti wengi wanalifanya ni kushughulika na Babu tu na kushindwa kuelewa umuhimu wa jumla wa kujipenyeza kwa ukomunisti na mafunzo waliokuwa wakipatiwa Wazanzibari katika itikadi ya kikomunisti huko Cuba, Ujarumani ya Mashariki, Nchi ya Umoja wa Kisovieti na China. Baada ya kurudi, makomred hawa walisababisha harakati za amani na zisizokuwa za kimapinduzi katika mchakato wa kisiasa pamoja na utawala bora zisiwezekane. Badala ya kujaribu kuwashtaki mmoja mmoja, bora serikali ingelitangaza hali ya hatari na kuwatenga kwa kipindi cha miaka fulani wote wale ambao hawakuwa tayari kuendelea na kufuata njia ya amani na ya kidemokrasia kuelekea uhuru kamili. Hata hivyo, kufikia hapo Waingereza (hasa Waziri aliyehusika na makoloni [Ian] Macleod) walitaka kunawa mikono yao, wawape Wazanzibari uhuru, na waondoke.

Mkutano wa Katiba katika Nyumba ya Lancaster

Mwisho wa mwezi Machi 1962 uliandaliwa Mkutano wa Katiba katika Nyumba ya Lancaster. Babu aliruhusiwa kuhudhuria mkutano huo kwa dhamana akiwa msikilizaji tu. Wakati wa mkutano huo Babu alipata habari kuwa Waingereza waliuambia uongozi wa wafuasi wa siasa za mrengo wa kulia wa vyama vya ZNP na ZPPP kuwa vyama hivyo havitakabidhiwa madaraka kama hawataepukana na wafuasi wa siasa za mrengo wa kushoto na kuwa Muhsin na Shamte walikubali kushirikiana na wakoloni juu ya hilo.

Wakiwa na shauku ya kukabidhi madaraka ya serikali na labda wakiwa na hakika ya kuwepo kwa serikali ambayo haitakuwa na wafuasi wa siasa za mrengo wa kushoto ndani yake, Waingereza walipendekeza kuwepo kwa serikali ya mseto. Hata hivyo, muungano wa Vyama vya ZNP na ZPPP haukuwa tayari kukipa Chama cha ASP zaidi ya nafasi tatu za uwaziri kati ya nafasi tisa wakati Chama cha ASP kilitaka uwepo uwakilishi ulio sawa na kiliendelea kudai kuwepo kwa uchaguzi kabla ya uhuru.

Palikuwepo vile vile tofauti muhimu kadha kuhusu sera ya serikali kati ya pande mbili hizo kuhusu suala kama vile mgawanyo wa ardhi na mgawanyo wa nafasi za kazi serikalini kati ya makabila. Hotuba ya Othman Sharif kwa niaba ya Chama cha ASP siku ya kwanza ya mkutano ilieleza kuhusu tofauti hizi.

Kiuchumi, kijamii na kisiasa mgawanyo hauna uwiano na idadi ya watu ilivyo. … asilimia 80% ya ardhi yenye rutuba na sehemu kubwa ya biashara na viwanda vimo mikononi mwa watu wachache na takriban nafasi zote muhimu za kazi za kiutawala wanazishikilia wao. Hali hii inahitaji kurekebishwa na kufanyiwa mabadiliko. (Imenukuliwa kutoka kwa Lofchie, 1965: 215)

Alidai kwa nguvu zake zote kuwepo kwa mpango madhubuti wa marekebisho ya umiliki wa ardhi miongoni mwa mabadiliko mengine. Msimamo huu wa kutaka marekebisho ya umiliki wa ardhi ndio msimamo ambao kwa muda mrefu ulikigawa Chama cha ASP, huku wa mrengo wa kulia wakiongozwa na Karume wakipinga marekebisho hayo – labda hii ikionyesha nafasi yake ya kitabaka zaidi kuliko kitu chengine chochote kile. Ama kwa Chama cha ZNP, wanaopenda maendeleo ndani ya chama hicho walipendelea kuwepo kwa marekebisho hayo lakini hawakuweza kuchukua msimamo wowote kuhusu hili. Matokeo yake ni kuwa muungano wa ZNP na ZPPP ulijitokeza waziwazi kupinga marekebisho ya umiliki wa ardhi.

