Utangulizi

Ni mahali pa ‘vituko vilivyoandaliwa vyema’, na safari za kuchunguza mazingira, ‘ni pepo ambayo jina lake tu huleta dhana ya kula njama; hivi ndivyo Zanzibar inavyoelezwa siku hizi. Kwa kiasi kikubwa, katika kipindi cha mwongo uliopita wa miaka ya 2000, Visiwani, kama visiwa viwili vya Zanzibar (Unguja na Pemba) vinavyoitwa, vimeuzwa ili kuwa kiwanja cha michezo kwa watalii kutoka nchi za magharibi. Hapa ndipo mahali ambapo tunatakiwa tuamini, kuwa panaanza na kumalizika kwa yale tuyaonayo leo, bila ya kuwa na yaliyopita ambayo yalikuwa na umuhimu wowote wa kisiasa au mustakabali wenye tofauti yoyote na yale ya hivi sasa. Hata historia yake inapatikana kama vidonge vya dawa vilivyofungashwa vizuri kwa matumizi ya watalii.

Lakini kama zilivyo ‘pepo’ nyingi za aina hiyo, kwa watu wanaoishi humo ukweli uko tofauti kabisa. Kwao, mambo kadha ya zamani ambayo bado yamo katika kumbukumbu zao yanaendelea kujitokeza tena hivi sasa.  Ndani ya chombo kinachowasafirisha watu baharini kutoka Dar es salaam kwenda Unguja na kurudi, kikundi cha vijana wanabishana kwa jazba juu ya mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 na yaliyotokea baada ya hapo, juu ya athari za muungano wa Zanzibar na Tanganyika uliofuatiwa na kuundwa kwa Tanzania, na michango ya Julius Nyerere, Abdulrahman Mohamed Babu na Abeid Karume. Katika magazeti yanayotolewa kila siku, matukio ya miaka ya 1960 na 1970 yanaendelea kuzusha mijadala mikali. Machungu ya wale waliowapoteza watu wao wanaowapenda na hasa njia za kuendeshea maisha yao katika kipindi kilichoshuhudia mabadiliiko hayo na matokeo ya kusikitisha yaliyofuatia mapinduzi hayo yanajitokeza katika maoni mbalimbali, majadiliano, kumbukumbu na mitandao ya kijamii. Na mikahawani, wale wasiopendelea chama chochote, ikiwa Chama cha Mapinduzi (CCM) au Chama cha Wananchi (CUF) hufanya utani juu ya “Serikali ya Umoja wa Kitaifa” iliyoanzishwa kwa shinikizo kutoka nchi za magharibi ambayo hivi sasa ina umri wa miaka minne na tayari imeanza kufanya nyufa. Watu hao husema kuwa, maafa yanarudiwa yakiwa mithili ya kichekesho. Wakati huo huo, kila mtu anaelewa juu ya kuwepo kwa jeshi la Marekani nchini. Wanafungua skuli, wanatoa tunzo na kujiimarisha visiwani, kwasababu, kama zilivyofichua nyaraka za siri zilizotolewa na Wikileaks ambazo zinaeleza kuwa, sasa, kama ilivyokuwa wakati wa mapinduzi ya 1964 na vita baridi, Zanzibar, kwa mara nyengine tena inaonekana kuwa ni kipande muhimu cha mchezo wa dama unaochezwa na Marekani kupitia sera zake za nchi za nje na za kijeshi katika Bara la Afrika.

Uingiliaji wa Marekani katika mambo ya ndani ya Zanzibar baada ya mapinduzi una vitu vingi vinavyofanana na uingiliaji wa hivi karibuni kabisa wa Marekani katika Bara la Afrika. Kusema kweli, mambo mengi ya mtindo uliobuniwa wakati wa vita baridi bado yanaendelea kutumika hadi hivi leo. Kama ilivyokuwa wakati wa machafuko ya Libya, nchini Zanzibar vile vile Marekani ilifanya kila juhudi ili ionekane kama kwamba ni ‘matakwa ya Afrika’. Lakini wakati NATO iliingilia kati na kuivamia Libya kupigana na majeshi ya Gaddafi, Visiwani Zanzibar Marekani iliisukuma Uingereza kuingilia kati na kuandaa Mpango wa Utekelezaji wa Zanzibar ambao ungeliwawezesha kuwashawishi kwa kuwatumilia akili wale viongozi inaoweza kuwachezea ili waiombe Uingereza iingilie kati kijeshi.

