Shukrani

Ingawa ni mimi niliekiandika Kitabu hiki lakini kwa sehemu kubwa sana kinatokana na juhudi za pamoja zilizozaliwa kutokana na fikra na tafkari za pamoja kupitia kwa Makomredi wenzangu, Khamis Ameir, Shaaban Salim na Hamed Hilal, ambao wote walikuwa ni makada wa Chama cha Umma Party. Sio tu walitowa maelezo juu ya harakati zao zilizopita lakini pia walichangia katika kukusanya nyaraka na picha pamoja na kutoa ufafanuzi wa matukio mbalimbali. Kwa hivyo ni kitabu chetu kwa pamoja, ni chao kama kilivyokuwa ni changu. Juu ya hivyo ni mimi peke yangu ninaechukuwa jukumu la makosa yoyote yatakayoweza kujitokeza katika kitabu hiki.

Ningelipenda pia kuchukuwa fursa hii kumkumbuka na kumuenzi Komredi wetu mpenzi Marehemu Qullatein Badawi, aliyetushajiisha na kutusaidia katika juhudi zetu za kukitafiti kitabu hiki. Ninamshukuru Hashil Seif Hashil ambae pia alikuwa ni kada wa Chama cha Umma Party kwa kunipa maelezo kuhusu harakati zake za kisiasa.

Katika kipindi nilichokuwa nikiandika kitabu hiki, Narendra Gajjar ndiye mtu aliekuwa nikiwasiliana nae sana. Kila mara akihakikisha kuwa tayari kunijibu maswali yangu kwa njia ya simu au barua-pepe, na bila ya kusita kunipatia mawasiliano na watu mbali mbali, nyaraka za kuvutia na fikra juu ya njia za kufanya kuweza kupata majibu ya masuala magumu na/au yaliyokuwa na utata.

Miongoni mwa wengine wengi walionisaidia ningelipenda kutowa shukurani zangu kwa Mohamed Saleh na Salma Maoulidii kwa kunipatia maandishi na machapisho yao, Mailys Chauvin kwa kunisaidia katika kuhakiki maelezo mbali mbali wakati alipokuwa Zanzibar pamoja na kuniruhusu kutumia picha yake ya Khamis, Badawi na Hashil iliyochukuliwa katika mwaka 2012. Ninamshukuru pia Firoze Manji kwa kunipa moyo katika kipindi ambacho sikuwa na uhakika kama mswaada wangu ungeliweza siku moja kuchapishwa na kuwa kitabu.

Shukrani zangu pia kwa wachapishaji wa Pluto Press na hususan Anne Beech kwa msaada wake na usahihishaji wake makini na wa kina.

Kwa tafsiri hii ya Kiswahili, shukrani zangu za kipekee za dhati ya moyo wangu ziwaendee Ahmada Shafi Adam aliyefanya kazi nzuri ya kukitafsiri kitabu, na Mohamed Saleh aliekihariri, pamoja na Mansab Abubakar, Firoze Manji, na Ludovick Mwijage waliowezesha uchapishaji wake.

Hatimae, ningelipenda kuishukuru aila yangu kwa kusoma na kudadisi sura mbali mbali za mswaada zinazofuata – bila ya shauku yao na kunipa moyo kwao kitabu hiki kamwe kisingeliweza kukamilika.

Amrit Wilson

 

License

Tishio la Ukombozi Copyright © 2016 by Amrit Wilson. All Rights Reserved.

Share This Book

Feedback/Errata

Comments are closed.