Babu akiwasili katika sherehe za kusherehekea kuachiwa kwake kutoka gerezani tarehe 29 April, 1963. Qullatein Badawi yupo mkono wa kulia mkabala na kamera.
Babu akiwasili katika sherehe za kusherehekea kuachiwa kwake kutoka gerezani tarehe 29 April, 1963. Qullatein Badawi yupo mkono wa kulia mkabala na kamera. Chanzo: Mohamed Amin/Camerapix

Khamis alikikumbuka kipindi hicho:

Palikuwepo na mgawanyiko uliokuwa wazi kati ya mawazo yetu na mawazo ya viongozi wa Chama cha ZNP juu ya suala la marekebisho ya umiliki wa ardhi, lakini haikuwezekana kwa wakati huo kuchukua msimamo. Mgawanyo mpya wa ardhi ni sehemu ya usoshalisti na kwa hivyo sisi tuliutaka, lakini tulijua kuwa tungeliupendekeza wakati huo, tusingelifanikiwa kwasababu wakati huo chama kilitawaliwa na mabwanashamba. Mwanzoni [siku za awali za ZNP] mabwanashamba walikuwa wachache ndani ya chama lakini wakati huu Ali Muhsin alikuwa akiwaingiza mabwana shamba wengi na watu wengine kwasababu za kikabila tu, Waarabu waliohusiana nae na kadhalika. (Mahojiano na Khamis Ameir, 2009)

Mkutano ndani ya Nyumba ya Lancaster ulikwama. Hatimaye, mwezi Machi 1963, Duncan Sandys, Waziri wa Nchi wa Uingereza anayeshughulikia Makoloni, aliitembelea Zanzibar na kushurutisha kuwepo kwa mpango wa usuluhishi ambapo uhuru wa ndani ungelitolewa mwisho wa mwezi Juni na baada ya wiki mbili kufuatiwa na uchaguzi mkuu.

Kundi kubwa la watu likisubiri kwa hamu kumkaribisha Babu mbele ya makao makuu ya Chama cha ZNP, Darajani mkabala na jengo la Bharmal.
Kundi kubwa la watu likisubiri kwa hamu kumkaribisha Babu mbele ya makao makuu ya Chama cha ZNP, Darajani mkabala na jengo la Bharmal. © Bettmann/CORBIS

Chama cha Kimapinduzi chaanzishwa

Kuachiwa kwa Babu na kushangiriwa kwake kwa makaribisho makubwa tarehe 29 April, 1963 kulichochea upya hamasa za wanachama wa YOU pamoja na watu wengine waliokuwa wakitaka maendeleo visiwani Zanzibar. Wafuasi wa siasa za mrengo wa kushoto walianza kukabiliana na wafuasi wa siasa za mrengo wa kulia wa Chama cha ZNP kwa nguvu zaidi kuhusu masuala mbalimbali. Wakati wa kuelekea kwenye uchaguzi wa Julai 1963, walidai kuwa chama kirudi katika msimamo wake wa awali wa kupinga ubeberu. Halikadhalika, ijapokuwa ulikuwepo ushirikiano wa kiuchaguzi na Chama cha ZPPP, Chama cha ZNP kijitenge na msimamo wa kisiasa wa Chama cha ZPPP wenye kuunga mkono ubeberu na kuwapinga Wabara na kitoe ilani yake ya uchaguzi itakayoweka wazi msimamo wake juu ya suala la ardhi, jukumu la tabaka la wafanyakazi na vipaumbele vya kiuchumi vya serikali mpya. Na la mwisho, lakini si la mwisho kwa umuhimu wake, ili kuonyesha kuwa Chama kimerudi katika msimamo wake wa awali, chama kiteue wagombea wenye kutaka maendeleo ili kugombea katika majimbo yaliyo salama badala ya kutumia ukabila kuwa ni kigezo cha kupendekeza wagombea (kwa kusimamisha wagombea Waarabu katika majimbo yenye Waarabu wengi na wagombea Waafrika katika majimbo yenye Waafrika wengi). Walidai kuwa ukabila usiwe ndiyo kigezo cha kutoa maamuzi juu ya nani agombee wapi na ni kwa kusimamisha wagombea wenye kutaka maendeleo ambao watakuwa ni wa makabila tofauti na watu wa majimbo wanayogombea tu ndipo Chama cha ZNP kitakapoweza kujiita kuwa ni chama cha mchanganyiko wa watu wa makabila mbalimbali.