Kwa nini uingiliaji kati huo haukutokea wakati wa, au mara tu baada ya machafuko ya Zanzibar? Kwa kiwango fulani, ilikuwa ni kwasababu ya kuwepo kwa chama cha kimapinduzi kilichoandaliwa vizuri kabisa, chama cha Umma Party. Ijapokuwa chama hiki sicho kilichoyaanzisha mapinduzi ya Zanzibar, chama cha Umma Party kiliyageuza mapinduzi ya Zanzibar kutoka kuwa maasi ya kihuni na kuwa upinzani wa kimapinduzi, na kuchukua madaraka ya dola na kuyadhibiti mnamo saa chache. Ama kuhusu umbile la mapinduzi yenyewe, kwa kila hali yalikuwa ni ya kwanza ya aina yake katika Afrika ya leo. Wakati nchi za Afrika, isipokuwa Kenya na Algeria, zilipata uhuru kwa njia ya majadiliano (visiwani Zanzibar, Waingereza walimkabisdhi madaraka Sultani) mapinduzi ya Zanzibar yalikuwa ndiyo ya kwanza kuupindua utawala wa serikali ya ukoloni mambo leo. Hapa, kama alivyoandika kiongozi wa Chama cha Umma Party, Abdulrahman Mohamed Babu, watu walikuja juu siyo kwasababu ya “kuipindua serikali iliyofilisika kisiasa na mfalme wa kikaragosi tu bali pia walifanya mapinduzi ili kuubadilisha mfumo wa kijamii ambao uliwakandamiza na kwa mara ya kwanza kuchukua majaaliwa ya historia yao katika mikono yao wenyewe” (Babu, 1989: 3).

Kurasa zinazofuata zinaelezea njia iliyofuatwa na chama cha Umma Party na makada wake, kwa kutumia ushahidi wa picha za kihistoria, mahojiano, na zile zilizokuwa nyaraka za siri za Marekani na Uingereza. Tunachunguza juu ya namna gani chama kiliibuka kutoka katika wimbi la maandalizi ya kupambana na ukoloni ili kukabiliana na watawala waliokabidhiwa madaraka na Uingereza wakati wa uhuru, na namna gani kilipanga mikakati ya kujenga umoja katika Zanzibar iliyokuwa imegawika kikabila (Angalia Sura ya 1 kwa mjadala juu ya ukabila na matabaka Zanzibar).

Kwa kuangalia uzoefu wa makada wa chama cha Umma, wengi wao wakiwa wamepatiwa mafunzo Cuba na Misri iliyoongozwa na Nasser, tunachunguza nini kilichotokea wakati wa mapinduzi yenyewe, vipi waliyalinda kwa kuziteka asasi za dola, na vipi kule kuwepo kwao (miongoni mwao si kama walikuwemo Waarabu wengi tu bali walikuwemo Waafrika na Wahindi vile vile) kulizuia machafuko dhidi ya Waarabu kuwa ndiyo madhumuni ya`mapinduzi.

“Palikuwepo na machafuko kila mahali,” kama anavyokumbuka Hashil Seif Hashil, aliyekuwa mjumbe wa Kamati Kuu ya Umoja wa Vijana wa Chama cha Umma (Umma Youth): ‘Watu wengi hawakujua walilokuwa wakilifanya. Jambo moja ambalo Chama cha Umma Party kilifanya lilikuwa ni kuelezea juu ya madhumuni ya mapinduzi – madhumuni yake hayakuwa kuua, kubaka au kuiba bali ni kuibadili nchi. Baadhi ya watu walielewa lakini ni wazi kuwa si kila mtu aliyeelewa’ (imenukuliwa kutoka Wilson, 1989: 12).

Kwa mtazamo wa makada wa Chama cha Umma Party, tunakiangalia vile vile kipindi cha baada ya mapinduzi, kuundwa kwa serikali mpya ya kimapinduzi ya ushirikiano kati ya Chama cha Umma Party na Chama cha Afro-Shirazi (ASP), chama kilichokuwa kimezongwa na migogoro, na miezi mitatu iliyofuatia ambayo ilimalizika kwa vitimbi dhidi ya mapinduzi. Katika kipindi hiki, chini kwa chini, Marekani na Uingereza walipanga kuivamia Zanzibar, walikula njama kumwua Babu, na walifanya kila waliloliweza kuleta mgawanyiko ndani ya serikali mpya. Mgogoro uliojitokeza ndani ya serikali ya kimapinduzi ulisababisha kuvunjwa kwa Chama cha Umma Party, lakini makada wake waliendelea kuwa pamoja na kushirikiana katika mambo mengi wakiwa kama ni kundi moja.

Marekani na Uingereza, hatimaye walifanikiwa ‘kuidhibiti’ Zanzibar na kuivuruga ari yake ya kimaendeleo kwa kuchochea muungano wa Zanzibar na Tanganyika ili kuunda nchi mpya, Tanzania, na raisi wake akiwa ni mtu wanaeweza kumwamini na mfuasi wa nchi za magharibi, Nyerere. Ni muungano uliopatikana kwa njia za hila, bila kufuata taratibu za kisheria zinazokubalika na bila ya kuwashauri wananchi wa nchi yoyote kati ya nchi mbili hizo. Ulianzishwa kwa njama za viongozi wanaopendelea nchi za magharibi wa Tanganyika, Kenya na Uganda.

Hali ya Zanzibar iliporomoka hususan baada ya muungano, na Karume, kiongozi wa ASP alianza kuvitawala visiwa hivyo kama kwamba visiwa hivyo ni mali yake binafsi, akiua, akitesa na kuwafunga gerezani wote wale wasiokubaliana na sera zake na kumpinga. Tunaiangalia miaka hii ya mateso kufuatana na masahibu yaliyowafika baadhi ya makada wa Chama cha Umma Party – wale waliofungwa gerezani na kuteswa Zanzibar na halikadhalika Bara.

Muungano uliandaliwa na kutekelezwa kwa siri lakini kwa kiasi kikubwa mchakato wa kuundwa kwake uliratibiwa kwa makini na Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, ambao nyaraka zao zimefichua sio kiasi cha dharau ya Wamarekani kwa viongozi wa Afrika tu bali pia kiwango cha uongo na ufidhuli wao. Si kama walipanga mauaji tu lakini vile vile waliwahonga na kuwajenga watu kama Nyerere ambao waliweza kuwadhibiti. Kwa mfano, mwezi Januari 1964, siku nane tu baada ya mapinduzi, G. Mennen Williams, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani anayeshughulikia Afrika ya Mashariki, katika waraka wa siri, alimweleza Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, ‘Kazi yetu kubwa ni kumjenga Nyerere …. Nyerere atahitaji vitu fulani vya mpango mpya ili kuimarisha madaraka yake’ (nukuu kutoka kwa Wilson, 1989:27).