Wafuasi wa siasa za mrengo wa kulia ndani ya Chama cha ZNP walizikataa hoja hizi. Maoni yao yalikuwa ni kwamba umoja kati ya vyama vya ZNP na ZPPP unapaswa kufurahiwa, na serikali ya muungano ya vyama viwili hivyo itakuwa na ‘Wazanzibari halisi wote’ na kusababisha kuporomoka kwa Chama cha ASP.

Hatimaye, mnamo mwezi Juni, katika mkutano mkuu wa chama wa kabla ya uchaguzi ambao viongozi walikuwa wapate idhini ya kushiriki katika Mkutano ufuatao wa Katiba katika Jengo la Lancaster, wafuasi wa siasa za mrengo wa kushoto walijiuzulu kwa wingi. Siku ya pili tu chama kipya cha kimapinduzi, Chama cha Umma Party, kilianzishwa.

Matokeo yake yalikuwa ya kuvutia. Vijana, hasa wa kutoka katika matabaka ya wafanyakazi na wakulima na wa kutoka katika vyama vyote vya kisiasa na makabila mbalimbali waliingia katika harakati. Mkutano wa hadhara wa kwanza wa chama hicho uliofanyika siku ya pili baada ya chama hicho kuundwa ulivutia maelfu ya watu. Athari yake ya kisiasa ilikuwa kubwa na katika kipindi cha chini ya wiki moja kiliwavutia mamia ya wanachama wapya kutoka katika matabaka na makabila yote. Kwa upande mmoja kiliwazindua watu kuhusu ukweli wa mambo yalivyo siku chache kabla ya uhuru – kuwa makundi ambayo hapo awali yalishirikiana na wakoloni sasa yamekuwa ndani ya vyama vikuu vya siasa yakijaribu kuuteka nyara uhuru na kuirudisha nchi nyuma katika ukoloni mambo leo. Kwa upande mwengine kilileta matumaini na mtazamo mpya kwa kuwafanya watu waelewe kuwa siku za usoni zinaweza kuwa ni tofauti – kuwa kwa ushiriki wao Zanzibar inaweza kuzuiliwa isifuate njia ya ukoloni mambo leo na badala yake kuwa taifa huru la kisoshalisti.

Katika miezi michache iliyofuata, Chama cha Umma Party kilianza kupanua wigo wake. Programu yake ilikiweka chama hicho katika hali ya uongozi wenye uelewa wa watu wenye kukandamizwa wa Zanzibar. Aydhan kikiwakilisha maslahi mapana ya Waafrika waliokuwa wanakandamizwa kiuchumi kutokana na ukoloni wa kigeni na mamwinyi wa ndani ya nchi na kupambana na ukandamizaji wa mabeberu kwa madhumuni ya kuleta usoshalisti Zanzibar (angalia kiambatisho 1). Madhumuni yake yalikuwa ni pamoja na kuleta ‘umoja wa watu wote wa Zanzibar na umoja wa watu wa Afrika ya Mashariki na wa Afrika nzima kwa misingi ya Umajumui wa Afrika.