Hivyo ndivyo hofu ilivyokuwa imetanda katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani kufuatia mapinduzi katika visiwa hivi vidogo, kiasi kwamba mnamo wiki chache tu Marekani ilimpeleka Zanzibar mmoja wa majasusi wake mwenye uzoefu mkubwa kutoka Shirika la Ujasusi la Marekani, Frank Carlucci, ambaye baadae alikuwa Waziri wa Ulinzi katika Serikali ya Ronald Reagan. Aliwasili moja kwa moja kutoka Kongo ambako Shirika la Ujasusi la Marekani lilikuwa limehusika sana katika kumpindua Lumumba. Kwa maneno ya Carlucci mwenyewe, Marekani ilibidi iwadhibiti waumini wa usoshalisti wa Zanzibar kwasababu ‘kama usingelikuwepo muungano, Zanzibar ingelikuwa Cuba ya Afrika na kutoka Zanzibar uasi ungelienea Bara zima’ (Imenukuliwa kutoka katika Wilson, 1987). Kwa kufuata ile sera iliyokuwepo kabla ya sera ya hivi sasa ya Kikosi cha Marekani katika Afrika (AFRICOM), Marekani ilianza kuandaa ule mkakati ulioitwa ‘eneo la udhibiti’ ambao ndani yake Afrika ya Kati na Afrika ya Mashariki (pamoja na Zanzibar) zingewekwa chini ya udhibiti wake, ili kuzuia ushawishi wa kisoshalisti kutoka Afrika ya Kaskazini usizifikie nchi za Kusini mwa Afrika na kuhatarisha rasilimali zao zilizowekezwa na nchi za magharibi.

Nyaraka zilizowekwa bayana za mawasiliano ya simu za upepo za Marekani na hati za serikali ya Uingereza kuanzia miaka ya 1960 na zile za miaka michache iliyopita zilizofichuliwa na Wikileaks zinaonyesha namna fulani ya mwendelezo na tofauti zake. Kuna aina ile ile ya mfululizo wa ukusanyaji wa habari za kijasusi (ila vyanzo vya hivi sasa haviishii na wanasiasa tu bali pia vinashirikisha maafisa wa kijeshi wa Tanzania na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali); ni wasiwasi ule ule kuhusu vijana, ambao katika miaka ya 1960 wamekuwa ‘wakifanya mazoezi na kupata mafunzo kwa kile kinachoweza kuelezwa kuwa mafunzo ya ushujaa wa kijeshi’ (HMSO, 1961: 3) na hivi sasa, kwa mujibu wa simu za upepo za Marekani, wanahusika na ‘kelele za hasira’ ‘zinazohitaji kuangaliwa kwa makini’ (Ubalozi wa Marekani, 2006b) na hofu ni ile ile ya Zanzibar kuwa sehemu ya mtandao wa maadui wa Marekani. Ila sasa mazimwi ni tofauti; wakati kwanza huko nyuma walikuwa Wakomunisti, sasa ni ‘Magaidi wa Kiislamu’.

Hebu linganisha, kwa mfano maelezo ya Carlucci yaliyopo hapo juu na wasiwasi huu wa Ubalozi wa Marekani uliopo Dar es Salaam, uliomo katika waraka wa siri wa kisera wa mwezi Julai 2008.

Wazanzibari ni miongoni mwa wanachama wa al-Qaeda (sic) waliohusika na mashambulizi ya ubalozi huu mwaka 1998. Kuna vikundi vya wanaowaunga mkono wenye siasa kali katika kanda yote ya utamaduni wa Mswahili (mwambao wa Kenya na Tanzania, Zanzibar na visiwa vya Ngazija vyenye kuzungumza Lugha ya Kiswahili). Kundi la vijana wa Kiislamu wasiokuwa na kazi, waliokata tamaa, wasio na matumaini yoyote, walio na hasira, waliotengwa, ambao magaidi wanaweza kuwaandikisha wawe miongoni mwao ni kubwa zaidi Zanzibar kuliko mahali pengine popote katika eneo la utamaduni wa Mswahili. Mahusiano ya kifamilia na ya kibiashara katika eneo la Waswahili ni ya namna ambayo, matokeo ya jambo lolote katika sehemu moja huwagusa wa sehemu nyengine katika eneo hilo. Kuongezeka kwa watu wenye siasa kali Zanzibar kutawaambukiza watu wa eneo lote.  (Ubalozi wa Marekani, 2008a)

Taswira ya vita baridi ilimaanisha kuwa Marekani iliamini kwamba China, au ‘Chicoms’ kama Wamarekani walivyowaita Wachina, ilihusika na kila mabadiliko ya hali ya hewa.

China ya wakati huo ilikuwa ni nchi tofauti sana na ilivyo hivi sasa. Ilitoa ilhamu na kuwa mfano kwa nchi zilizokuwa zikiendesha mapambano dhidi ya ukoloni katika Afrika na Asia. China, ‘kwa juhudi zake yenyewe’, kama alivyoandika Babu, na ‘dhidi ya matatizio yote, imeibuka kuwa miongoni mwa washindani wa uongozi wa dunia. Ilichochea hisia zote za furaha na matumaini kwa wanaokandamizwa ambao bado walikuwa wakipambana katika hali ya shida kubwa’ (Babu, 1996:327).

Uzoefu wa China umebainisha kuwa kuna haja ya kuwepo kwa uzalendo wa kiuchumi na mkakati mkubwa na mpana wa kujenga uchumi wa kujitegemea (fikra ambazo bado zinafaa katika zama hizi za vita vipya vya kikoloni). Walishawishi kuwepo kwa sera ya kuwa na uchumi wa kujitegemea ambayo ilikuwa katika hatua za kutekelezwa Zanzibar pale kundi la wapinga mapinduzi walipoubuni Muungano.

Hata hivyo, China juu ya ushawishi wake, haikuhusika moja kwa moja na machafuko hayo, na kama zile silaha za maangamizi zilizoshindikana kuonekana nchini Iraq, Marekani ilitafuta na kutafuta lakini haikuweza kupata silaha zozote za Kichina. Hata hivyo, waliambiana wenyewe kwa wenyewe katika mawasiliano ya siri kuwa ‘Ijapokuwa haukupatikana ushahidi wenye uthibitisho, ushahidi wa kimazingira wa kuhusika kwa Chicom katika machafuko ya Zanzibar … unadhihirisha waziwazi kushiriki kwa Chicom katika kutoa fedha na kuandaa mipango ya maasi hayo … bado hakuna ushahidi madhubuti ‘ ( imenukuliwa kutoka Wilson, 1989: 37)

Hofu ya Marekani ya kuuogopa ushawishi wa China haikutoweka. Kusema kweli, imerudi kwa nguvu ikiwa na umbo jipya wakati China na Marekani wanashindania rasilimali za Afrika, hasa mafuta.

Mpaka hivi sasa China imekuwa tayari kupata rasilimali zake kwa njia ya biashara, kwa kutoa bidhaa za viwanda vidogo kwa kubadilishana na malighafi, na ujenzi na uendelezaji wa miundombinu – kama vile njia za reli na madaraja ili kuuwezesha utaratibu huu kuendelea.

Hivi sasa mkakati wa Marekani katika Afrika ni tofauti kabisa. Umekuwa ni pamoja na uvamizi wa kijeshi, kuziondoa serikali madarakani na kuweka au kuimarisha serikali zinazoipendelea Marekani (kama ile ya Tanzania) zinazosaidia unyonyaji wa rasilimali kwenda Marekani na Ulaya. Hata hivyo, jeshi la Marekani katika Afrika linataka lionekane kuwa ni jeshi la ‘kirafiki’. Nchini Tanzania kwa mfano, waraka wa siri wa Ubalozi wa Marekani mwezi Juni 2009 umeeleza kuwa, kiasi cha miaka mitatu iliyopita serikali ya Tanzania ilikubali kuanzishwa kwa Kikosi cha Kiraia katika Mwambao wa Waswahili chini ya usimamizi wa Kikosi Kazi cha Pamoja cha Marekani – Pembe ya Afrika. Kikosi hiki cha kiraia ambacho tumekipa jina jingine la Kikosi cha Marekani katika Afrika (AFRICOM) kinaendesha miradi ya kibinaadamu na kusaidia katika kujenga uwezo wa Shughuli za Kijeshi na za Kiraia (CMOs) za Jeshi la Wananchi wa Tanzania.’ (Ubalozi wa Marekani; 2009a).