Chama hicho kiliwavutia wanachama wa FPTU, wengi wao wakiwa wamekiacha Chama cha ZNP na kujiunga na Chama cha Umma, huku wakiiacha serikali ya muungano wa vyama vya ZNP na ZPPP bila ya vyama vya wafanyakazi vyenye kuiunga mkono. Kilijenga pia uhusiano wa karibu na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi la ZPFL lililojiunga na Chama cha ASP. Kama Lofchie alivyoeleza:

Wanachama na viongozi wa ZPFL wengi wao walikuwa ni Waafrika kutoka Bara na kisiasa walikiunga mkono moja kwa moja Chama cha ASP. Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi la FPTU …… hapo awali lilionyesha msimamo wa kuwa na chuki na Waafrika kutoka Bara kama kilivyokuwa Chama cha ZNP lakini baada ya kuondolewa kikwazo hiki mtazamo wa kiitikadi wa namna moja ulianza kuyaleta pamoja mashirikisho mawili haya. (Lofchie, 1965: 261)

Khamis, Katibu Mkuu wa Shirikisho la FPTU alithibitisha hili. “Chama cha Umma Party kilikuwa ni chama kidogo lakini kiliungwa mkono na vyama vya wafanyakazi, siyo na FPTU tu lakini pia na wafanyakazi kutoka Shirikisho jengine la vyama vya wafanyakazi la ZPFL ijapokuwa shirikisho hili lilikiunga mkono Chama cha ASP.” (Mahojiano na Khamis Ameir, 2009)

Wakati akiendelea kuuita muungano wa vyama vya ZNP na ZPPP kuwa ni wa ‘siasa za wastani’, Lofchie alivutiwa, hata bila ya yeye mwenyewe kupenda, na Chama cha Umma Party ambacho alisema, kilijumuisha katika shughuli zake Wazanzibari kadha waliokuwa na uwezo mkubwa wa kuongoza na kilikuwa na nidhamu ya ‘hali ya juu na kilisukwa vizuri. Kilifuata itikadi unganishi madhubuti ya Kimarx na kupata utiifu mkubwa kwa wafuasi wengi’ (Lofchie, 1965: 262). Ijapokuwa inaonekana kuwa alisahau kumtaja Babu katika kurasa 258 za kwanza za kitabu chake cha kurasa 281, baadae Lofchie alieleza kuwa:

Babu…. Alitambuliwa dunia nzima kuwa ni kiongozi gwiji wa siasa za Zanzibar, na katika kipindi kifupi alikiweka chama cha Umma mbele ya takriban makundi yote ya upinzani yaliyokuwa katika mapambano…. na kuwa na uhusiano madhubuti wa kufanyakazi pamoja na vyama vikubwa vya wafanyakazi, vyombo vya habari na hata na wanachama wengi waliokuwa na ushawishi wa ASP. (Lofchie, 1965: 258)

Hatimaye, tarehe 10, Disemba 1963 Uingereza iliipa rasmi Zanzibar uhuru. Sultani alikuwa ndiye Mkuu wa Nchi akiwa na madaraka ya kumteua mrithi wake, huu ukiwa ndiyo mfumo walioutaka ili waweze kuendelea kuvidhibiti Visiwa vya Zanzibar.

Sasa, ukandamizaji ulizidi kwa kiwango kikubwa. Safari za kwenda Bara au Ulaya zilizuiliwa, upekuzi wa majumba na ukamataji wa watu yalikuwa ni mambo ya kawaida, na Ali Muhsin, Waziri wa Mambo ya Ndani, alijipa madaraka makubwa ya ukandamizaji. Miswada miwili ya sheria ilitangazwa, miswada ambayo ingeliipa uwezo serikali kukipiga marufuku chama chochote cha siasa na kulipiga marufuku gazeti lolote ambalo ingeliona kuwa ni la hatari.