Shughuli za Kijeshi na za Kiraia ni pamoja na jeshi la Marekani kufanya kazi pamoja na serikali na Mashirika yasiyo ya Kiserikali (angalia ukurasa wa 140) kufanya upelelezi, utekaji nyara, utesaji na shughuli mbalimbali za kijeshi za kushughulikia ushindani mkali/unyonyaji wa rasilimali zinazoendelea kupungua na changamoto nyingine zinazoweza kujitokeza dhidi ya Marekani. (Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la pamoja la Marekani, 2008).

Kitengo cha Utafiti cha Bunge la Marekani kinatupa habari nyengine za ziada kuhusu ‘jina’ AFRICOM. Likiwa ni shirika linalounganisha na kuratibu shughuli za jeshi la Marekani barani Afrika, AFRICOM ilianzishwa mwaka 2008 chini ya Utawala wa Bush ili ‘kuendeleza madhumuni ya usalama wa kitaifa ya Marekani katika Afrika na bahari zinazolizunguka bara hilo. Hii inadhihirisha wazi mtazamo wa kikoloni katika Afrika, kama ilivyoelezewa katika Mkakati wa Usalama wa Kitaifa wa Bush wa 2002: ‘Katika Afrika ahadi na fursa ziko bega kwa bega na maradhi, vita na umasikini wa kukatisha tamaa. Hili ni tishio maradufu kwa tunu za Marekani – yaani kulinda heshima ya binadamu – na kipaumbele chetu cha kimkakati – kupambana na ugaidi wa kimataifa’ (Bush, 2002).

Hata hivyo, ijapokuwa imedhamiriwa ‘kupambana na ugaidi wa kimataifa’, moja ya madhumuni makubwa ya AFRICOM ni kuudhibiti ushawishi wa Wachina, kuizuia China isipate mafuta na rasilimali nyengine, na kuzichukua kwa ajili ya kuzipeleka Marekani. Hilo ndilo walilokuwa wakilifanya Marekani huko Libya (Engdahl, 2011).

Kama alivyoandika Patrick Henningsen:

Vita vya makampuni ya kimataifa, vya kugombania umiliki na udhibiti wa rasilimali za dunia zilizobaki na utoaji wa nishati…. vitapiganwa kupitia mawakala wengi, na katika medani zilizoenea sehemu mbalimbali duniani lakini hilo halitasemwa na Waziri wa Habari wa Ikulu ya Marekani wala na Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza. (Henningsen, 2011)

Badala yake, kitakachoelezwa yatakuwa ni maelezo ya taswira za uongo zitakazolazimisha uingiliaji kati wa Marekani kwa ‘sababu za kimaadili’, kwa mfano ‘uingiliaji kati kwasababu za kibinadamu’ kama ilivyokuwa kwa uvamizi wa Libya na kabla ya hapo Somalia, kutokomeza silaha za maangamizi ya halaiki na kuleta demokrasia kama ilivyokuwa Iraq na zaidi hivi karibuni Iran, au kuhalalisha vita dhidi ya ugaidi kama ilivyo Afghanistan na Somalia hivi sasa.

Ni kwa mukhtadha huu wa mwisho ndiyo Zanzibar inaonekana kuwa ni sehemu ya kanda ya kimkakati, kuanzia kwenye pembe ya Afrika na Rasi ya Arabuni hadi Ethiopia na visiwa vya Shelisheli kwa kupitia Kenya. Hapa ndipo vita dhidi ya ugaidi vinapoendeshwa kwa miongo michache iliyopita, na kuna kila uwezekano wa vita hivyo kuongezeka. Ni katika eneo hili la nchi zinazopakana na Bahari ya Hindi ndimo vituo vya siri vya ndege zinazoruka bila ya rubani vinamojengwa (Channel 4 News, 2011) ili kuilenga nchi yoyote ya Afrika ya Mashariki ambayo haitairuhusu Marekani kuzipata rasilimali zake. Kutoka hapa ndipo ndege hizi zisizokuwa na rubani zinapoanzia kuruka na kulizunguka bara zima la Afrika ili kuwalenga wananchi wasiokuwa na silaha, zikiua wanaume, wanawake na watoto ambao majina yao husahauliwa hivi hivi na ambao vifo vyao si chochote ila ni vifo vya ‘raia tu wakati wa vita’: kwa mfano, angalia Press TV (2012).

Takriban kila nchi katika Afrika ya Mashariki ina utajiri wa rasilimali ambazo Marekani inazitafuta. Hivi sasa ni Somalia (ambayo ina vitalu vya mafuta na madini ya urani) ambavyo vinalengwa katika mashambulizi ya awamu ya pili, kesho inaweza kuwa Sudan kwa mara nyengine, katika mzunguko wa pili, na labda baadae siku za mbele inaweza hata ikawa Zanzibar kwa rasilimali zake za mafuta na gesi. Katika miaka ya 1990 yaliyotendeka Somalia yalichukuliwa kuwa yanahusiana na msaada wa kibinadamu kwa waathirika wa njaa, msaada ambao ulikuwa ukizuiliwa na ‘wababe wa kivita’. Leo ni kuhusiana na ugaidi unaofanywa na al-Shabaab; kesho itakuwa ni kikundi tofauti cha kigaidi. Vita dhidi ya ugaidi siku zote huweza kuwaona ‘magaidi’ kila pahala. Wanaweza kuwa ni watu wa kawaida wanaoendelea na shughuli zao ambazo zinazuia wizi wa makampuni ya kimataifa, au yanaweza kuwa ni mashirika yanayomea chini ya mwavuli wa ubeberu – na kusababisha hasira za umma dhidi ya dhulma zake au baadhi ya wakati kushajiishwa na kuanzishwa na ubeberu wenyewe, lakini mara zote katika maeneo yenye utajiri wa rasilimali.

Barak Obama aliweka wazi katika utangulizi wa taarifa yake juu ya punguzo la matumizi ya ulinzi kwamba “njia za upatikanaji” ndicho kile ambacho Marekani inachotaka. ‘Wakati tunayaunda upya majeshi yetu tuta endelea kuwekeza katika kuyawezesha yale yaliyo muhimu kwa mafanikio yetu ya siku za usoni, ikiwa ni pamoja na ujasusi, upelelezi, mapambano dhidi ya ugaidi; kupambana dhidi ya silaha za maangamizi ya halaiki, kufanya shughuli dhidi ya mazingira yanayotuzuia’ (Wizara ya Ulinzi ya Marekani 2012). Taarifa yake juu ya ‘punguzo la matumizi ya kijeshi’, inathibitisha vile vile ‘ushirikiano wa kimkakati’ na majeshi ya Afrika. Hii ina maana kuwa vita katika Afrika vitaendelea kupiganwa kwa kuyatumia majeshi ya nchi kama vile Ethiopia, Kenya na Tanzania, bila ya kuwepo kwa upinzani mkubwa dhidi ya ubeberu, tutayaona zaidi ya haya siku za usoni, na watakuwa Waafrika ndio wanaouliwa na wanajeshi wa Kiafrika wanaoua na kufa ili kulinda rasilimali kwa ajili ya Marekani.