Chama cha Umma Party, kikielewa kuwa ndicho kitakacholengwa na sheria hizi, kiliunda umoja wa kimkakati na ASP, chama rasmi cha upinzani na wakati huo huo kikaunda chama cha Wanahabari, The Zanzibar Journalist Organisation ambacho kiliyaunganisha magazeti ya upinzani – siyo ZaNews na Sauti ya Umma tu lakini pia Afrika Kwetu, gazeti lililokuwa likikiunga mkono chama cha ASP, Jamhuri ambalo lilikuwa likitolewa na kiongozi wa zamani wa ZPPP ambaye alijiunga na ASP, na majarida na magazeti mengine kadha. Kwa kupitia magazeti haya Chama cha Umma kiliwaandaa wananchi nje ya Baraza la Kutunga Sheria na kufanya kampeni dhidi ya sheria mpya zinazopendekezwa.

Hata hivyo, juu ya upinzani mkali, serikali ilifanikiwa kuzipitisha sheria hizo. Wakati huo huo iliamua kulifanyia mabadiliko jeshi la polisi kwasababu tu idadi kubwa ya askari wa jeshi hilo walikuwa kutoka Bara na kwa hivyo watawala wa ZNP-ZPPP kuwaona kuwa ‘hawaaminiki’. Maafisa wa vyeo vya juu wa polisi, na askari polisi wa kawaida ambao waliajiriwa na Waingereza kutoka Tanganyika, Kenya na Nyasaland (Malawi), wote walipoteza kazi zao bila ya fidia. Haikuwa jambo la kushangaza kuwa walishikwa na hasira na uchungu. Wengi wao waliachishwa kazi bila ya kurudishwa makwao, na kundi hili, ambalo lilipata mafunzo ya kutumia silaha lilibaki Zanzibar.

Haki na demokrasia ambayo watu waliipigania wakati wa mapambano dhidi ya ukoloni ilipotea. Tarehe 6 Januari 1964 chama cha Umma Party kilipigwa marufuku kama ilivyotegemewa, gazeti lake la kila siku nalo lilipigwa marufuku na mali zake kuchukuliwa. Mara baada ya hapo, polisi walizivamia nyumba za viongozi wake. Nyumbani kwa Babu, baada ya kushindwa kupata kitu chochote cha hatari walifukua bastola ya zamani isiyoweza kutumika, labda ukumbusho wa afisa wa zamani wa kikoloni alieishi ndani humo zamani. Upatikanaji huu wa bastola uliandikwa na polisi kama idhibati yao.

Siku ya pili, washabiki wa Chama cha Umma Party waliokuwemo katika jeshi la polisi walimuonya Babu kuwa angelishtakiwa kwa kosa la uhaini – kosa ambalo adhabu yake ni kifo – na walimtaka aondoke Zanzibar. Babu aliamua kutorokea Dar es Salaam, ilikuepuka kukamatwa na kujaribu kutafuta mwanasheria ambaye angelimtetea kama angelishtakiwa. Ilikuwa ni safari ya kihistoria iliyofanyika kwa ngarawa na ambayo imekuwa ni hekaya ya Zanzibar— ikielezewa katika daraja tofauti na ufasaha. Safari hii iliwezekana kwasababu Badawi aliweza kuipata ngarawa kwa msaada wa Saleh Sadallah na Abdulaziz Twala, wanachama wapenda maendeleo wa ASP.

Baadaye, yeye na Babu walisafiri hadi Fumba, kijiji cha wavuvi kusini-magharibi ya Zanzibar ambako ngarawa ilikuwa ikisubiri na kutoka hapo Babu akifuatana na Ali Mahfoudh walisafiri na kuvuka bahari hadi Dar es Salaam.

Palikuwa na wasiwasi mkubwa na minong’ono ilianza kusambaa kuwa baadhi ya wanachama wa Umoja wa Vijana wa ASP na wahuni fulani walipanga kuuchoma moto mji wa Zanzibar mnamo siku chache zijazo. Mapinduzi ya Zanzibar yalikuwa yakinukia.

License

Tishio la Ukombozi Copyright © 2016 by Amrit Wilson. All Rights Reserved.

Share This Book

Feedback/Errata

Comments are closed.