Kuhusu vita dhidi ya ugaidi, vita hivi vimeonyesha kuwa na manufaa kwa Marekani na haviwezi kuachwa. Taarifa ya Obama inaweka wazi kuwa vitaendelea – na kutekelezwa, kwa njia kama tujuavyo za ‘kurejesha wahalifu’ ‘mauaji’ na ‘mauaji ya kuwalenga watu mahasusi’. Tanzania (kama ilivyo Kenya) imethibitishwa kuwa haya yanafanyika na serikali ya Kikwete ikiwa inahusika kikamilifu kwa zaidi ya mwongo mmoja sasa. Kuanzia mwaka 2003 serikali imekuwa ikifanya vitendo vya utekaji nyara na kurejesha wahalifu kwa amri ya Marekani. Tukio moja la kushtua la mtu aliyetekwa nyara, akasafirishwa kwa ndege kuzunguka dunia nzima mpaka kwenye eneo moja la Shirika la Ujasusi la Marekani lijulikanalo kwa jina la ‘maeneo meusi’ (Interights, 2011), akateswa na kuachiwa miaka mitatu baadae, bila ya kufunguliwa mashtaka, hivi sasa lipo kwenye Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Haki za Raia. Pale ambapo vitendo kama hivi vimefichuliwa hadharani, maafisa wa Kimarekani huvihalalisha kwa kutoa sababu za kupambana na ugaidi Afrika ya Mashariki unaohusisha sio kurlipuliwa kwa ubalozi wa Marekani Dar na Nairobi tu (kitendo kinachoaminiwa kuwa ni ulipizaji wa kisasi kwa kuhusika kwa Marekani katika kurudishwa, na tuhuma za kuteswa kwa wanachama wanne wa chama cha Egyptian Islamic Jihad waliokamatwa nchini Albania), lakini pia katika kipindi cha miaka michache iliyopita, kwa vitendo vya al-Shabaab.

Kuundwa kwa Tanzania kulikofanywa na Uingereza na Marekani kumeifanya Zanzibar irudi nyuma nusu karne nzima na katika kipindi hicho kuingizwa katika sehemu ya Tanzania Bara (iliyokuwa nyuma haijaendelea) na serikali yake (kuchangia zaidi katika) kuivunja nguvu kazi yake ya uzalishaji. Tokea kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa nchini Tanzania mwaka 1992, vyama vikubwa viwili vya Zanzibar ambavyo wafuasi wake wanatoka katika kundi hilo hilo la wapiga kura, kama walivyokuwa wanatoka katika pande mbili zilizokuwa zikipingana katika miaka ya 1950 na kusababisha kutokea mapinduzi ya 1964 wameendelea kupingana kama zamani. Hata hivyo, hivi sasa wameungana katika serikali ya umoja wa kitaifa. Lakini serikali kama hiyo ina maana gani katika hali kama hii, na kwa nini Marekani na Ulaya walizibembeleza na kuzitishia pande mbili zinazopingana kuianzisha? Nini sababu ya uingiliaji kati huu wa kisiasa na kidiplomasia wa nchi za Magharibi? Kama nyaraka za Wikileaks zinavyoonyesha, ulifanywa ili kupunguza makali ya tishio dhidi ya udhibiti wa kibeberu lililokuwa likiashiriwa kutokana na hasira za wanaokandamizwa, wasiokuwa na kazi na vijana wasioona hatma yoyote. Kwa maneno mengine, ulianzishwa ili kujenga mazingira tulivu Zanzibar na Tanzania Bara, ambako makampuni ya kimataifa yataweza kufanya shughuli zake na kupora utajiri wa rasilimali za sehemu hii ya Afrika.

Wakati tunakwenda mitamboni, Zanzibar ipo katika kipindi kigumu wakati muundo wa Muungano unajadiliwa siyo na wanasiasa tu, bali hata na watu wa kawaida pia watakuwa na kauli. Vijana na wanaharakati wa Zanzibar walio katika mapambano wanaitaka Zanzibar ya namna gani? Sauti zao zitasikilizwa? Historia ya Zanzibar katika kipindi cha nusu karne iliyopita inaonyesha mambo mawili ya kimsingi. La kwanza ni haja ya kuwa na umoja wa dhati ambao utaondoa shaka baina ya watu zilizoikumba Zanzibar na kwa hivyo kuanza ujenzi wa siasa mpya. La pili ni mwamko wa kisiasa na upinzani dhidi ya ubeberu na vita vyake na uporaji wake usiokuwa na huruma. Katika visiwa hivi, kama ilivyo pengine popote katika Afrika, ubeberu umepingwa hapo kabla. Leo unaweza kupingwa na lazima upingwe tena.

License

Tishio la Ukombozi Copyright © 2016 by Amrit Wilson. All Rights Reserved.

Share This Book

Feedback/Errata

Comments are closed.